Monday, 2 September 2013

Mauaji ya kutisha mkoani Simiyu

                 
                             Wakazi wa Simiyu wakiwa katika moja ya mikutano yao 

Na Kelvin Matandiko, Mwananchi  (email the author)

Posted  Agosti31  2013  saa 22:34 PM
Kwa ufupi
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee, wastani wa watu watatu walikuwa wakiuawa kila wiki na kikundi hicho cha watu kinachofahamika kama Baraza la Kimila katika Mkoa wa Simiyu, wakiwamo wanawake na watoto.


Simiyu. Siyo kundi la Sungusungu, Polisi Jamii au askari wa makundi ya kiharakati au kisiasa unaoweza kufahamu. Hakuna ofisi wala vikao wanavyokaa kusikiliza mashtaka kabla ya uamuzi, mbaya zaidi hakuna anayejitambulisha kama mfuasi wa baraza hilo, lakini linatoa hukumu na kutekeleza mauaji ya kutisha.
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee, wastani wa watu watatu walikuwa wakiuawa kila wiki na kikundi hicho cha watu kinachofahamika kama Baraza la Kimila katika Mkoa wa Simiyu, wakiwamo wanawake na watoto.
Wanachama wa kikundi hicho maarufu Dagashida, hufahamiana muda wa kupokezana ‘Mbiu’inaposikika kama ishara ya kuhudhuria tukio la utoaji wa hukumu.
Unaweza kulinganisha na Kundi la Al-Shabaab, kwani baraza hilo hufanya maasi na kusambaa msituni kwa muda wa siku zisizopungua tano wakihofia kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi.
Baraza hilo ni mfano wa kamati ya ulinzi au mahakama inayojiendesha kwa kufuata miiko na kanuni zake katikati ya Serikali inayoendeshwa kwa utawala wa sharia, likidaiwa kutoka Kabila la Wasukuma na jamii ya Kinyantuzu waliopo Mkoa wa Simiyu.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu aliyeomba kutotaja jina lake gazetini kwa sababu za siyo msemaji wa polisi alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili akishauri atafutwe mhusika ili atoe ufafanuzi kuhusu matukio hayo.
Hali ilivyo kwa sasa
Mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kufika Vijiji vya Igangabilili, Nyamiswi, Badugu, Shigala, Budalabujiga na Mikoma vilivyopo Wilaya za Itilima, Bariadi, Busega na maeneo mengine mkoani humo.
Hofu iliyopo siyo kwa wanakijiji tu, bali hata mgeni yeyote, wakiwamo watumishi wa Serikali kama walimu, watakaoonekana kuwa tofauti na jamii hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa hata kwa mwandishi wa habari atakayebainika kuingilia utaratibu wao, atakutana na adhabu kali.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamiswi Kata ya Gambushi, Leah Muhami anasema kuwa hali ni mbaya na kwamba mbali ya kuchoshwa na ukatili huo, wanakijiji wamekuwa wakihofia kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuogopa kuonekana wasaliti kwa baraza hilo wakihofu kugharimu maisha yao.
“Yaani wakikusikia unatoa taarifa zao polisi, lazima maisha yako yatakuwa hatarini. Watakushughulikia na wanapofanya mauaji hutakiwi kuonekana ukiwa na simu ya mkononi, ”anasema Leah.


Ukatili unavyofanyika
Katibu wa CCM kutoka Wilaya ya Itilima, Jumaa Iadhi anasema ukatili huo, umekuwa ukifanyika kwa kulipiza kisasi, ugomvi wa mirathi, mipaka ya ardhi na njama zozote za kupangwa kwa namna yoyote, hata na watu wenye fedha.
“Kwa mtu ambaye watamhisi au kupelekewa tuhuma za aina yoyote dhidi yake, watapiga mbiu na kumweka katikati, kisha watampiga faini ya pesa ambazo anatakiwa kuzitoa papo kwa papo,”anasema Iadhi.
Anasema kuwa awali, baraza hilo walikuwa wakikusanya fedha na kuzipeleka kwenye ujenzi wa visima, madarasa au madawati. “Wakati mwingine imeshakuwa ni kama mradi wao wa kujipatia pesa za pombe, yaani ni ukatili usiovumilika,”anasema Iadhi.
Mwingine ni Michael Miraji, ambaye ni mkazi wa wilayani Bariadi anasema kuwa sababu za kukithiri kwa matukio hayo ni jamii hizo kukosa huduma ya Jeshi la Polisi, kukosekana kwa imani za kidini na elimu.
“Makanisa na misikiti ni muhimu sana, mbali na mambo mengine kisaikolojia watu wanajengewa tabia ya ustaarabu, lakini huku hadi mwenyekiti wa kijiji, unakuta naye hana dini yoyote,” anasema Miraji.
Anaongeza kuwa umbali uliopo kati ya Kituo cha Polisi na kijiji ni takriban kilometa 60. “Kwa umbali huo, askari wamekuwa wakikuta tukio tayari limeshatokea, hivyo ni vigumu sana kudhibiti, labda Serikali iongeze nguvu kwa mkoa huu wa Simiyu kama sehemu ya Operesheni Maalumu.
Matukio ya karibuni
Baadhi ya matukio ya hivi karibuni ni pamoja lililotokea Kata ya Zagayu ambapo wanawake wawili waliteketezwa kwa moto na baraza hilo kwa tuhuma za ushirikina.
Mbali na tukio hilo, tukio jingine ni la mauaji ya kuchomwa moto nyumba na familia ya watu watatu katika Kijiji cha Budalabujiga.
Mmoja kati ya maofisa usalama mkoani humo, ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake anasema kuwa ingawa ukatili huo umepungua, lakini bado kuna changamoto kubwa katika vijiji vya Kata ya N’hobora.
“Juzi kuna wanakijiji watatu waliuawa kwa mapanga wakihusishwa na ushirikina, pia kuna Kata ya Mkoma imekuwa na mauaji sana,” anasema na kuongeza:


