Na Florence Majani, Mwananchi
Posted Ijumaa,Septemba20 2013 saa 10:54 AM
Posted Ijumaa,Septemba20 2013 saa 10:54 AM
Kwa ufupi
Matokeo ya utafiti huo ambayo yalichapishwa
Agosti mwaka huu yanaonyesha kuwa vidonge hivyo vya uzazi kwa wanaume
vitazuia kutunga mimba bila ya kuathiri uwezo wa mwanamume kushiriki
tendo la ndoa kama kawaida.
Ni dhahiri kwamba wanaume watashtuka, lakini huenda nao wakashiriki uzazi wa mpango bila upasuaji
Vidonge vya uzazi wa mpango vimezoeleka kutumiwa
zaidi na wanawake pekee, kiasi kwamba ni jambo la ajabu kusikia kuwa
wanaume nao wanaweza kuvimeza.
Hata hivyo, watafiti mbalimbali wamefanikiwa
kutengeneza vidonge vya uzazi ambavyo vinazifanya mbegu za kiume
katika mfuko wa uzazi wa mwanamume zisiwe na nguvu ya kuweza kutungisha
mimba. Utafiti wa dawa hiyo ambao umewaumiza kichwa wanasayansi kwa
miaka mingi umewezesha kupatikana kwa vidonge hivyo ambavyo havina
vichocheo kama vile wanavyotumia wanawake ambavyo huingia katika mfuko
wa mbegu za uzazi na kisha kuzidhoofisha.
Matokeo ya utafiti huo ambayo yalichapishwa
Agosti mwaka huu yanaonyesha kuwa vidonge hivyo vya uzazi kwa wanaume
vitazuia kutunga mimba bila ya kuathiri uwezo wa mwanamume kushiriki
tendo la ndoa kama kawaida.
Dk James Brander wa Taasisi ya Dana-Farber anasema
utengenezaji wa vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume umekuwa na
changamoto kubwa kutokana na upatikanaji wa dawa ambazo zinaweza
kuzuia mfumo wa utengenezwaji wa seli za mbegu za kiume.
Dawa hizo ziitwazo JQI zilizotengenezwa katika
maabara ya Bradner zinafanya kazi kwa kulenga protini maalumu zilizoko
katika korodani ambazo ni muhimu katika uzazi.
Vidonge hivyo vilichanganywa na vichocheo vya ‘Desogetrel’ ambazo huzuia uzalishwaji wa mbegu za kiume.
Profesa Malise Kaisi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya
Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambaye ni Mtanzania wa kwanza
kuzalisha watoto kwa njia ya upandikizaji (IVF) anasema ana wasiwasi
mkubwa kuhusu dawa hizo kutumiwa kwa wanaume.
“Dawa za uzazi wa mpango ni rahisi kutumiwa na
wanawake kwa sababu wanawake wana mfumo mwepesi kwa dawa kufanya kazi na
kuzuia utungishwaji wa mimba,” anasema.
Hata hivyo, Profesa Kaisi anahisi kwa wanaume
itakuwa hatari kwao kutumia dawa hizo kwani kunaweza kusababisha hata
kuua kabisa uzalishwaji wa mbegu.
“Wanaume wana maumbile tofauti na mwanamke.
Korodani za mwanaume ni kama kiwanda kinachofanya kazi usiku na mchana.
Kwa siku moja mwanamume anazalisha mbegu milioni 10,” anafafanua Prof.
Kaisi.
Katika kuzifanyia utafiti, panya dume alipewa dawa
hizo, kisha akawekwa pamoja na mwenza wake ambapo licha ya kujamiiana
hata baada ya miezi kadhaa panya jike hakupata mimba.
Utafiti huo ulibaini kuwa pamoja na kuzuia uzalishwaji wa mbegu, vilevile dawa hizo zilionekana kuwa hazina madhara yeyote kwa kuwa hazina mchanganyiko wa vichocheo vya aina yoyote.
Utafiti huo ulibaini kuwa pamoja na kuzuia uzalishwaji wa mbegu, vilevile dawa hizo zilionekana kuwa hazina madhara yeyote kwa kuwa hazina mchanganyiko wa vichocheo vya aina yoyote.
“Hazikuwa na madhara ya vichochezi (hormone).
