Kwa ufupi
- Huku akizungumza kwa umakini na kujiamini alisema, “ CCM kimejaa ubaguzi, siasa za chuki na kimeshindwa kusimamia misingi imara ya kutetea masilahi ya wananchi. Wazanzibari kataeni hali hii, wekeni tofauti za vyama pembeni, Zanzibar kwanza vyama baadaye. Tusimamie muungano wa heshima, haki na usawa.”
Zanzibar. Siku saba tangu Halmashauri Kuu ya
Chama Cha Mapinduzi (Nec), kumvua uanachama, Mwakilishi wa Jimbo la
Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf Himid, kutokana na
kukiuka miiko ya chama hicho, ameibuka jana na kukiponda chama hicho
kuwa kimejaa siasa za chuki na ubaguzi.
Huku akizungumza kwa umakini na kujiamini alisema,
“ CCM kimejaa ubaguzi, siasa za chuki na kimeshindwa kusimamia misingi
imara ya kutetea masilahi ya wananchi. Wazanzibari kataeni hali hii,
wekeni tofauti za vyama pembeni, Zanzibar kwanza vyama baadaye.
Tusimamie muungano wa heshima, haki na usawa.”
Himid ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Maridhiano
Zanzibar yenye wajumbe sita, alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la
wazi lililoandaliwa na kamati hiyo katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani na
kuongozwa na mwanasiasa mkongwe ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati
hiyo, Hassan Nassor Moyo.
Katika hotuba yake ya dakika 46, Mansour ambaye
kwa nyakati tofauti amewahi kuwa Waziri na Naibu Waziri wa Maji,
Nishati, Ardhi na Mazingira, Waziri wa Kilimo, Waziri asiyekuwa na
Wizara Maalumu na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, aliendelea
kusimamia msimamo wa muundo wa muungano wa serikali tatu kwa kufafanua
kuwa, “Muundo wa muungano wa serikali tatu ni wimbi kubwa halizuiliki
tena.”
Mansour ambaye alisema hajui sababu za kufukuzwa
kwake CCM, alisisitiza: “Sitakwenda mahakamani kukata rufaa kwa sababu
nilichaguliwa na wananchi hivyo sitaki kuwawakilisha kwa mgongo wa
mahakama,”
“Pia sina pesa za kuchezea huko mahakamani.
Sihitaji malumbano, katika uchaguzi mdogo sitagombea kwa sababu sitaki
kuendeleza machungu kwa wananchi wa jimbo langu na pia najiepusha na
siasa za matusi, naweza kufikiria kugombea mwaka 2015.”
Katika kongamano hilo mmoja wa wajumbe wa kamati
hiyo, Mohamed Ahmed Al-riyami alitangaza kujivua uanachama wa CCM, kwa
maelezo kuwa chama hicho kimepoteza mwelekeo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi