Na Kelvin Matandiko, mwananchi
Posted Septemba14 2013 saa 9:37 AM
Posted Septemba14 2013 saa 9:37 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam: Serikali kupitia Tume ya Kuratibu
na Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, imeanza kutafuta mwarobaini wa
kumaliza sakata la usafirishaji wa dawa za kulevya baada ya kuwaomba
wadau mbalimbali nchini kushiriki uchangiaji wa maoni ya kuboresha
sheria mpya.
Mbali na hilo pia imeomba mapendekezo ya kuunda
chombo maalumu na kuanzisha mahakama maalumu ya kuendesha kesi za dawa
za kulevya ili kukomesha biashara hiyo nchini.
Hatua hiyo imekuja baada ya siku kadhaa serikali
kutangaza kuanzisha chombo hicho, kutunga sheria mpya na kuanzisha kwa
mahakama inayojitegemea ili kushughulikia kesi za watuhumiwa kutokana na
ongezeko la usafirishaji na utumiaji wa dawa hizo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi
alisema tume na sheria zilizopo hazina nguvu ya kupambana na sakata hilo
kwa sasa.
“Adhabu zilizopo kwenye sheria ya sasa
haziwaogopeshi wafanyabiashara ndio sababu ya kuongezeka kwa matukio
hayo, kwa hivyo tunatoa mapendekezo ya sheria hii mpya kwa wadau ili
waweze kutoa maoni yao jinsi ya kudhibiti mitandao ya biashara hiyo,”
alisema.
Akiwakabidhi waandishi wa habari mapendekezo ya
sheria hiyo, Lukuvi alisema Oktoba 30, mwaka huu itakuwa ni mwisho wa
kupokea mapendekezo hayo kutoka kwa wadau.
Aidha, Lukuvi alisema mbali na kuwepo kwa Kikosi
Maalumu cha Jeshi la Polisi(Task Force), serikali inapendekeza kufanyika
kwa maboresho hayo ili kwenda sambamba na mazingira ya sasa.
.“Hata hiyo task force iliyopo kwa sasa
haitambuliwi kisheria katika utekelezaji wa jukumu hilo, adhabu zilizopo
zimepitwa na wakati ukilinganisha na ilivyokuwa kwa miaka ya 1995 tangu
kuanzishwa kwake, kwa hivyo tunataka kuongeza nguvu,” alisema Lukuvi.
Agosti 31, mwaka huu mshambuliaji nyota wa zamani
wa timu ya soka ya Simba na Taifa, Joseph Kaniki ‘Golota’ na bondia
Mkwanda Matumla wanashikiliwa huku Addis Ababa, Ethiopia wakituhumiwa
kusafirisha dawa za kulevya.
Kukamatwa kwao kumezidi kuongeza idadi ya
Watanzania maarufu waliotiwa mbaroni nje ya nchi katika siku za karibuni
wakituhimiwa kwa makosa hayo.
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya
Watanzania wawili, wasanii Agnes Gerald Masogange na Melisa Edward
kukamatwa kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini wakituhumiwa
kusafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150 na thamani ya
Sh6bilioni.
Aidha, tukio lingine limetokea baada ya meli ya
mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa na maofisa forodha na
askari wa doria wa Italia katika Pwani ya Sicily, Bahari ya
Mediterranean ikiwa na tani 30 ya dawa za kulevya aina ya bangi zenye
thamani ya Pauni za Uingereza 50milioni (Sh125 bilioni).
Kaniki na Matumla walikamatwa kwenye Uwanja wa
Ndege wa Bole, Addis Ababa wakati wakijiandaa kupanda ndege ya Shirika
la Ndege la Ethiopia tayari kwa safari ya kuelekea Paris, Ufaransa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI