Saturday, 14 September 2013

‘Ushirikina China huchochea biashara ya meno ya tembo’

Na Ramadhani Hassan na Irene Mossi, Mwananchi

Posted  Septemba14  2013  saa 9:28 AM
Kwa ufupi
Akizungumza baada ya kupokea matembezi ya wanaharakati wa kujitolea yaliyoandaliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya wanyamapori Afrika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam juzi, Nyalandu alisema imani hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya tembo wa Afrika.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema imani za kishirikina zilizokithiri nchini China kwamba mtu akivaa kipande cha meno ya ndovu kinamsaidia kupata maisha mazuri, ndiyo inayosababisha kukithiri kwa biashara haramu ya tembo barani Afrika.
Akizungumza baada ya kupokea matembezi ya wanaharakati wa kujitolea yaliyoandaliwa na taasisi inayojihusisha na masuala ya wanyamapori Afrika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam juzi, Nyalandu alisema imani hiyo inachangia kwa kiasi kikubwa mauaji ya tembo wa Afrika.
Alisema imani hiyo imefanya bei ya pembe za ndovu nchini humo kuwa kubwa maradufu na kuwavutia wafanyabiashara wengi wenye mitaji mikubwa, kujitumbukiza katika biashara ambayo ina athari kubwa nchini.
Kwa mujibu wa waziri, wanaotumika ni vijana wa Kitanzania ambao hata hivyo hawanufaiki na chochote.
“Wanaonufaika na biashara hiyo haramu ni wafanyabiashara wakubwa wa hapa nchini na China pia viongozi wakiwemo wa Serikali” alisema.
Nyalandu alisema Serikali itazungumza na Serikali ya China ili kujenga ushirikiano wa kuwatangaza hadharani watakaokamatwa au kubainika wakijihusisha na biashara hiyo na kwamba mali zao pia zitataifishwa.
SOURCE: MWANANCHI