Posted Jumanne,Septemba17 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni katika muktadha huo tunatafsiri tukio la
wiki iliyopita ambapo Padri wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya
Mpendae, Anselmo Mwang’amba alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
Tunaungana na wananchi wote ambao wamekuwa
wakipaza sauti kulaani kushamiri vitendo vya kihalifu vya kumwagia watu
tindikali. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu, tumeshuhudia matukio mengi
ya watu kumwagiwa tindikali, hasa Visiwani Zanzibar. Jambo
linalozidisha hofu na wasiwasi katika jamii ni kutokamatwa na kufikishwa
mahakamani wahalifu hao ambao mpaka sasa hakuna anayejua nia yao au
sababu zinazowasukuma kufanya unyama huo dhidi ya binadamu wenzao.
Kwa namna ya pekee vitendo hivyo vinavyoshika kasi
kila kukicha vimewachanganya wananchi wa pande zote mbili za Muungano.
Dhana potofu imejengeka kwamba wahalifu hao wanafanya hivyo ikiwa ni
njia ya mkato ya kulipiza visasi. Lakini matukio karibu yote ya kumwagia
watu tindikali hayakuonyesha dalili zozote za kulipa visasi, bali ni
vitendo vya jinai vyenye mrengo uliovishwa sura ya kisiasa na udini.
Ni katika muktadha huo tunatafsiri tukio la wiki
iliyopita ambapo Padri wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mpendae,
Anselmo Mwang’amba alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana. Tukio
hilo ni mfululizo wa matukio mengine mengi ya aina hiyo ambayo yalianza
kujitokeza mwaka uliopita. Itakumbukwa kwamba pazia la uovu huo
lilifunguliwa rasmi kwa kumwagiwa tindikali Mkurugenzi wa Manispaa ya
Zanzibar, Rashid Ali Juma akifuatiwa na Katibu wa Mufti Zanzibar, Fadhil
Suleyman Soraga aliyemwagiwa tindikali Novemba 6, 2012.
Padri wa Kanisa Katoliki, Ambrose Mkenda
alijeruhiwa vibaya kwa risasi Desemba 26 mwaka jana mjini Zanzibar,
akifuatiwa na Padri Evaristus Mushi pia wa Kanisa Katoliki mjini humo
aliyeuawa kwa kupigwa risasi. Sote tunakumbuka tukio la mwezi uliopita
ambapo wasichana wawili raia wa Uingereza waliokuwa wakifanya kazi za
kujitolea visiwani humo walimwagiwa tindikali mchana kweupe.
Tukiweka kando tukio la kushambuliwa kwa wasichana
hao na lingine la Mkurugenzi wa Home Shopping Centre aliyemwagiwa
tindikali jijini Dar es Salaam, matukio mengine tuliyotaja hapo juu
yalitokea Zanzibar na hakika yaliwalenga viongozi wa dini. Upo ushahidi
kwamba viongozi hao wa dini walikuwa wakikemea vikali vitendo vya vurugu
na uvunjaji wa sheria vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya watu, hasa
wakati wa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya.
Kinachosikitisha mpaka sasa ni kwamba waliofanya
uhalifu huo bado hawajakamatwa. Kama tulivyodokeza hapo juu, hali hiyo
inatia hofu na mashaka, kwani kila mmoja wetu anajiuliza zamu ijayo
itakuwa ya nani? Tunajiuliza inakuwaje kundi dogo la wahalifu linazizidi
nguvu serikali zote mbili pamoja na Jeshi la Polisi ambalo halionekani
kuwa na mbinu, mikakati na uwezo wa kuwakamata watu hao waovu?
Hatutaki kuamini kwamba wanaofanya uhalifu huo
hawajulikani kwa jamii. Tunashindwa kuamini kwamba jamii inaweza kukaa
kimya hata baada ya Jeshi la Polisi kutangaza zawadi nono kwa
watakaofanikisha kukamatwa kwa watu hao.
Hapana shaka matukio hayo yanatupeleka pabaya kama
taifa na hakika huu ni mwanzo wa kutokomeza sekta ya utalii na nyingine
nyingi zinazochangia katika kukuza uchumi.
Tusijidanganye kamwe kwamba sheria kali au vyombo
vya dola pekee vinaweza kukomesha uovu huo pasipo jamii kutoa
ushirikiano. Hapana shaka kuwa, hali hiyo ndiyo iliyochangia pia vyombo
vya dola kushindwa kuwakamata wahuni waliokuwa wakifanya vitendo vya
kibaguzi kwa misingi ya dini kwa kuchoma makanisa na sehemu za starehe,
zikiwamo baa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI