MTUHUMIWA, Manfred Adam anayekabiliwa na kesi ya kutishia kuua katika
hali isiyotarajiwa amelimwaga kojo katika Mahakama ya Mwanzo na kuleta
vurugu kubwa zilizosababisha kuvunjika kwa meza ya Mahakama ya Mwanzo ya
Mazimbu mkoani Morogoro mwanzoni mwa wiki hii.
Katika vurugu hizo
zilizolazimisha shughuli za mahakama kusimama kwa muda wa saa mbili,
askari wawili waliokuwepo eneo la tukio walishindwa kumdhibiti Manfred,
kitendo kilichofanya kuitwa kwa wengine zaidi ambao waliweza kumtuliza
mtuhumiwa huyo.
Hakimu Alisile Mwankejela aliyekuwa akisikiliza kesi
hiyo namba 322 ya mwaka 2013 pamoja na makarani wa mahakama hiyo
walitimua mbio kuhofia kudhurika, mara tu baada ya vioja hivyo kuanza
kufuatia kuahirishwa kwa kesi ya mtuhumiwa huyo ambayo itasomwa tena
Septemba 24, mwaka huu.
“Ni kweli tukio hilo limetokea
baada ya kuhairisha kesi, mshitakiwa huyo alikojoa mahakamani na kufanya
vurugu kubwa,” alisema hakimu huyo alipokutwa ofisini kwake. Karani wa makahama hiyo, Kidawa Minangu alimwambia mwandishi wetu;
“Manfed
asubuhi aliletwa hapa kwa ajili ya kesi yake, alipofika tuliita jina
lake na aliingia mahakamani na kusomewa mashitaka yake, kesi
ilipohairishwa cha ajabu alivua suruali na kukojoa hapa mahakamani,
tuliwaita askari wawili wa hapa mahakamani walipomkamata alianza
kupigana nao na kuvunja meza za mahakama ndipo tulipoamua kuomba msaada
wa askari wengine ambao walifika na kumdhibiti.”
Source: : bongo.blogspot.com