Tuesday 22 October 2013

Watuhumiwa mafunzo ya ugaidi wasomewa upya mashtaka


“Wengine wawili walikamatwa na kifikia adadi ya watu 13 na kwamba uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.”PHOTO|FILE 
Na Haika Kimaro, Mwananchi

Posted  Jumanne,Oktoba22  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mahakama ilielezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Mtwara. Watuhumiwa 11 wa ugaidi waliokamatwa wakifanya mafunzo ya kijeshi yenye asili ya kigaidi msituni Wilaya ya Nanyumbu, Mtwara wamefikishwa katika mahakama ya Mkoa Mtwara na kufunguliwa upya mashtaka baada ya kesi yao ya awali kuondolewa katika mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mfawidhi Mtwara, Ladislaus Komanya alisema shauri hilo limesomwa upya baada ya kuhamishiwa Mahakama ya Mkoa kutoka Mahakama ya Wilaya.
Komanya alisema washtakiwa wote wanakabiliwa na makosa mawili.
Kwa mujibu wa wakili huyo, kosa la kwanza ni kuwa, kati ya Septemba 21 na 26 mwaka huu wanadaiwa kufanya mkusanyiko usiokuwa halali wenye lengo la uvunjifu wa amani.
Shtaka la pili ni kufanya uchochezi, ambapo Septemba 26 mwaka huu Wilaya ya Nanyumbu kwenye msitu walikutwa na machapisho ya kanda za cd zenye video za uchochezi hali iliyowapelekea watu kujengea hofu.
Mahakama ilielezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine ya kusikilizwa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Mtwara, Dynes Lyimo alisema dhamana ipo wazi kwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wakazi Mtwara watakaosaini mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh5 milioni mmoja kati yao awe ni mtumishi wa Serikali ama taasisi inayotambulika na awe na barua ya utambulisho toka kwa mtendaji wa Serikali ya Mtaa anakoishi.
Hakimu wa mahakama hiyo aliahirisha kesi hiyo na kusema kuwa itatajwa tena Novemba 11 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Stephen Zelothe alisema kuwa watuhumiwa wengine wawili walikamatwa na kifikia adadi ya watu 13 na kwamba uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

SOURCE: MWANANCHI