Friday, 27 September 2013

Kikwete kuipangua Tanesco

Rais Kikwete 
Na Mwandishi Wetu

Posted  Ijumaa,Septemba27  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Wateja nchini wamekuwa wakilalamikia shirika hilo kwa kushindwa kuboresha huduma zake.


New York. Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali ina mpango wa kulifumua Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili likidhi mahitaji ya nchi.
Akizungumza juzi na ujumbe wa Shirika la Millenium Challenge (MCC), ulioongozwa na Daniel Yohannes jijini New York, Rais Kikwete alisema Serikali italifanyia Tanesco mageuzi muhimu na marekebisho makubwa.
Alisema marekebisho hayo yanalenga kuisaidia Serikali kuharakisha jitihada zake kusambaza umeme kwa wananchi wengi zaidi.
Serikali imeliweka suala la usambazaji umeme kwa wananchi mijini na vijijini, miongoni mwa maeneo yake ya vipaumbele.
“Pia, Serikali yetu itaangalia viwango vya malipo vinavyotozwa na Tanesco kwa wateja wake,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Mageuzi haya katika Tanesco ni muhimu sana na yameanza kufanyika, hakika Serikali imedhamiria kuyakamilisha mageuzi hayo muda mfupi iwezekanavyo.”
Rais Kikwete alisema Tanzania imeamua kuwa, fedha za awamu ya pili za MCC zitaingizwa kupanua zaidi huduma za umeme.
“Wakati naingia madarakani mwaka 2005, ni asilimia 10 ya Watanzania waliokuwa wanapata umeme. Miaka saba iliyopita, asilimia hiyo imepanda na kufikia 21 ikiwa ni asilimia 11 zaidi kuliko miaka 50 ya Uhuru. Lengo la sasa ni kuifikisha asilimia 30 au zaidi 2015,” alisema Rais Kikwete.
Katika mazungumzo hayo na Rais Kikwete, Yohannes alitaka kujua ni hatua zipi zinazochukuliwa na Serikali kurekebisha changamoto zinazoikabili Tanesco.
Pia, hatua gani zinachukuliwa kukabiliana na matatizo ya rushwa.
Katika mazungumzo hayo, Yohannes alimwelezea Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ombi la Tanzania kuingizwa katika awamu ya pili ya misaada ya Serikali ya Marekani kupitia MCC chini ya Akaunti ya Milenia Tanzania (MCA(T)).
 
Nchi nyingine za Afrika ambazo maombi yao yanafikiriwa kwa awamu ya pili, ni Morocco, Msumbiji na Lesotho.


Tanzania ndiyo nchi iliyopokea sehemu kubwa zaidi ya msaada wa MCC duniani kwa awamu ya kwanza, ambako ilipewa Dola 698 milioni za Marekani ambazo zimeingizwa katika miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, usambazaji umeme vijijini, miradi ya maji na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia.
Serikali ya Tanzania imeamua fedha za awamu ya pili, kuingizwa kupanua zaidi huduma za umeme na ujenzi wa barabara za vijijini kwa nia ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma za umeme.
Lengo ni kuboresha barabara za vijijini maeneo yanayozalisha mazao kwa wingi zaidi.
Tayari, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kwenye Bunge la Bajeti alieleza kuwa Tanesco itavunjwa na kuundwa kampuni mbili au tatu.
Profesa Muhongo alisema lengo ni kuhakikisha shirika hilo linafanya kazi kwa ufanisi, kwa sababu tatizo lililopo ni utendaji mbovu.
Pia, alitangaza vita ya kuwafukuza vigogo wa Tanesco watakaoshindwa kuwaunganishia umeme wateja kwa bei ya punguzo. Hata hivyo, kumekuwa na ukatikaji umeme mara kwa mara.

 SOURCE: MWANANCHI