Tuesday 3 September 2013

Tanzania yatoa tamko juu ya Rwanda kuongeza tozo ya ushuru wa barabara.


                               
 Siku moja baada ya serikali ya Rwanda kupandisha tozo ya ushuru wa barabara yaani Road toll kwa takribani asilimia  200 kwa magari yaliyosajiliwa Tanzania na kudaiwa kusababisha adha kubwa kwa wafanyabiashara mpakani mwa nchi hizo katika eneo la Rusumo Wilayani Ngara serikali ya Tanzania nayo imetoa ufafanuzi wa suala hilo huku serikali ikitakiwa kutoa maelezo ya kina bungeni juu ya mgogoro wa wafanyakazi wa Tazara.
Nje ya bunge akilitolea ufafanuzi suala hilo naibu waziri wa uchukuzi Mh Charles Tizeba amesema suala hilo kwa mara ya kwanza liliibuka katika mkutano wa nchi za Afrika ya Mashariki uliofanyika nchini Rwanda ambapo nchi hizo zilikubaliana kutoza tozo zinazofanana na kwamba mchakato huo unaendelea.
Kuhusiana na kuongezeka kwa tozo hiyo naibu waziri huyo amesema baada ya kupata taarifa hizo kwa haraka  amewasiliana na waziri wa miundo mbinu wa Rwanda aliyemtaja kwa jina la Prof Rwakabamba ambaye amekiri uwepo wa hatua hiyo ya kupandisha tozo hiyo kutoka dola za kimarekani 152 hadi kufikia dola za kimarekani 500 kwa magari yaliyosajailiwa Tanzania na kwamba agizo hilo limetolewa na waziri wa fedha wa Rwanda kwa mdomo na kuelezea hali ilivyo sasa.
Ndani ya bunge, baada ya kamati za bunge za uongozi na kanuni kukutana hatimae bunge limeitaka serikali kutoa maelekezo ya kina kuhusiana na suala la mgogoro kati ya wafanyakazi wa shirika la reli ya Tanzania na Zambia Tazara ndani ya bunge kwa kueleza kiini cha mgogoro huo na hatua gani madhubuti zimechukuliwa kuutatua kabla ya mkutano huu wa 12 wa bunge kumalizika.
Katika hatua nyingine kwa siku ya pili bunge limeendelea kuujadili ili kuupitisha muswaada wa sheria ya vyama vya ushirika ya mwaka 2013 huku kukiwa na malumbano makali kwa wabunge bila ya kujali itikadi yao ya vyama kutuhumiana kwa kuhusika katika ubadhirifu ama matumizi mabaya ya fedha za ushirika katika maeneo ambayo wamewahi kuwa na nyadhifa,huku suala la uwepo wa chama kilele yaani appex likipigiwa upatu wa kufutwa kwa madai ya kuwanyonya,kuwakandamiza wakulima sambamba na kuongeza gharama za uendeshaji kwa ushirika.

Source: ITV daima-IPPMEDIA