Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Wakati wote huo, Naibu Spika ambaye alikuwa
akiendesha kikao hicho alikaa kimya bila kuwataka wabunge hao wa chama
chake kujielekeza katika kujadili Muswada huo.
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya
Katiba ulipitishwa Bungeni wiki iliyopita na kinachosubiriwa sasa ni
Rais Jakaya Kikwete muda wowote kuutia saini kuwa sheria au kuukataa.
Tunatambua fika ukweli kuwa, kwa mara nyingine katika kipindi cha mwaka
mmoja, Rais ameingizwa majaribuni katika namna ambayo atapaswa tena
kutumia umakini na busara zake ili kukwepa kuingia katika mtego wa
kikatiba uliotegwa na wabunge wa chama chake cha CCM.
Tunasema hivyo kwa sababu Muswada huo muhimu kwa
mustakabali wa nchi yetu ulipitishwa na Bunge pasipo kujadiliwa. Wabunge
wa upinzani waliposusia mjadala wa Muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi
wa Bunge kutokana na tofauti zilizojitokeza baina yao na Naibu Spika,
Job Ndugai, ilitegemewa kwamba wabunge wa CCM waliobaki Bungeni
wangewatendea haki wananchi kwa kuujadili Muswada huo kwa kina na
umakini mkubwa kwa kutanguliza mbele masilahi ya taifa letu.
Lakini kwa mshangao wa wengi, hasa wananchi
waliokuwa wakifuatilia matukio hayo katika televisheni, wabunge hao
hawakuujadili Muswada huo na badala yake wakajikita katika kuporomosha
matusi ya nguoni, kutoa kejeli na kuwapiga vijembe wabunge wa upinzani
kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi waliosusia mjadala huo.
Wabunge wa CCM, wakiwamo baadhi ya mawaziri walisimama mmoja baada ya
mwingine kutoa kauli za kibabe na kusema Muswada huo lazima upitishwe
kutokana na wingi wao katika Bunge hilo.
Wakati wote huo, Naibu Spika ambaye alikuwa
akiendesha kikao hicho alikaa kimya bila kuwataka wabunge hao wa chama
chake kujielekeza katika kujadili Muswada huo. Hapo ndipo alipoonyesha
bayana kukosa busara za kuliongoza Bunge kupata mwafaka wa Muswada huo
nyeti. Matokeo yake ni kumwingiza Rais Kikwete kwenye mkenge kwa kumtaka
aukubali Muswada huo ili uwe sheria, huku akijua kwamba ulikuwa batili
kutokana na kupitishwa kwa hoja ya nguvu.
Sio nia yetu kuorodhesha hapa hoja zote za wabunge
wa upinzani ambazo Naibu Spika Ndugai alikataa kuzisikiliza na
kusababisha mtafaruku mkubwa Bungeni, hatimaye wabunge wa upinzani
wakaususia mjadala wa Muswada huo na kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge. Hata
hivyo, moja ya hoja hizo ni umuhimu wa kutoa muda zaidi kwa wananchi wa
Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu Muswada huo kabla haujapitishwa na
Bunge.
Kwa jumla, wananchi wengi wamepaza sauti kupinga
mchakato uliotumiwa na wabunge wa CCM kuupitisha Muswada huo. Gazeti
hili leo limechapisha habari inayotoa kilio cha wananchi mbalimbali
wanaomtaka Rais Kikwete asisaini Muswada huo kutokana na upungufu mkubwa
uliomo. Hata hivyo, sisi tunadhani Rais Kikwete atumie busara kama
alivyofanya katika suala kama hili mwaka jana. Anaweza kuupitisha kuwa
sheria, lakini akairudisha sheria hiyo Bungeni ili ifanyiwe marekebisho
makubwa.
Tungependa kulitahadharisha Bunge kwamba kazi ya
kutunga Katiba ya nchi sio lelemama. Ni mchakato usiohitaji vitendo vya
kupimana nguvu au kutunishiana misuli. Ni kazi inayohitaji maridhiano na
ushirikiano miongoni mwa wadau. Inahitaji kuvumiliana, kushauriana na
kuelekezana katika hali ya utulivu. Ndio maana kuigeuza kazi hiyo kuwa
suala la chama fulani cha siasa ni kukaribisha ‘majanga’ kwa nchi yetu.
Kama ambavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikisisitiza, wingi wa
watoa hoja sio muhimu. Jambo muhimu ni nguvu ya hoja.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI