Na Zaina Malongo, Mwananchi
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 12:54 PM
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 12:54 PM
Kwa ufupi
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH,Dk Marina Njelekela
anasema kutokana na kupatikana kwa mtambo huo wa kisasa hospitalini
hapo, wanaiomba serikali iwape fedha hasa zile ambazo imekuwa ikitumia
kuwasafirisha, kuwatibu wagonjwa wa moyo hasa nchini India na
kwingineko.
Kupatikana kwa mtambo huo kutasaidia
serikali kuondokana na mzigo wa asilimia 70 ya wagonjwa wa moyo
wanaopata rufaa ya kwenda kutibiwa nje.
Ndoto ya Watanzania hasa wale wasio na uwezo,
wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo kutibiwa haraka na kwa gharama nafuu
inaelekea kuwa ya kweli.
Ni baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
kusema kuwa sasa itaweza kupunguza wagonjwa wenye matatizo ya moyo
wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 60.
Matarajio hayo ya MNH kwa wagonjwa hao yanatokana na kupata mtambo maalumu wa kisasa utakaosaidia kufanya upasuaji wa moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH,Dk Marina Njelekela
anasema kutokana na kupatikana kwa mtambo huo wa kisasa hospitalini
hapo, wanaiomba serikali iwape fedha hasa zile ambazo imekuwa ikitumia
kuwasafirisha, kuwatibu wagonjwa wa moyo hasa nchini India na
kwingineko.
Badala yake, MNH inaomba fedha hizo ziwasilishwe
hospitalini hapo ili wagonjwa wengi zaidi waweze kutibiwa nchini.
Anasema mtambo huo unaojulikana kwa jina la Catherization Laboratory,
ndiyo mtambo ambao wagonjwa wengi nchini walikuwa wakisafirishwa nje
kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.
Anasema mtambo huo ulioigharimu serikali Sh3.6
bilioni utasaidia katika kumchunguza mgonjwa mishipa na shinikizo ndani
ya moyo na maradhi makubwa ya kazaliwa nayo kwa lengo la kujiridhisha
kama anapaswa kufanyiwa upasuaji au kuwekewa kifaa saidizi katika moyo
wake.
Anaongeza kuwa MNH imepata uwezo wa kupatiwa
mtambo huo baada ya baadhi ya madaktari wake kupatiwa mafunzo nchini
India na Israel tangu mwaka 2008 ambapo wagonjwa 453 wenye maradhi ya
moyo wamefanyiwa upasuaji.
“Kwa sasa upasuaji wa moyo unaofanyika katika
hospitali yetu (Muhimbili0 ni sawa na ule unaofanyika katika vituo
vikubwa vya upasuaji moyo duniani kote,”anasema Dk Njelekela
Mkurugenzi huyo wa MNH anasema kuwa kupatikana
kwa mtambo huo kutasaidia serikali kuondokana na mzigo wa asilimia 70 ya
wagonjwa wa moyo wanaopata rufaa ya kwenda kutibiwa nje.
“Sambamba na asilimia 70, pia serikali
itapunguza gharama ya dola za Marekani 10,000 kwa kulipia matibabu ya
mgonjwa mmoja anaetibiwa nje ya nchi ukilinganisha na Dola 6,000 kwa
matibabu ya hapa nchini.
“Kupitia uwepo wa kituo hicho hapa Muhimbili,
uongozi wa hospitali upo katika mazungumzo na Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii ili kulipia kiasi cha dola za Marekani 6,000 badala ya dola
10,000 kwa gharama ya mgonjwa mmoja anaepatiwa rufaa ya kupeleka nje ya
nchi,” anasema Dk Njelekela .
Dk Njelekela anaongeza kuwa miongoni mwa huduma zinazofanywa
katika kitengo hicho cha moyo ni upasuajai wa wa kuziba matundu kwenye
moyo,kubadilisha valvu ambazo zimebana na kushindwa kuruhusu damu
kupita kwenye moyo au kulegea na kufanya damu kuvuja kwenda sehemu
isiyohusika na kurudisha moyo katika hali yake ya kawaida.
Dk Njelekela anasema sambamba na kitengo hicho
kutoa huduma hiyo ya tiba, pia itafanya huduma nyingine ikiwamo kliniki
ya magonjwa ya valve ,moyo kutanuka ,mishipa kuziba,mapigo kushuka
pamoja na ugonjwa wa moyo ya kuzaliwa kwa watoto na upasuaji.
Takwimu za Serikali kupitia Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa hadi Aprili mwaka huu wagonjwa 402
walisafirishwa nje kwenda kupata matibabu ambapo kati ya hao, 189
walikuwa na matatizo ya moyo, 39 saratani , 34 figo na wengine 140
magonjwa mengine .
Rufaa hiyo ilitokana na wagonjwa hao kushindwa kupata matibabu yao nchini.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika kituo
hicho, Dk Robert Mvungi anasema kulingana na takwimu pamoja na tafiti
zilizofanywa nchi inaonyesha asilimia 30 ya Watanzania wa vijijini na
mjini wana matatizo ya ugonjwa wa moyo.
“Ugonjwa wa moyo umeendelea kuongezeka kwa kiasi
kikubwa mjini na vijijini ambapo asilimia 30 ya Watanzania waliopo
Kusini mwa Jangwa la Sahara baraniAfrika wanaugua ugonjwa huo,”anasema
Dk Mvungi.
Anafafanua kuwa vyanzo vikuu vya ugonjwa wa moyo
ni pamoja na unene, kuugua ugonjwa wa kisukari na mfumo wa maisha hasa
kipato kinapoongezeka.
Anasema kati ya asilimia 20 hadi 30 ya
Watanzania wana unene uliokithiri ambao unahatarisha afya zao na
kusababisha upatikanaji wa ugonjwa wa moyo.
Anasema Dk Mvungi kuwa kulingana na kuwepo kwa
viashiria vya ugonjwa huo kama ilivyoanisha, hata hivyo wagonjwa wengi
wanaowasili katika kupima afya zao wanafika hospitalini wakiwa wapo
katika hatua ngumu ya kupona ugonjwa huo. Anaongeza kuwa baada ya kuanza
kwa kutibu ya ugonjwa huo Muhimbili, wagonjwa 453 tayari
wameshafanyiwa upasuaji .
Hata hivyo, mtaalam huyo anaeleza kuwa kitengo
hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi wa kada
mbalimbali ,ambapo wanatakiwa wawe 365 badala ya 121 ya wataalamu
waliopo sasa hali inayosababisha kukidhi mahitaji halisi ya utoaji wa
huduma.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango ya Hospitali ya
Taifa Muhimbili, Agnes Kuhenga anasema mgonjwa mwenye rufaa kutoka
katika hospitali nyingine atatibiwa kwa gharama ya Sh10,000 kwa kumwona
daktari, Sh20,000 kama akilazwa na Sh50,000 kama atapatiwa upasuaji.
Anasema katika kuwatibu wagonjwa hao katika kituo
hicho kuna wagonjwa wa aina tatu ambapo wagonjwa wenye msamaha,wagonjwa
wenye bima .
Anasema kwa wagonjwa wenye msamaha kulingana na sera ya
taifa,wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi ,wanaougua Kifua Kikuu (TB)
na watoto wenye umrichini ya miaka mitano watatibiwa bure.
Anasema kwa upande wa wagonjwa wengine watakaofika
katika katika kitengo hicho watatibiwa kulingana na utaratibu wa
daktari husika kwa mgonjwa wake.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI