CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kujiuzulu kwa kushindwa kulipa madeni ya walimu nchini.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana pia ametoa muda wa miezi sita kwa Waziri huyo na Naibu wake Philip Mulogo kutekeleza hilo agizo hilo vinginevyo chama kitawatumia wabunge wake kuwatimua kwa nguvu.
Kwa mujibu wa taarifa za madeni zilizokusanywa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), hadi sasa walimu wanadai malimbikizo yao ya Sh bilioni 49 ambayo hajalipwa na Serikali.
Kinana alikuwa akihutubia mikutano ya hadhara jana katika wilaya za Bariadi na Busega.
Alisema CCM haiko tayari kuona walimu wakinyanyaswa wakati wana madai ya msingi.
Hivi sasa imejengeka tabia kwa baadhi ya mawaziri na watendaji wa wizara ya kuwadharau walimu na hata kuwanyanyasa huku wengine wakishusha utu na heshima ya walimu kwa kuwatukana, alisema.
Kinana ambaye yupo katika ziara ya mikoa ya Kanda ya Ziwa alisema kwa mawaziri kushindwa kutatua kero za walimu, imefika wakati wahusika waondoke wenyewe na wasipofanya hivyo chama kitawaagiza wabunge wake wawafukuze kwa nguvu.
“Ninatoa muda wa miezi sita kwa Waziri wa Elimu na wasaidizi wake wakiwamo watendaji kuhakikisha wanalipa madeni ya walimu haraka. Haiwezeni hii ni nchi ya watu wote wakiwamo walimu wadharauliwe na hata kunyanyaswa kwa maneno ya matusi
“Hili hapana CCM haiko tayari kuona walimu kila siku wakipigwa danadana kutokana na uzembe wa watu waliokabidhiwa dhamana za kuongoza sekta ya elimu katika nchi yetu,” alisema.
MTANZANIA ilimtafuta Katibu Mkuu wa CWT, Ezekiah Oluoch ambaye alisema hadi sasa madeni ya walimu yamefikia Sh bilioni 49 ambayo ni malimbikizo ya mishahara na mapunjo.
“Kila mara tunawaambia kuwa ni vema Serikali itafute Sh bilioni 100 katika fungu la dharura ili iweze kulipa madeni ya walimu na iachane nao lakini hawasikii,” alisema Oluoch.
Source: Mtanzania Kupitia Jamii forum
TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO TASAO