Saturday, 14 September 2013

Watafiti madini wajeruhiwa wakidaiwa kuwa majambazi


Na Gasper Andrew, Mwananchi

Posted  Septemba14  2013  saa 9:58 AM
Kwa ufupi
Wananchi waliwavamia Peter Lucas (30) na Edwin Rwekiza (25), wakiwa kazini na kuwapiga kwa kutumia silaha za jadi ikiwemo marungu.


Singida. Wafanyakazi wawili wa Wakala wa Jiolojia kutoka Dodoma mjini,wamepigwa na kujeruhiwa wakiwa kazini na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Irisya Tarafa ya Sepuka Wilaya ya Ikungi, kwa kuhisiwa kuwa majambazi.
Wananchi waliwavamia Peter Lucas (30) na Edwin Rwekiza (25), wakiwa kazini na kuwapiga kwa kutumia silaha za jadi ikiwemo marungu.
Wakala hao ambao wanafanya kazi chini ya Wizara ya Nishati na Madini walikuwa Singida kwa kazi ya kuchora ramani za kijiolojia na kutafiti zaidi maeneo yaliyobainishwa kuwa na dalili ya madini kupitia uchunguzi wa helikopta...
Wafanyakazi hao waliumizwa vichwani na Edwin ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma mwaka wa pili akichukua masomo ya jiolojia, amevunjika mifupa ya kichwani na hali yake ni mbaya.
Juzi jioni Edwin alisafirishwa kwa ndege kupelekwa Hospitali ya KCMC Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya matibabu zaidi. Kwa upande wa Peter, anaendelea na matibabu katika hospitali ya mkoa mjini hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Singida, Manase Mbasha alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba lilitokea Septemba 11 mwaka huu.
Alisema ofisi ya mkuu wa mkoa imewaandikia wakuu wa wilaya zote juu ya ujio wa wafanyakazi wa wakala wa jiolojia kutoka Dodoma, kufanya kazi katika maeneo yaliyobainishwa kuwa yana uwezekano wa kupatikana kwa madini mbalimbali.
“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Singidas,kurejesha utamaduni wao uliozoeleka wa kufuata taratibu,kanuni na sheria pale wanapokuwa na wasiwasi na wageni wanaoingia katika maeneo yao.
SOURCE: MWANANCHI