Mwanamume atakayezitumia hatabadilika tabia au mwili kupata mabadiliko
yeyote yale” anasema Dk Martin Matzuk, mtafiti mwingine wa dawa hizo.
Dk Matzuk anasema hakuna kinga yeyote nyepesi ya
uzazi wa mpango kwa wanaume iliyowahi kugunduliwa tangu kugunduliwa kwa
mipira ya kiume miongo kadhaa iliyopita.
Inaelezwa kuwa utafiti huo ni mkubwa na
utakaoleta mapinduzi katika uzazi wa mpango baada ya vidonge vya uzazi
kwa wanawake kuonekana na upungufu kadhaa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Cyriel
Massawe wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi Muhimbili ,
anasema iwapo kweli dawa za uzazi wa mpango zitagunduliwa basi
zitasaidia wanandoa kujadili namna bora zaidi ya kupanga uzazi.
“Wenza wanapokuwa na uchaguzi wa kutosha wa namna
ya kupanga uzazi inawasaidia wote wawili. Kwa mfano kama mama ana
matatizo kadhaa, basi baba atachukua jukumu la kutumia vidonge ili
kupanga uzazi,” anasema Dk Massawe.
Anasema kwa sasa wanaume wana njia moja tu ya
kupanga uzazi ambayo ni mipira ya kiume hivyo basi iwapo njia nyingine
zaidi zimepatikana basi itasaidia.
Dk Massawe anasema vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume bado vina changamoto kwa sababu ya mfumo wa uzazi wa mwanamume.
“Zile dawa zinatakiwa zikazuie uzalishwaji wa
mbegu kwa wanaume kwa hiyo ili kuingilia mfumo wa uzalishwaji na pindi
mwanamume atakapoacha kutumia awe kama kawaida…ni changamoto” anasema.
Hata hivyo, Dk Massawe anasisitiza kuhusu
ushirikiano wa wenza katika kupanga uzazi na kusema kuwa, ni suala
linalohitaji watu wawili kujadiliana ili kujua ni njia ipi na salama ya
uzazi wa mpango.
Anaongeza kuwa wenza wanapopanga uzazi
itawasaidia kuimarisha afya zao, za watoto na hata kupunguza mzigo wa
majukumu ambayo hayakutarajiwa.
Utafiti mwingine unaofanana na huu ulifanywa mwaka
2010 ambapo wanasayansi waliwauliza wanawake na wanaume iwapo wanaume
wanaweza kutumia dawa za uzazi wa mpango pindi zitakaposhauriwa na
wafamasia.
Katika utafiti huo ulioongozwa na Dk Judith Eberhardt wa Chuo
Kikuu cha Masuala ya Jamii,wanaume, 140 na wanawake 240 waliulizwa
kuhusu matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume.
Hata hivyo matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa
ingawa wanaume wote walisema watafurahi kutumia vidonge hivyo lakini
wanawake walipata hofu iwapo wenza wao watakubali kutumia vidonge hivyo
au kuvitumia inavyotakiwa ili kuimarisha uzazi wa mpango.
Katika utafiti huo, wanaume walio kwenye
mahusiano ya kudumu walitoa maoni ya kuvikubali vidonge hivyo huku wale
walio katika mahusiano ya muda mfupi waliikosoa njia hiyo ya uzazi wa
mpango.
Mei 2009, wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha
Manchester, Uingereza walitumia wanawake na wanaume kuzifanyia utafiti
njia za uzazi wa mpango kwa wanaume kujua iwapo zinafanya kazi ipasavyo
na zina manufaa.
Watafiti hao waliwaambia wenza walioshiriki
katika utafiti huo kuwa wanaume pekee watumie njia za uzazi wa mpango
huku wanawake wakiambiwa kutotumia njia yeyote ili kupima iwapo njia za
uzazi wa mpango zinafanya kazi kwa ubora au la.
Hata hivyo, wanaume kadhaa nchini walioulizwa
iwapo watakubali kutumia njia yeyote ya uzazi wa mpango ikiwemo vidonge
na wanaume wanane kati ya kumi, walikataa kutumia njia yeyote ile.
Mmoja wao, Edwin Mnzeru anasema, yeye na mke
wake hawawezi kutumia njia ya uzazi wa mpango ya vidonge, mipira ya
kiume, wala ya kitanzi kwa sababu zina madhara kiafya na ni kinyume
na dini.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI