Kuna
msemo wa Kiswahili usemao ‘akipenda chongo huita kengeza’. Nimetoa
msemo huu kwa nia njema tu ya kutaka kuangalia matukio kadhaa ya vurugu
au ghasia, yanayotokea mara kwa mara hapa nchini na kusababisha baadhi
ya watu wanaokuwa maeneo ya matukio kuumia, kujeruhiwa na wengine
kupoteza maisha yao.
Matukio ni mengi tunayasikia au kushuhudia yanapotokea kwenye michezo,
mikutano, mihadhara ya dini, maandamano na vikao mbalimbali vya siasa,
utawala na sheria. Matukio yote hayo yanapotokea husababishwa na watu
wakiwa na sababu zao za kukubali au kukataa jambo au neno fulani -- iwe
la ukweli, uonevu, dhuluma, ubabe, ubinafsi, sifa, mbwembwe au madaraka
-- kutendwa dhidi ya watu wengine.
Unapotokea
mgongano huo wa mawazo kati ya wanaotaka kutenda na wasiotaka
kutendewa, ndipo tafrani ya maneno makali, matusi, ugomvi, vurugu au
ghasia hutokea na watu kuumizana bila kwanza kutafakari madhara ya
kupenda chongo kuita kengeza. Ila tafakuri hiyo hujitokeza baada ya watu
wamekwishavurugana na kuumizana.
Chongo
ni hali ya kuwa na jicho moja. Kengeza ni jicho lenye mboni iliyokwenda
upande (macho makengeza). Ukweli, kuna mtu ana jicho moja, lakini wewe
kwa kumpenda huyo chongo, unasema hana chongo ana makengeza. Mtu
anapenda jambo fulani au kundi fulani.
Ukweli,
jambo au kundi hilo lina makosa, wewe bado utalipenda na kulitetea
katika makosa yake japokuwa unatambua kuwa jambo au kundi hilo lina
makosa. Kwa desturi watu hawapendi chongo wanapenda makengeza.
Tunashuhudia
wakulima wanavyogombana na ndugu zao wafugaji kuhusu maeneo yapi ya
kilimo na yapi ya ufugaji. Wakulima wanalia mazao yao shambani yanaliwa
na kuharibiwa na mifugo inayochungwa katika mashamba yao. Wasuluhishi wa
migogoro kama hiyo wanasema kuwa wafugaji wakachungie wapi, wakati hii
ni nchi yao! Wote hao wanapokaidi kufuata taratibu wanaingia katika
vurugu na ugomvi.
Wachimba
madini wadogo nao wanalia na kusema kuwa wananyang’anywa maeneo yao
waliyoyagundua yenye madini na kupewa wachimbaji madini wakubwa wenye
mitaji mikubwa na vifaa bora vya kazi (wakiwamo wawekezaji kutoka nchi
za nje). Wasuluhishi wanatoa maelezo kuwa maeneo hayo ni ya wachimbaji
wakubwa, wamepewa tangu miaka kadhaa iliyopita. Wachimbaji madini wadogo
wanapopinga tayari watu wanaingia kwenye vurugu.
Waumini
wa dini wanapofanya maandamano kudai haki yao ya kikatiba ya kuabudu,
kukataliwa na polisi wasifanye maandamano, kwa malengo kuwa wanaleta
udini, uchochezi, hawana kibali cha maandamano au kuna sababu za
kiintelejensia. Waumini wanapokaidi na kupinga maelezo ya polisi na
kufanya maandamano, wanakutana na nguvu ya polisi na kutiwa adabu.
Wanasiasa
wanapokusudia kufanya mikutano ya hadhara kuelezea sera za vyama vyao,
au kukerwa na tamko fulani la Serikali, wakati mwingine hunyimwa kibali
cha kufanya hivyo, na polisi hutoa maelezo kuwa wanataka kuhatarisha
amani na utulivu uliopo.
Wanasiasa
wanapokaidi na kufanya mikutano kwa lazima, Serikali huwaona ni
wafedhuli, polisi huwatawanya na kutembeza mkong’oto kwa wanasiasa hao
na kuvunja mikutano. Ghasia zinatokea. Mifano kama hiyo ipo mingi
kuanzia kwa wanafunzi wa vyuo, walimu, madaktari, wanaharakati na vyama
vya wafanyakazi, wote hao wanaangukia pale pale penye kupenda chongo
kuita kengeza.
Septemba
6, 2013, tumeona kupitia vyombo vya mawasiliano na umma kitimtim na
pata shika hadi nguo kuchanika na watu kuumizana ndani ya Bunge la
Tanzania, baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kutoa amri ya kutolewa ndani
ya Bunge kwa Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe,
ambaye ni Waziri Mkuu Kivuli, kutokana na kiongozi huyo kukaidi kukaa
chini baada ya kuambiwa mara tatu na Naibu Spika.
Sina
haja ya kurudia kuelezea chanzo cha mkasa huo wa Naibu Spika Ndugai na
Mbowe kwa urefu, la msingi ni kuangalia nani kaanzisha vurugu bungeni.
Baadhi ya wananchi wanasema Naibu Spika huyo hakutumia busara kumtoa
Mbowe ndani ya Bunge, angemsikiliza.
Wananchi
wengine wanasema Mbowe hakutumia busara. Kwamba kwanini hakutii amri ya
Naibu Spika ya kumtaka akae chini? Mbowe kweli alikataa kukaa chini,
lakini akionesha dalili ya kutekeleza amri ya kutoka ndani ya Bunge.
Vipi
wabunge wengine kuacha viti vyao -- Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi, na Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulambai -- kuwa
mstari wa mbele kumzuia Mbowe asitoke na kuwazuia askari wa Bunge
wasifanye kazi zao.
Wananchi
bado wanazungumza na kutoa maelezo na maswali anuwai, kuhusu mwenendo
wa viongozi wawili hao (Ndugai na Mbowe), wabunge wa vyama vya upinzani,
wabunge wa CCM na wabunge wa Chadema.
Matukio
kadhaa yakiambatana na vurugu, kauli za matusi na kejeli ndani na nje
ya Bunge zilizopata kutokea, zinatoa taswira gani kwa wananchi na
mustakabali wa uongozi wa Taifa letu la Tanzania.
Bunge
ni muhimili mmoja kati ya mihimili mingine miwili, Serikali na Mahakama
ya dola Tanzania. Bunge linatunga sheria na kufuatilia utendaji kazi wa
Serikali kuona kama inatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kufuata taratibu
(kanuni) zilizowekwa kisheria. Vipi muhimili huo unajiletea wenyewe
sokomoko?
Tunaweza
kuangalia kanuni za Bunge la Tanzania na tamaduni za mabunge katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, kote huko bado tutaelekezwa kutii
amri ya Spika wa Bunge na Kanuni za Bunge husika. Busara si kanuni wala
sheria ni hekima, akili na falsafa.
Je,
wabunge waliocheza kilinge kisicho chao hawakustahili kutii kanuni za
Bunge, hawakupaswa kuwa na busara? Au ndiyo ukipenda chongo kuita
kengeza? Tafakari kabla ya kusema!
SOURCE: JAMHURI MEDIA
|