Saturday, 21 September 2013

Mbaroni kwa kuchochea kuususia Mwenge

21st September 2013
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara , Zelothe Steven
Polisi mkoani Mtwara, imewatia mbaroni  watu watatu, wakiwamo wawili wa familia moja kwa tuhuma za kukutwa na vipeperushi vinavyokataza wananchi kushiriki mbio za Mwenge wa Uhuru, uliofika  mkoani humo wiki iliyopita.

Watu hao ni Hassani Nahembe (34), Bakari  Nahembe (70) anayetajwa kuwa baba mzazi wa mtuhumiwa wa kwanza na Seleman Nangumbi (34).

Wakati huo huo, wanakijiji cha Rwelu mkoani hapa wameilalamikia hatua ya polisi ya kuwapiga , kuharibu mali zao na kupora fedha wakati wa kuendesha msako wa kuwakamata wapinga Mwenge kijijini hapo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Said Mnyeto, alithibitishia  kuwa watu hao walikamatwa baada ya polisi kufanya upekuzi nyumbani  kwa  Nahembe.
Alisema Nahembe alilalamikiwa na jeshi hilo kusambaza vipeperushi hivyo.

“Usiku wa kuamkia Septemba 12, saa 11 alfajiri, nikiwa msikitini alikuja mwanakijiji mmoja na kuniambia naitwa nje, nilipotoka niliwakuta  polisi watatu  wakinisubiri,” alisema Mnyeto.

Alisema, baada ya kutoka nje walimweleza kuwa awapeleke nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya kufanya upekuzi.

“Kama Mwenyekiti wa kijiji ambaye ninafanya kazi za serikali   niliwapeka kwa  mtuhumiwa, alikataa kupekuliwa na kuwataka  polisi  hao kupekuliwa kwanza kabla hawajampekua yeye,” alisema.

“Askari walikubali, wakapekuliwa  kisha wakaingia ndani walipofika chumbani walikuta bahasha walipoiangalia waliona ina  vipeperushi vitatu,” alifafanua Mnyeto.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, vipeperushi vilikuwa na maneno: “Wananchi wasishiriki kwenye Mwenge, mabomu yatapigwa na nchi jirani.”

Mnyeto  alisema baada ya kupekuliwa kuliibuka purukushani kati ya polisi  na mtuhumiwa ambaye alidai vipeperushi hivyo vimerushwa chumbani kwake  na polisi hao.

“Vurumai  ziliwafanya wanakijiji kukusanyika  nyumbani kwa Nahembe na kusababisha zogo, huku vijana wakiwashambulia kwa maneno askari hao,” alisema.

Aliongeza kuwa alimsihi mtuhumiwa huyo  akubali kufungwa pingu ili aambatane na polisi kutoa maelezo kituoni.

Mnyeto alifafanua kuwa wakiwa safarini kuelekea kituoni, walikuta barabara imefungwa kwa magogo  na kwamba sehemu karibu tano zilikuwa na magogo makubwa  na polisi walipofika kituoni,  walitoa taarifa kwa kiongozi wao aliyeamuru kikosi kwenda kijijini hapo kuangalia usalama.

“Yalikuja  magari manne yakiwa na  askari wa kutuliza ghasia (FFU)  waliozagaa kila mahali, wanakijiji waliogopa na kukimbia porini, hadi walipotoka saa 10 jioni,” alisemaa Mnyeto.

Lukia Namwangala (37) mkazi wa kijiji hicho, alisema askari walifika nyumbani kwake na kumuamuru atoke ndani na kwamba baada ya amri hiyo alikimbilia porini.

Aliongeza  kuwa: “Wakati nakimbia nilimwona polisi  anaingia chumbani na jioni niliporudi baada ya msako niliingia chumbani na kukuta   kitanda changu kimevurugika.”

Pia alisema fedha ambazo hata hivyo hakutaja kiasi chake, alizozikopa Vicoba na kuzihifadhi chini ya godoro hakuzikuta, hivyo `kujenga’ hisia kwamba ziliporwa na askari hao.

Kwa upande wake, Yusuf  Seleman (40) alidai askari hao walifika nyumbani kwake na kuingia dukani kisha  kuchukua boksi tatu, mbili za juisi na moja la sipi soda.

“Wakati askari wanakuja niliingia chumbani na kufunga mlango, wakaingia dukani wakachukua hivyo vitu, baada ya hapo walizunguka nyuma ya nyumba yangu wakaikuta pikipiki yangu wakafungua na kuweka chumvi,”Alisema.

“Pikipiki yangu wameitia chumvi, wameniingiza katika umaskini, yaani hii  haitanifaa tena,“ alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara , Zelothe Steven, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa malalamiko ya wananchi dhidi ya polisi, alisema kama wana malalamiko  wafike  kwake ili awasikilize.
 
CHANZO: NIPASHE