Na James Magai, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Hata hivyo, kupitia kwa wakili wao, Mohamed
Tibanyendela walikata rufaa Mahakama Kuu, wakiwasilisha sababu tisa za
kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu, iliyowatia hatiani pamoja na
adhabu yake.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, imewaachia huru wafuasi 52 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokuwa wakitumikia adhabu ya
kifungo cha mwaka mmoja jela.
Wafuasi hao wa Ponda waliachiwa huru jana baada ya
Mahakama Kuu kutengua adhabu ya kifungo hicho waliyopewa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu.
Wafungwa hao walihukumiwa kifungo hicho na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Machi 21, 2013 baada ya kutiwa hatiani
kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama
kutenda makosa, kukaidi amri ya Polisi kabla na baada ya kufanya
maandamano yaliyozuiwa na Polisi, kufanya mikusanyiko haramu na
kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa wakili wao, Mohamed
Tibanyendela walikata rufaa Mahakama Kuu, wakiwasilisha sababu tisa za
kupinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu, iliyowatia hatiani pamoja na
adhabu yake.
Katika hukumu yake jana, Jaji Salvatory Bongole
licha ya kukubaliana na hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu kuwa
washtakiwa walikuwa na hatia, lakini alikubaliana na hoja za wakili wao
Mohamed Tibanyendela kuwa adhabu waliyopewa haikuwa sahihi kulingana na
makosa yaliyowatia hatiani.
Katika shtaka la pili, warufani walitiwa hatiani
kwa kosa la kufanya mikusanyiko haramu na shtaka la tatuwalitiwa hatiani
kwa kosa la kukaidi amri halali ya Jeshi la Polisi.
Jaji Bongole alisema kwamba katika makosa hayo warufani walishtakiwa chini ya Sheria ya Jeshi la Polisi.
Alisema kuwa kwa mujibu wa Miongozo ya Jeshi la
Polisi (Police General Oders-PGO), warufani hao walipaswa kuhukumiwa
adhabu ya faini ya Sh50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela na si mwaka
mmoja.
“Hivyo ninakubaliana na hoja za wakili wa warufani
kuwa utetezi wa kupunguziwa adhabu haukuzingatiwa wakati wa kuadhibiwa
na ninatengua adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja na kuibadilisha kuwa
kifungo cha miezi mitatu jela,” alisema Jaji Bongole na kuongeza:
“Warufani walihukumiwa adhabu hiyo Machi 21, 2013
na leo ni Oktoba 21, 2013. Kutoka Machi 21 hadi Oktoba 21, 2013
wameshakaa jela zaidi ya miezi mitatu, basi wameshamaliza kifungo chao.”
Pia Jaji Bongole alikubaliana na hoja za Wakili
Tibanyendela kuwa Hakimu wa Mahakama ya Kisutu Fundi Fimbo alikosea
kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama na kuwaadhibu kwa kosa hilo
wakati tayari alikwishawatia hatiani kwa kosa la kufanya mikusanyiko
isiyo halali.
Uamuzi huo ulipokewa kwa shangwe kubwa na wafuasi hao wa Ponda,
ndugu, jamaa na marafiki zao waliofika mahakamani hapo kufuatilia hukumu
hiyo.
Wakati wakitoka nje ya ukumbi wa mahakama, baada
ya kuchiwa huru, katika kushangilia wafuasi hao walikuwa wakikariri
maneno, Takbirrrr, Alah Akbal.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI