Na Ananilea Nkya
Posted Jumatano,Septemba25 2013 saa 14:22 PM
Posted Jumatano,Septemba25 2013 saa 14:22 PM
Kwa ufupi
Nauona ujumbe huu kama ujumbe wa mtu aliaye
nyikani. Hivyo kwa heshima na taadhima nakuomba rais wangu uusome na
kuutafakari kwa jinsi Mungu anavyokujalia.
Natumaini hujambo na Mungu wetu mwema anaendelea kukujalia afya njema, furaha na amani. Hongera sana kwa ujenzi wa taifa letu.
Ninakuandikia leo hii 23/09/2013 ujumbe huu wa
wazi wenye maneno machache ambayo yalinijia akilini mwangu usiku wa
manane na nikalazimika kuamka mapema na kuyaweka kwenye kumbukumbu.
Napitisha ujumbe huu kwenye jukwaa la Mabadiliko lakini naridhia kwamba
chombo chochote cha habari kinaweza kuuchapisha, nimeridhia.
Nauona ujumbe huu kama ujumbe wa mtu aliaye
nyikani. Hivyo kwa heshima na taadhima nakuomba rais wangu uusome na
kuutafakari kwa jinsi Mungu anavyokujalia.
Rais wangu Kikwete, awali ya yote niweke bayana
kwako kwamba mimi Ananilea Nkya, sina chama chochote cha siasa
ninachofungamana nacho na wala sina mpango wowote wa kuwa mwanasiasa ama
kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa. Naridhika sana na
taaluma yangu na hakika nijuavyo mimi, wanahabari anayetambua na
kutekeleza majukumu yake kwa taifa lake, mchango wake unakuwa ni mkubwa
pengine kuliko mchango wa mtu mwingine yeyote katika nchi yake.
Rais wangu, ujumbe wangu ni mfupi tu, kwamba
tulipofika sasa kama nchi, hakuna Rais awe kupitia Chadema, CCM,
NCCR-Mageuzi au chama kingine chochote atakayeweza kuivusha nchi hii
2015 kwa hali tuliyofikia sasa.
Mwanasiasa pekee mwenye UWEZO na MAMLAKA ya
kuivusha nchi hii tuweze kubaki salama kama taifa moja la watu
wanaopendana kwa dhati ni wewe peke yako.
Rais wangu Kikwete, kwa maono niliyoyapata usiku
wa kuamkia leo, nakuona ukiivusha nchi yetu hii kwa kujitoa mhanga ili
ipatikane KATIBA MPYA YA UKWELI itakayondoa mamlaka mikononi mwa mtu
mmoja mmoja au chama kimoja kimoja na badala yake kurejesha mamlaka
mikononi mwa umma wa Watanzania, ili tuepuke balaa la umwagaji damu
linaloinyemelea nchi yetu tuendako.
Rais wangu Kikwete, mimi ni ndugu yako wa ukweli.
Ni Mtanzania ninayeipenda na kuithamini sana nchi yangu na wananchi
wenzangu. Nakuomba ufungue macho yako ya rohoni uione TUZO YA DUNIA YA
UTUMISHI ULIOTUKUKA inayokuja taratibu kwako kutokana na utumishi wako
ukiwa Rais wetu.
Hata hivyo, Rais wangu Kikwete, ukiwasikiliza
wasioithamini Tanzania na roho za Watanzania wenzao, watu wenye fikra
kwamba chama cha siasa ni zaidi ya nchi na kufanya mambo yanayotoa dhana
kwamba CCM ni zaidi ya Tanzania na kwamba bila CCM kutawala hakuna
Tanzania, nishani hiyo itakuponyoka na hakika mimi nitasikitika sana.
Rais wangu Kikwete, nakutia shime, songa mbele kwa UJASIRI upate
kuifikia na kuipokea nishani yako, Tanzania tujulikane duniani kote na
heshima yetu ipande juu kama nchi ya mfano inayoweza kufanya mabadiliko
yake ya ukweli kwa amani, furaha na mshikamano.
Siku hiyo ya wewe utakapokuwa unapokea nishani
hiyo, mimi Ananilea Nkya, ni mmoja wa Watanzania watakaobubujikwa na
machozi ya furaha kwa kuifikisha TANZANIA kwenye USHINDI.
Binafsi, Rais wangu Kikwete, ninakuamini na
kukuthamini sana maana ninakujua tangu zama ukishiriki nasi harakati za
ukombozi wa wanawake kimapinduzi pale kwenye matamasha ya jinsia ambayo
yalikuwa yanaandaliwa kwa pamoja kati ya Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP) kwa kushirikiana na mashirika washirika wa FEMACT. Nakujua
uhalisia wako unapoamua kusimamia jambo, linatoka. Mungu akubariki sana
na aendelee kukutunza na sote tuendelee kuombeana.
Mimi kwa sasa niko masomoni, ninaamini Mungu akitujalia tutaonana siku hiyo ya TUZO au kwenye harakati ukistaafu.
Wasalaam, Ananilea Nkya
SOURCE: MWANANCHI
Wasalaam, Ananilea Nkya
SOURCE: MWANANCHI