Wednesday 18 September 2013

Dk Magufuli amuumbua mkandarasi


Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli akitoa maelekezo jana alipotembelea kuangali maendeleo ya  mradi wa ujenzi wa barabara ya Ndundu- Somanga(km 60) mkoani Pwani.Kushoto kwake ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik.Picha na Mwanakombo Jumaa 
Na Habel Chidawali

Posted  Jumatano,Septemba18  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni wa Kampuni ya Italia ya SIETCO baada ya kulegalega katika ujenzi wa barabara ya lami huku akitoa visingizio.


Dodoma. Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameiagiza Kampuni ya SIETCO inayojenga Barabara ya Migori-Fufu, kuacha visingizio na ikabidhi kazi hiyo Februari 15, 2014 kwa mujibu wa mkataba vinginevyo ifungashe na kuondoka nchini.
Dk Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kushtukiza katika ujenzi wa Barabara ya Dodoma–Iringa kwa kiwango cha lami, ujenzi unaoendelea sasa.
SIETCO ni Kampuni ya Ujenzi kutoka Italia ambayo ni miongoni mwa makandarasi watatu wanaojenga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 260 kutoka Iringa hadi Dodoma na kipande chenye urefu wa kilomita 93.8.
“Hawa watu hawafai kabisa, walivurunda kazi katika Barabara ya Singida–Isuna hivyo wana rekodi mbaya na leo wanaonekana kuwa watashindwa, sasa nawaagiza kuwa wakishindwa kukamilisha ujenzi huu wasipewe kipande chochote cha barabara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Magufuli.
Kuhusu kipande cha Barabara ya Dodoma-Fufu (Km 70.9), alimsifia Mkandarasi wa Kampuni ya China Communication Construction Co. Ltd (CCCC), baada ya kujiridhisha kuwa ujenzi wake umefikia asilimia 73.
Waziri Magufuli alisema, kumekuwa na tabia ya baadhi ya makandarasi kugeuza Tanzania shamba la bibi ambalo kila mtu anavuna na kuondoka.
Mhandisi wa ujenzi Mkoa wa Dodoma, Leonard Chimagu, alisema ujenzi wa barabara katika mkoa huo unakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya wafugaji kutokutii sheria na hivyo kupitisha mifugo kila wakati barabarani na kuharibu miundombinu.

SOURCE: MWANANCHI