Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 12:28 PM
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 12:28 PM
Kwa ufupi
Katika tukio la jana, raia wa Canada, Tabitha
Leah Ritchie (28) amekamatwa nchini Colombia baada ya kujaribu kupanda
ndege kurejea Canada akiwa na tumbo bandia la ujauzito alimokuwa
ameficha dawa ya kulevya aina ya Cocaine.
Ni wazi kwamba vita vya kupambana na dawa za
kulevya si ndogo, kwani kwa namna inavyoonekana ni kwamba wenye
kujihusisha na biashara hiyo, licha ya baadhi kudaiwa kushirikiana na
wafanyakazi wasio waaminifu katika vyombo vya ulinzi, wanabuni mbinu
tofauti kukwepa mkono wa sheria.
Tatizo la dawa za kulevya ni la dunia nzima, sio
Tanzania au Afrika tu, kuna raia wengi wa kigeni wamenaswa nchini
Colombia mwaka huu wakiwa na dawa za kulevya.
Katika tukio la jana, raia wa Canada, Tabitha Leah
Ritchie (28) amekamatwa nchini Colombia baada ya kujaribu kupanda ndege
kurejea Canada akiwa na tumbo bandia la ujauzito alimokuwa ameficha
dawa ya kulevya aina ya Cocaine.
Leah aliyekuwa anajifanya mtalii akirejea Toronto,
alihojiwa na polisi katika uwanja wa ndege wa Bogota. Polisi alimshuku
na kumuuliza alikuwa amesalia na miezi mingapi kujifungua.
Alijibu kwa ukali mno , hali iliyomfanya ofisa mmoja wa polisi kumtilia shaka zaidi na kuamua kumfanyia ukaguzi zaidi.
Ofisa huyo aligusa tumbo na kuhisi lilikuwa baridi mno na Ngumu sana, ndipo wakaamua kumkagua zaidi.
Walimkuta na dawa za kulevya zilizokuwa zimefungwa
ndani ya tumbo hilo bandia ambalo mwanamke huyo alikuwa amelivaa kwa
kufunga tumboni.
Inasemekana alisema ana miezi saba ya ujauzito
lakini baada ya polisi kumkagua walimpata na Cocaine kilo mbili
iliyokuwa ndani ya vipochi viwili
Leah atashtakiwa na huenda akafungwa jela kwa miaka mitano au minane.
Mwaka huu pekee karibu watu 150 wamekamatwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa Bogota.
Karibu theluthi moja ya waliokamatwa walikuwa raia wa kigeni, kwa mujibu wa maofisa wakuu nchini Colombia.
Wakati hayo yakiendelea nje, hapa nchini
inabainika kwamba kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya kumeleta
utamaduni mpya katika baadhi ya vijiwe vya vijana jijini Dar es Salaam.
Kulingana na utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya
katika vijiwe, baadhi ya vijana wamebuni utamaduni wa kufanya mazoezi ya
kubeba dawa za kulevya tumboni kwa kumeza mbilimbi bila kutafuna, ili
iwapo itatokea nafasi ya aina hiyo muda wowote, wawe tayari kuingia
kazini.
Uchunguzi uliofanywa maeneo ya Kinondoni,
Magomeni, Vingunguti, Manzese, Msasani, na Temeke, umegundua zao la
mbilimbi limekuwa likitumika kama kifaa cha kupima uwezo wa mbebaji wa
dawa za kulevya.
Sababu kubwa ya kutumiwa kwa mbilimbi ni ukweli
kwamba ukubwa wa kete za dawa za kulevya unakaribiana na ule wa zao hilo
(mbilimbi).
Mwandishi alishuhudia vijana wakiwa katika makundi
ya watu 10 hadi 15, kwa nyakati tofauti wakiwa natika vijiwe
wakishindana kumeza mbilimbi bila kutafuna. Kuna baadhi walionekana kuwa
na uwezo wa kumeza mpaka mbilimbi 30 kwa robo saa, huku wengine
wakienda mbali zaidi ya hapo, japo wengine walionekana kushindwa.
Kwa mujibu wa maelezo yao ni kwamba ukifikia hatua
hiyo, unapewa cheo cha Punda, jina linalomaanisha kuwa uko tayari
kubeba mzigo na kusafirisha kwenda nchi yoyote utakayotumwa.
Kwa mujibu wa vijana hao, wale wanaoonekana kumeza
mbilimbi hizo ndio huchukuliwa, na kutengenezewa pasi za kusafiria na
kuendelea kupewa miongozo mingine. Kutokana na mazoezi hayo, inasemekana
hata upatikanaji wa zao hilo ambalo mara nyingi hutumika kutengeneza
chachandu, umeanza kuwa wa taabu hasa baada ya bei yake kupanda tofauti
na awali.
Baadhi yao huwalazimu watumiaji kuagiza tunda hilo
kutoka katika Mkoa wa Tanga, na wengine Mombasa, Kenya ambako
hupatikana kwa wingi.
“Kwa Dar es salaam, Mbilimbi zinapatikana Kisutu
tu kwa sasa na kwa baadhi ya watu ambao wamepanda miti labda uani kwao
na sio kubwa kama zile ambazo tunatakiwa kumeza kwa hiyo inabidi sasa
kuanza kuingia mikoani kuzisaka”, alisema mmoja wa vijana waliokutwa
maeneo ya Feri, Dar es Salaam.
Inasemekana kutokana na uhaba wa matunda hayo
ambayo hustawi sana katika mikoa ya Pwani, wakazi wengi wa Jijini Dar es
Salaam wameanza kulima miti hiyo ndani ya uzio wa nyumba zao ili kuweza
kuhudumia wateja wao kwa ukaribu.
Maeneo ya Magomeni Mikumi yanatajwa kuwa maarufu
kwa zao hilo, wakazi wengi hasa kinamama wamekuwa wakipanda zao hilo
ndani ya uzio wa nyumba zao na kulihudumia ipasavyo ili kupata matunda
yenye ukubwa unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya vijana wanaofanya
mazoezi ya kubeba mzigo. Hata hivyo si wote wanaopanda mbilimbi kwa
ajili ya kujifanyia mazoezi ya dawa za kulevya.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI