Wednesday, 25 September 2013

Mchungaji Lusekelo ainanga CCM

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo 
Na Fidelis Butahe

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mbali na kuiponda sheria ya mabadiliko ya katiba, Lusekelo alisema lingekuwa jambo la busara kama Bunge la Katiba lingekuwa na wajumbe ambao sio wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinashinikiza kusainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, ili ipatikane katiba itakayokibeba chama hicho.
Wakati Lusekelo akieleza hayo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gosper Bibble Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe, amesema kuwa diwani, mbunge, waziri na rais haina maana kuwa una mamlaka yote dhidi ya Watanzania.
Kauli za viongozi hao wa dini, zimekuja katika kipindi ambacho vyama vya siasa, wanaharakati na wananchi wamekuwa wakimshinikiza Rais Jakaya Kikwete, kutosaini muswada huo na badala yake, urejeshwe bungeni, ili ukafanyiwe marekebisho kwa maelezo kuwa una kasoro nyingi.
Akizungumza na gazeti hili Lusekelo maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ alisema CCM inatambua kuwa mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba kama yakipita, chama hicho kitakuwa katika wakati mgumu, hivyo ni lazima kihakikishe kuwa hatua hiyo inakwama.
“Hiki chama kinaweza hata kung’oka madarakani kama mapendekezo ya sasa yatapita. Namshauri Rais Kikwete asikilize malalamiko ya Watanzania kuhusu muswada huu, asisaini na aurudishe bungeni ili ufanyiwe marekebisho,” alisema na kuongeza kuwa;
Kitendo cha wabunge wa chama kimoja kuwa wengi katika Bunge la Katiba, Zanzibar kutokushirikishwa katika utoaji wa maoni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kumaliza majukumu yake baada ya kukabidhi rasimu katika Bunge la Katiba, ni kasoro kubwa zilizoibuliwa na wanasiasa lakini zikapuuzwa.
Mbali na kuiponda sheria ya mabadiliko ya katiba, Lusekelo alisema lingekuwa jambo la busara kama Bunge la Katiba lingekuwa na wajumbe ambao sio wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wake, Askofu Kakobe wakati akizungumza katika ibada ya misa ya pili kanisani kwake Mwenge Dar es Salaam, alisema viongozi wa nchi wamechaguliwa kwa neema ya mungu, wasitumie nafasi zao kuamua kila jambo hata kama halina maslahi kwa nchi na wananchi wanaowaongoza.
“Viongozi wanatakiwa kuacha kujigamba na kujiona wao ni kila kitu, nafasi walizonazo ni dhamana tu na siku moja Mungu anaweza kuwanyang’anya na kuwapa wengine,” alisema kiongozi huyo wa kidini.

SOURCE: MWANANCHI