Kwa ufupi
Rufaa hiyo ilikatwa mara baada ya Mahakama Kuu,
Kanda ya Dodoma kutupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na wakazi
wawili wa kijiji cha Makiungu mkoani Singida, Shabani Selema na Paskali
Hallu, Aprili 27, mwaka jana.
Dodoma. Wakili wa walalamikaji katika rufaa ya
kupinga ushindi wa ubunge katika jimbo la Singida Mashariki, Godfrey
Wasonga jana alipata wakati mgumu baada ya mawakili wa upande wa
walalamikiwa kudai maombi ya kuiondoa kesi hiyo yana lengo baya na pia
hayakufuata taratibu za kisheria.
Rufaa hiyo ilikatwa mara baada ya Mahakama Kuu,
Kanda ya Dodoma kutupilia mbali kesi hiyo iliyofunguliwa na wakazi
wawili wa kijiji cha Makiungu mkoani Singida, Shabani Selema na Paskali
Hallu, Aprili 27, mwaka jana.
Walalamikiwa katika rufaa hiyo ni Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu, Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Kesi hiyo namba 49 ya mwaka jana, iliendeshwa jana
katika majengo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, chini ya jopo la majaji
watatu wa mahakama ya rufaa likiongozwa Jaji Engela Kileo.
Majaji wengine waliokuwa katika jopo hilo ni Natalia Kimaro na Salum Masati .
Katika kesi hiyo iliyokuwa na mvuto kwa watumishi
wa mahakama na wanachama wa Chadema, Wasonga aliwasilisha ombi la
kutoendelea na kesi hiyo kwa sababu walalamikaji wametaka kutoendelea na
kesi hiyo.
Alisema maombi hayo hayakufuata kifungu namba 102
cha kanuni za mahakama ya Rufaa cha mwaka 2009, ambacho kinamtaka kuleta
maombi hayo kabla ya Msajili kupanga siku ya kusikilizwa kwa shauri.
Pia aliomba mahakama iwapo italazimika kufuta kesi
hiyo basi iamue pia ni nani atalipa gharama za kesi hiyo,lakini
ikizingatia kuwa Selema alipeleka mahakamani kiapo cha kukana kumweleza
Wasonga kukata rufaa.
“Sisi tuliosumbuliwa, tutalipwa nani gharama zetu,
ninaiomba mahakama kutokubali ombi la ku- with draw (kuondoa) kesi
kwasababu limeletwa kwa nia mbaya lakini kama itaipendeza mahakama
kuondoa kesi hii basi tunaomba gharama zote azibebe Wakili msomi
Wasonga,”alisema na kuongeza.
Haitakuwa haki kuwalipisha gharama za rufaa wakati
hakupokea maelekezo kutoka kwao ya kufungua kesi. Ila kwa gharama za
mahakama ya chini walipe walalamikaji.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili wa Serikali
Mkuu, Vicent Tangoh, ambaye alisema kuwa hata kifungu cha kanuni
kilichotumika ya 102 ya Mahakama ya Rufaa, haikuwa sahihi.
Alisema kifungu hicho kinamtaka muombaji kupeleka
maombi ya kuondoa kesi kwa msajili wa mahakama na si mahakamani kama
alivyofanya Wasonga.
“Mahakama haijapewa mamlaka ya kuondoa kesi katika kifungu cha
kanuni hii, hivyo maombi yake (Wasonga) hayajakamilika,” alisema Tangoth
aliyekuwa akisaidiwa na mawakili wa serikali, Onesmo Mpinzile na Killey
Mwitasi.
Alipopewa nafasi ya kujibu hoja hizo Wasonga
alisisitiza kuwa hakuweza kuitaarifu mahakama mapema kwa sababu mteja
wake (Hallu) alimletea taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na rufaa
hiyo Septemba 6 mwaka huu, wakati ambapo tayari msajili wa mahakama
alikuwa ameshapanga tarehe ya kesi hiyo.
Hata hivyo, alivyotakiwa kueleza ni kwanini
ametumia kanuni hiyo ambayo mawakili wenzake wanasema kuwa si sahihi,
Wasonga alisema hakuna kanuni nyingine inayompa nafasi ya kuomba
kuondolewa kwa kesi inapofikia katika hatua hiyo na wakati kukiwa na
mapingamizi yaliyowasilishwa mahakamani.
Hali hiyo, ilimfanya jaji Kileo kumhoji mara
kadhaa kama jambo analolisema kama ana uhakika nalo, “ una uhakika kuwa
hakuna kanuni nyingine.”
Jaji Kileo alisema, “hatutaki hapa ustadi wala malumbano ya kisheria, tunachotaka hapa ni haki itendeke kwa pande zote mbili.”
Wakili Wasonga alisema gharama za rufaa hiyo
zitalipwa na Hullu (mlalamikaji namba mbili) kwasababu yeye ndiye
aliyechelewa kuwasilisha ombi ka kutoendelea na kesi hiyo.
Hata hivyo, kwa zaidi ya mara moja Jaji Kileo
alionyesha kukerwa na tabia ya Wasongwa kucheka wakati kesi hiyo
ikiendelea. Lakini Wasonga alimjibu, “ndio sura yangu ilivyo mheshimiwa
Jaji.”
Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Jaji Kileo
aliahiriha kesi hiyo kwa muda wa saa moja na baadaye kurejea na uamuzi
wa kuiondoa huku akiamuru gharama za rufaa kulipwa na Hullu.
Jaji Kileo aliamuru gharama za mahakama kuu kulipwa na walalamikaji wote wawili.
“Si sera ya mahakama kulazimisha kuendelea nakesi
na kukataa maombi haya (ya kuondolewa kwa kesi ), itakuwa ni
kinadharia,”alisema Jaji Kileo.
SOOURCE: MWANANCHI
SOOURCE: MWANANCHI