“Takwimu za matukio hayo zimeanza kupungua kutokana na juhudi za utawala mpya wa Mkoa wa Simiyu ulioanzishwa hivi karibuni.”
Anaongeza: “Mwaka mmoja uliopita tulikuwa tunapokea taarifa za matukio ya vifo viwili mpaka vitatu vya wanakijiji kuuawa kikatili kutoka ndani ya kila kijiji, lakini kwa sasa zinaweza kumalizika siku tatu mpaka wiki hatujasikia.”
Mwalimu wa Sekondari ya Biashara wilayani Bariadi, Mwangwa Bujiku anasema kuwa ukatili huo umejenga hofu hata kwa walimu wanaopangiwa kwenda kufundisha maeneo ya vijiji vya mkoa huo.
“Wenyeji wa eneo hili hawapendi mtu anayekuwa tofauti na wao kiuchumi, hata ukiongea Kiswahili wanaona unajidai. Kuna mwalimu alipangiwa Kata ya Dutwa, alionekana kuishi tofauti wakamtengenezea kesi ya kutembea na mwanafunzi,” anasema Bujiku.
Anafafanua kuwa vijana wa baraza hilo waliamua kumpigia mbiu mwalimu huyo na kumpiga faini na kumfilisi kila kitu.
“Yule mwalimu akachukuliwa uhamisho na walikuwa wamepanga kumuua kabisa,”anasema.
Linatumika kwa visasi
Katibu wa Umoja wa Wazazi mkoani humo, Fadhil Murani anasimulia akisema kuwa mbaya zaidi baraza hilo limekuwa likitoa hukumu kwa kutumia hisia na tuhuma zisizokuwa na uhakika.
“Halafu mtuhumiwa wakishamweka katikati, haruhusiwi kujitetea wala kuzungumza chochote, matokeo yake wanamchoma moto au wanamuua kwa mapanga,”anasema Murani.
Anasimulia kuwa asilimia kubwa ya vijana wa baraza hilo kwa sasa wanatumiwa na watu wenye fedha katika ugomvi wa mipaka ya ardhi na mashamba.
“Mfano; kama una adui yako ukapeleka pesa kidogo kwa wazee wa baraza hilo au ukawanunulia pombe, halafu ukamshtaki mtu, lazima utasikia yule mtu kavamiwa usiku na kuuawa kwa mapanga au watampigia Mbiu na kamchoma moto,”anasema Murani.
Mmoja wa wanavijiji kutoka Kata ya Mahuni, Deo Ngulyati anasema kuwa malengo halisi ya kuwepo kwa baraza hilo yamepotea kwani limegeuka kuwa adui na hasara katika ustawi wa jamii.
“Zamani lilikuwa ni baraza linalosaidia ukuaji wa ustawi wa jamii na kuchochea maendeleo, walidhibiti migogoro, walihamasishana kwenye misiba na majanga, kujenga huduma za kijamii na walizuia uhalifu,” alisema Ngulyati.
Changamoto kwa Jeshi la Polisi
Moja kati ya changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa Jeshi la Polisi mkoani Simiyu ni hofu ya kuendelea kusambaa kwa mauaji na hukumu hizo.
Baadhi ya Askari Polisi mkoani humo wamezungumza kwa nyakati tofauti juu ya changamoto inayoendelea kujitokeza kupitia baraza hilo.
Mmoja kati ya askari hao aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, anasema kuwa vijana wa baraza hilo wakishatekeleza hukumu yao kwa raia hukimbilia msituni na kujificha mfano wa Kundi la Al- Shabaab wakiwindana na polisi.
Anaongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni viongozi wa Serikali za Mitaa na viongozi wa kisiasa kutotoa ushirikiano.
“Hakuna mwanasiasa, awe diwani au mwenyekiti wa kijiji anayeingia bila kushirikisha baraza hilo, kwa hivyo wanapokuwa madarakani wanakosa ujasiri wa kuwakemea kwa maovu wanayoyafanya,” anasema askari huyo.
Akichangia hoja hiyo, askari mwingine katika kundi hilo anasema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya wanakijiji wameshaanza kutoa taarifa za matukio ya mauaji yanapofanyika.
“Tukimkamta mmoja wa vijana wa baraza hilo changamoto nyingine inajitokeza kwenye ushahidi mahakamani. Hakuna mwanakijiji atakayekubali kusimama mahakamani kutoa ushahidi, kwa hofu ya kuuawa. Inabidi mtuhumiwa aachiwe huru kwa kukosa ushahidi,” anasema askari huyo.
Itaendelea……………………

source: Mwananchi