Tuesday 22 October 2013

Aliyemwapisha Rais Kenyatta afukuzwa kazi


“Naomba jibu kwa unyenyekevu. Hata hivyo, nitakuwa tayari kufika mbele ya JSC kutoa majibu yangu Jumanne Oktoba 15 au siku yoyote inayofaa kwenu,” Maelezo ya Gladys Shollei kwenye barua yake kwa JSC. 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Oktoba21  2013  saa 12:36 PM
Kwa ufupi
Akielezea uamuzi huo, Jaji Mutunga alitaja ukosefu wa nidhamu, ukiukaji wa kanuni za kazi za maofisa wa mahakama, ukiukaji wa sura ya sita ya Katiba inayohusu maadili na kukaidi maagizo ya wakubwa wake, kama sababu zilizosababisha JSC kumsimamisha kazi Shollei.
 
Ni mwanamama Gladys Shollei ambaye alikuwa  Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya.
Nairobi. Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Gladys Shollei amefukuzwa kazi kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuwadharau makamishna wa Tume inayosimamia idara hiyo (JSC).
Shollei ndiye aliyemwapisha Rais Uhuru Kenyatta alipoingia madarakani mwaka huu.
Kwenye taarifa ya uamuzi huo iliyosomwa na Jaji Mkuu Willy Mutunga mwishoni mwa wiki, JSC ilitoa sababu tano za kumsimamisha kazi Shollei, ambapo msajili huyo alishutumiwa kwa kukosa maadili.
“Baada ya kusoma madai yote yaliyomkabili msajili mkuu wa mahakama na baada ya kusoma majibu yake, ikizingatiwa kwamba aliamua kujitokeza mbele ya tume, tumeamua kwa pamoja kumsimamisha kazi mara moja,” alisema Jaji Mutunga.
Kwa hatua hiyo, Shollei anakuwa msajili mkuu wa Mahakama wa kwanza kufutwa kazi tangu Idara ya Mahakama ifanyiwe marekebisho ili kuafiki matakwa ya Katiba ya sasa.
Aidha, ni ofisa wa pili wa ngazi ya juu kwenye idara hiyo kupigwa kalamu, baada ya aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu, Nancy Baraza kufutwa mwaka jana.
Akielezea uamuzi huo, Jaji Mutunga alitaja ukosefu wa nidhamu, ukiukaji wa kanuni za kazi za maofisa wa mahakama, ukiukaji wa sura ya sita ya Katiba inayohusu maadili na kukaidi maagizo ya wakubwa wake, kama sababu zilizosababisha JSC kumsimamisha kazi Shollei.
“Kutokana na uzito wa masuala yaliyosababisha kusimishwa kazi kwa Shollei, JSC inaialika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ifanye uchunguzi wa kina kuhusu masuala haya,” alisema Jaji Mutunga.
“Madai yaliyotolewa kumhusu Shollei ni mazito sana. Pesa zinazohusishwa katika madai hayo ni Sh2.207 bilioni. Amekubali madai 33 ambapo Sh1.7 bilioni pesa za walipa ushuru ziko katika hatari ya kupotea. Amekataa madai 38 ambayo yanafikia Sh250 milioni ilhali majibu yake kuhusu Sh361 milioni yanakanganya,” alisema.
Jaji Mutunga alisema kuwa JSC imeweka madai yote yanayomkabili Shollei, majibu yake na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na JSC katika tovuti yake.
Mwezi uliopita, Shollei aliiandikia barua JSC akiifahamisha kwamba yuko tayari kufika mbele yake kuanzia Oktoba 15, kujibu madai dhidi yake.

Kwenye barua hiyo, Shollei alisema ingawa aliomba JSC imwongezee muda zaidi ili ajitayarishe kufika mbele yake kupitia arifa aliyomtumia Dk Mutunga, alisema hakuwa amepata jibu wakati wa kuandika barua hiyo.
Shollei pia aliomba kwamba aruhusiwe kuyajibu madai dhidi yake hadharani, mbele ya  wanahabari. Awali, Shollei waliafikiana kusuluhisha tofauti kati yao nje ya mahakama. Hii ni baada ya Shollei kwenda mahakamani akitaka JSC ambayo ndio mwajiri wake izuiwe kumchunguza
SOURCE: MWANANCHI