Thursday, 12 September 2013

Matumla: Napigana ili nisife njaa

 “Daktari alinizuia kupigana tangu Mei mwaka huu,’’Bondia Rashid ‘Snake man’ Matumla  
Na Imani Makongoro, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Septemba12  2013  saa 9:28 AM
Kwa ufupi
Matumla ambaye alitembelewa na gazeti hili nyumbani kwake maeneo ya Keko Mwanga, Dar es Salaam na kushuhudia maisha yake nje ya ngumi, alisema hana jinsi zaidi ya kupigana mapambano ya utangulizi ili kupata pesa ya kujikimu.


Matumla ameshiriki mara tatu michezo ya Olimpiki, mwaka 1988, 1992, 1996. .
Dar es Salaam. Licha ya umaarufu aliowahi kuwa nao bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid ‘Snake man’ Matumla hali yake kiuchumi na kiafya imezidi kuwa tete huku mwenyewe akikiri mambo yake kumwendea kombo.
Matumla bondia aliyewahi kuiletea sifa Tanzania miaka ya 1990 aliliambia gazeti hili jana kuwa amekuwa akipigana kutokana na hali ngumu ya maisha licha ya maradhi yanayomkabili kipindi hiki.
“Nadhalilika hivi sasa, maisha yangu ni magumu mno, nacheza ngumi kiubishi ili kutafuta fedha ya kujikimu kila kitu changu hivi sasa hakiendi vizuri,” alisema bondia huyo kwa huzuni katika mahojiano na gazeti hili.
Matumla ambaye alitembelewa na gazeti hili nyumbani kwake maeneo ya Keko Mwanga, Dar es Salaam na kushuhudia maisha yake nje ya ngumi, alisema hana jinsi zaidi ya kupigana mapambano ya utangulizi ili kupata pesa ya kujikimu.
“Kila kitu changu hivi sasa kinaniendea kombo, nilifanya biashara ya mahindi huko Tanga imekufa vivyohivyo na ile ya mbao, napigana ulingoni nikiwa mgonjwa ili nipate fedha kwani sina fedha kabisa,” alisema bondia huyo kwa masikitiko.
Matumla ambaye anabainisha kusumbuliwa na mgongo na miguu anadai hivi sasa anatumia tiba ya kienyeji baada ya kushindikana hospitalini na kueleza kuwa alicheza pambano lake la Agosti 10 mjini Morogoro na Maneno Oswald akiamini amepona kumbe ilikuwa tofauti na maradhi yanayomkabili .
“Napata tabu sana, leo hii nadhalilika, kila kitu kinaniendea kombo kweli, nadhalilika ila sina jinsi,” alisema Matumla kwa masikitiko.
Bondia huyo aliyewahi kutembelea gari aina ya Benz enzi zake, alibainisha kuwa amepigana mapambano mengi akiwa tayari na maumivu hayo, lakini alifanya hivyo ili apate pesa lakini hakuwa na nguvu za kupigana.

SOURCE: MWANANCHI