Saturday 21 September 2013

CUF yataka wahamiaji haramu wafukuzwe Z’bar



Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Uenezi na Mawasiliano wa CUF, Umma Salim Bimani
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimeitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushughulikia kwa haraka suala la wahamiaji haramu visiwani Zanzibar kama inavyofanyika Tanzania Bara. Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Uenezi na Mawasiliano wa CUF, Umma Salim Bimani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, Vuga Wilaya ya Mjini Unguja. Alisema suala la uhamiaji haramu Zanzibar limekuwa sugu kwa vile watu huingia nchini bila ya kuzingatia kanuni na taratibu za sheria, huku mamlaka husika zikionekana kufumbia macho suala hilo.

“Suala la kuwahamisha wahamiaji haramu lisiishie Tanzania Bara. Tanzania ni muungano wa nchi mbili za Tanzania Bara na Zanzibar,’’ alisema.

Hata hivyo, alisema Zanzibar ni kisiwa, endapo watuwataachiwa na kuingia bila ya sababu maalumu inaweza ikaathirimiundombinu mbalimbali ukiwamo uchumi, siasa, jamii na utamaduni wa Zanzibar.

Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Hamad Masoud alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa makini kuhusu utoaji wa taarifa zake kwa umma.

Aliyasema hayo kutokana na matamshi ya hivi karibuni ya Kamishna wa Polisi, Mussa Ali Mussa kwamba wamekamatwa watu 15, watatu wakiwa ni watu wanaojihusisha na kundi la ugaidi la al-shabab.

Alisema kauli hiyo haipaswi kutolewa kwa vile inaweza kuleta athari kwa nchi na taifa zima.

SOURCE: MTANZANIA