Posted Jumanne,Septemba24 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Hoja ya Tanzania hapa ni kwamba miradi
inayozungumziwa na nchi hizo tatu haitofautiani hata kidogo na ile
iliyojadiliwa mwaka jana chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Rais wa Kenya,
Mwai Kibaki.
Hatua ya Serikali kukiri hadharani kwamba nchi
za Kenya, Rwanda na Uganda kutoihusisha Tanzania katika mambo yanayohusu
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kunatishia uhai wa jumuiya hiyo ni
ishara kwamba mpasuko katika chombo hicho ni mkubwa mno kuliko wengi
tulivyodhani.
Mipasuko baina ya nchi na nchi au miongoni mwa
nchi zilizo katika jumuiya kama zilivyo nchi wanachama wa EAC ni jambo
la kawaida. Hata hivyo, migogoro kama hiyo hutatuliwa kufuatana na
taratibu za kidiplomasia na kiitifaki zilizopo. Tulitegemea tofauti
zilizopo miongoni mwa baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo
zitatuliwe kwa kufuata taratibu hizo.
Hivyo, Waziri Samuel Sitta alipojitokeza hadharani
wiki iliyopita na kuzilaumu nchi hizo kwa kuitenga Tanzania, wachunguzi
wa masuala ya kidiplomasia waliiona hatua hiyo kama ishara ya nchi za
EAC kushindwa kupata suluhisho la migogoro iliyopo. Mgogoro uliopo hivi
sasa unafuatia hatua ya Rwanda, Kenya na Uganda kuanzisha ushirikiano wa
pamoja katika maeneo ya miundombinu, biashara na visa ya pamoja.
Tanzania imevunjwa moyo na mwenendo wa nchi hizo,
lakini imesema kwa vile nchi hizo zimechukua uamuzi huo, Tanzania
itapaswa kujiweka kando. Pamoja na Ibara ya 7(3) iliyounda jumuiya hiyo
inatoa fursa kwa nchi wanachama kuwa na ushirikiano wa pekee, Tanzania
inasema hatua ya nchi hizo tatu ilipaswa kujadiliwa na nchi zote
wanachama kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa.
Hoja ya Tanzania hapa ni kwamba miradi
inayozungumziwa na nchi hizo tatu haitofautiani hata kidogo na ile
iliyojadiliwa mwaka jana chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Rais wa Kenya,
Mwai Kibaki. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli itokayo Isaki hadi
Rusumo mpakani mwa Rwanda na ile ya Ivinza mpakani mwa Burundi. Mkutano
huo pia ulikubaliana kushirikiana katika nyanja za nishati na mafuta.
Tanzania pia inazilaumu nchi hizo tatu kwa
kulazimisha kuwapo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, huku zikijua
kwamba suala hilo liliundiwa kamati ambayo inatazamiwa kutoa ripoti yake
katika mkutano wa wakuu wa nchi Novemba mwaka huu. Msimamo wa Tanzania
ni kwamba ina uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya muungano, hivyo
haitaki kuburuzwa na kuingizwa kichwakichwa katika mambo yanayohitaji
tathmini jadidi na umakini mkubwa kabla ya kuyatekeleza.
Hata hivyo, zipo tetesi kwamba Tanzania imeziudhi
nchi hizo kwa mwendo wake wa kinyonga katika kutoa msimamo katika mambo
mengi nyeti, ikiwa ni pamoja na: Kuanzisha visa ya pamoja; Suala la
umiliki wa ardhi; Sarafu ya pamoja; na Kuanzishwa haraka kwa Shirikisho
la Afrika Mashariki. Tanzania inaonekana kwa nchi hizo kutokuwa na
utashi wa kisiasa na kudaiwa kuegemea zaidi katika umoja wa nchi za SADC
badala ya EAC.
Lakini suala lisilozungumzwa hadharani ni hofu
iliyozikumba nchi hizo kutokana na fursa za kiuchumi ilizonazo Tanzania
hivi sasa, kiasi cha kuiwezesha kuipiku hata Kenya kama nchi yenye
uchumi mkubwa kuliko nyingine katika Ukanda huu katika miaka michache
ijayo. Hivyo, katika hali ya sasa Tanzania haina sababu ya kutaharuki.
Ni kwa manufaa yake kubaki katika EAC kama mwanachama, lakini kama
Waziri Sitta alivyosema, isikubali kuburuzwa na kuingizwa kichwakichwa
katika mambo yasiyo na tija kwa wananchi wa Tanzania.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI