Dodoma jana. Picha na Fidelis Felix
Kwa ufupi
Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya
Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa
wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni
mgongano.
Dodoma. Muswada wa Sheria ya
Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika mkutano wa 12 wa
Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa utajadiliwa Bunge
lijalo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema
kwamba kuahirishwa huko kumetokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba,
Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya
maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.
Muswada huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika
kikao cha Bunge kinachoendelea ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
“Ukisoma huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa
Tanzania Bara na Zanzibar sasa sheria hii ina apply vipi (inatumikaje)
Zanzibar wakati kule tuna sheria yetu tayari?” alihoji Mbunge mmoja wa
Zanzibar.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana,
alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na
utakaojadiliwa ni ule wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.
“Bunge litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni
kweli huo Muswada wa Kura ya Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko
kwenye ngazi ya kamati,” alisema Joel.
Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa muswada ambao
ulishaingizwa kwenye ratiba ya Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.
“Ni kweli muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili
bado kuna mashauriano yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo
waliokwamisha muswada huo kutokana na mgongano wa sheria.
“Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya
Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa
wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni
mgongano,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), alisema tangu mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha
Kamati ya Bunge kwamba mapendekezo hayo yana upungufu.
Muswada pekee uliobaki wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba unatarajiwa kuwasilishwa leo huku ukitarajiwa kuibua mjadala
mzito kutokana na misimamo ya baadhi ya wabunge.
Muswada huo unawasilishwa wakati CCM kikiwa kimeweka msimamo wa kupinga baadhi ya mambo katika Rasimu ya Katiba.
Yanayotarajiwa kuzua mjadala
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
amekiri kupokea mapendekezo kutoka kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya
Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba akisema wametaka kuangaliwa upya kwa
kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema
sasa wataweka sifa za mwombaji wa nafasi hizo na wasiokuwa nazo
hawatagombea.
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unataka
wawakilishi kutoka makundi ya jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba,
lakini wabunge wanataka idadi iwe 200.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi)
alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha kuwa mabunge ya Katiba
hushirikisha watu wengi ili kupata uwakilishi mpana tofauti na
mapendekezo yaliyotolewa.
Mkosamali ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema
wajumbe wa Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.
Kifungu kingine ni kile kinachohusu Kamati ya
Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa
na Spika wa Bunge la Jamhuri na Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na
yule wa SMZ, Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Bara na Waziri wa
Katiba na Sheria wa Zanzibar na Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni.
Mkosamali alisema muswada huo wa Mabadiliko ya
Katiba unasema mwenyekiti wa muda atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka:
“Mwenyekiti wa muda atokane na Chama cha Majaji wastaafu maana wao
hawafungamani na upande wowote.”
source: Mwananchi
source: Mwananchi