Kwa ufupi
Wataka wawili hao wafutiwe mashtaka yanayowakabili kwenye mahakama hiyo, ili kuweka uthabiti kwenye utawala wao
Nairobi. Muungano wa Afrika (AU) umeiandikia barua
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC)kuitaka kusitisha kesi za
watuhumiwa wa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 nchini Kenya.
Watuhumiwa hao ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, na makamu wake William Ruto, pamoja na mwandishi Joshua Arap Sang.
Katika barua hiyo Muungano huo uliitaka mahakama
hiyo kusitisha kesi hiyo mpaka ombi la kutaka kesi hizo kurejeshwa Kenya
litakapoamuliwa.
AU pia inataka Ruto na Rais Kenyatta kuruhusiwa
kuchagua vikao wanavyotaka kuhudhuria wakati wa kusikilizwa kwa kesi zao
kutokana na majukumu yao ya kikatiba.
Kwenye barua iliyoandikwa kwa ICC, AU ilisema kuwa
mahakama hiyo mwanzo ilipaswa kuamua kuhamishia kesi hizo nchini Kenya
kabla ya hata kuanza kuzisikiliza.
Katika barua hiyo ilidaiwa AU pia iligusia suala
la rufaa ambayo iliwasilishwa katika mahakama hiyo na mwendesha mkuu wa
mashtaka Fatou Bensouda dhidi ya kumruhusu Ruto kuhudhuria tu baadhi ya
vikao.
Muungano huo ulielezea kuhusu mikutano mikuu
miwili ya usalama inayotarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu ambayo Rais
Kenyatta hataweza kuhudhuria kwa sababu kesi ya Ruto itakuwa
inasikilizwa ICC.
AU iliongeza kuwa kesi hizo zitahujumu jukumu la
Kenya katika ukumbi wa kimataifa ikisisitiza kuwa hazipaswi kuathiri
majukumu ya viongozi hao wawili.
AU ilisema kuwa licha ya kuwa Kenya imekuwa ikiheshimu mahakama hiyo, inapaswa kufanya hivyo kwa kuzingatia Katiba yake.
Hatua hiyo ya AU ni mwendelezo wa juhudi za wakuu
wa nchi wanachama ambao walipitisha azimio la kuwalinda viongozi walioko
madarakani dhini ya ICC.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI