Friday 13 September 2013

Weruweru wasisitiza elimu kwa wanawake

Mkuu wa zamani wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru mkoani Kilimanjaro, Dk Maria Kamm (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Zuhura Muro, kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya shule hiyo, jijini Dar es Salaam jana. Zuhura ni mwanafunzi wa zamani wa shule hiyo. Picha na Fidelis Felix 

Na Elias Msuya na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba13  2013  saa 10:39 AM
Kwa ufupi
Maadhimisho hayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanawake maarufu waliosoma shule hiyo akiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha Rose Migiro yalijikita kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.


Wito huo, umetolewa na watu mbalimbali waliowahi kusoma katika shule hiyo kongwe hapa nchini
Dar es Salaam. Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru, iliyoko mkoani Kilimanjaro  yameendelea kufana baada ya aliyekuwa mkuu wa shule hiyo, Dk Maria Kamm kusisitiza umuhimu wa elimu kwa wanawake.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanawake maarufu waliosoma shule hiyo akiwemo aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk Asha Rose Migiro yalijikita kuzungumzia umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela aliyekuwa mshereheshaji, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen  Kijo- Bisimba na maofisa mbalimbali wa Serikali ambao pia walisoma katika shule hiyo.
Akizungumzia historia ya elimu kwa wanawake nchini, Dk Maria Kamm alisema kumwelimisha mtoto wa kike ni kuelimisha Taifa.
“Ukimuelimisha mtoto wa kike unakuwa umeelimisha Taifa zima, lakini ukimuelimisha mwanamume unakuwa umeelimisha mtu mmoja,” alisema Dk Kamm.
“Mwanamke wa Afrika, jinsi alivyo na thamani kubwa. Yeye ndiye anayelea watoto katika familia, anabeba mizigo mgongoni na kichwani,  hiyo ndiyo nguvu ya mwanamke,” alisema.
Hata hivyo,  alisema changamoto kubwa kwa wanawake wa Afrika ni kukosa elimu na akasisitiza kuna umuhimu wa kutoa elimu kwa wanawake.
Kuhusu uongozi wake katika Shule ya Weruweru, Dk Kamm alisema aliingia wakati Mwalimu Nyerere ameanzisha Sera ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo pia ilitakiwa kutekelezwa kwenye elimu.
“Niliingia Weruweru wakati nchi imefungua ukurasa mpya wa Sera ya Ujamaa na Kujitegemea. Imani yangu ilikuwa ni kuiendesha shule hiyo kwa mfumo huo.
“Nikatenga madarasa na kuweka uongozi wa makundi ya watu 10 kama ilivyokuwa mabalozi ya nyumba 10,. Viongozi wote walichaguliwa kwa kura, hata kwenye michepuo kulikuwa na viongozi…shule yetu ilikuwa inajitegemea kwa kila kitu. Ni mara chache tu tulihitaji msaada wa Serikali,” alisema.
Awali akimkaribisha Dk Kamm, Balozi Mwanaidi Maajar alisema ndoto ya mwalimu huyo ya kuelimisha mtoto wa kike imetimia na kwamba wao kama wahitimu wanaweka mkakati wa elimu kwa miaka 50 ijayo.

“Wakati Serikali inasema mtoto aliyepata mimba asisome, Mama Kamm aliwasomesha hivyo hivyo. Leo wanawake tunafanya nini ili kutetea elimu kwa watoto wa kike.”
Mwenyekiti wa Bodi ya MCL ambaye pia ni mmoja wa wanafunzi wa zamani wa Shule ya Weruweru, Zuhura Muro, alisema njia pekee ya kumkomboa mtoto wa kike ni kumpatia elimu na kwamba wakati umefika kwa wanawake waliopata elimu kuwasaidia watoto hao kupata elimu bora.

SOURCE: MWANANCHI