Kwa ufupi
Siku moja kabla ya onesho, msiba wa Albert
Mangwea ukatokea, na hapo ikamlazimu mwanamuziki huyo kuahirisha onesho
lake, na kulisogeza wiki mbili mbele huku akiahidi asilimia 15 ya faida
atakayopata, angeipeleka kwa familia ya Albert Mangwea.
Mama wa MwanaHip Hop aliyewahi kuaminika kuwa
bingwa wa mitindo huru, Albert Mangwea aliyefariki mwezi Mei mwaka huu,
Denisia Costantine Mangwea ameibuka na kumtetea mwanamuziki wa kizazi
kipya Hamis Mwin’juma ambaye anatuhumiwa kuahidi pesa kwa mama huyo na
kuingia mitini.
Sakata hilo ambalo limekuwa likiripotiwa tangu
mwishoni mwa wiki iliyopita, linatokana na kitendo cha mwanamuziki huyo
(MwanaFA) ambaye aliwahi kuahirisha onesho lake, baada ya kifo cha
msanii mwenzake (Albert Mangwea), kutokuweka hadharani hitimisho la
ahadi aliyoitoa kwa familia ya marehemu.
Tarehe 31 ya mwaka huu ilikuwa ni tarehe ya onesho
la The Finest ambalo MwanaFA alikuwa akitimiza miaka 13 ya muziki wake,
akawa na lengo pia na kuugeuza muziki wa Hip Hop uwe na sura ya
kistaarabu na kibiashara pia ili kuuongezea aina ya mashabiki.
Siku moja kabla ya onesho, msiba wa Albert Mangwea
ukatokea, na hapo ikamlazimu mwanamuziki huyo kuahirisha onesho lake,
na kulisogeza wiki mbili mbele huku akiahidi asilimia 15 ya faida
atakayopata, angeipeleka kwa familia ya Albert Mangwea.
Baada ya mazishi, Onesho la The Finest lilifanyika
Juni 14, na baada ya hapo, MwanaFA hakuonekana akisema kwenye mitandao
wala kwenye redio kuhusiana na mapato yake kwenye onesho hilo na kiasi
gani alipeleka kwa Mama Mangwea. Tangu onesho hilo, huu ni mwezi wa tatu
na ndipo gazeti moja la kila wiki likaandika kuhusiana na suala hilo,
jambo ambalo linaendelea kuzungumzwa kila kukicha kwenye vyombo vya
habari. Na ndipo gazeti hili liliamua kwanza kumtafuta Mwana FA na
kuongea naye.
Kauli ya MwanaFA
Akiongea na Mwananchi, MwanaFA alikiri kuahidi
kutoa fedha hizo na aliahidi asilimia 15 ya faida itakayotokana na
mapato ya onesho la The Finest.
“Nakiri kukosea jambo moja, nilipoahidi, niliongea
na wanahabari lakini wakati wa kutoa, nilitoa bila kutangaza, na hii
kutoa jamani ni moyo, haina haja kumtangaza mtu kwa kuwa umemsaidia au
umempa pole”, alifafanua MwanaFA
Alisema katika mapato aliyoyapata kutokana na
onesho hilo ambayo yalikuwa ni jumla ya shilingi 19.5 milioni, alitoa
milioni tatu na kuzikabidhi kwa mama huyo, ingawa si taslimu,
aliziingiza kwenye akaunti yake, katika benki ya Exim. Alifafanua kwamba
alilifanya hili kwa moyo na hakuwa na nia ya kujitangaza kwa hiyo
alilimaliza akawa anaendelea na shughuli zake. Baada ya kauli hii,
Mwananchi likapiga mguu mpaka Kihonda kwa mama yake Mangwea, Bi Denisia
Costantine Mangwea
Mama Mangwea ashangaa!
Alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo Mama Mangwea
alikiri kwamba ameumia sana moyo baada ya kusikia ripoti ya kwamba
MwanaFA anadaiwa hakutoa hizo pesa kwani alitoa kipindi kile kile cha
msiba.
“Kabla hata ya arobaini, aliweka benki kisha akaja
na mwenyewe, hakuna na waandishi kama wanavyofanya wenzake, alikuja
mwenyewe tukaongea, na mara kwa mara tunawasiliana, wanataka kumtia doa
kijana wa watu ni muungwana sana”, alifafanua mama Mangwea.
Kwa uthibitisho zaidi mama huyo alitoa risiti aliyokabidhiwa na
MwanaFA ikionesha kiasi cha fedha alichotoa na tarehe halisi ambayo
fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti yake.
“Naomba kwa niaba ya familia niwathibitishie
alitoa na mngemwacha kijana wa watu aendelee na shughuli zake, kwani
alitoa kwa nia njema na ndiyo maana hakutaka kuitangaza sana”, alimaliza
mama huyo. Katika wiki mbili hizi vyombo mbali mbali, na hata kwenye
mitandao ya kijamii kumekuwa na mjadala kuhusiana na ahadi hiyo ya
MwanaFA iliyodaiwa kuwa hewa
SOURCE: MWANANCHI