Friday, 13 September 2013

Elimu ya msingi iwe kidato cha nne

Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi,Dk Shukuru Kawambwa 



Posted  Ijumaa,Septemba13  2013  saa 11:15 AM
Kwa ufupi
Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, bado ni mapema mno kusema kwamba mambo yote yalikwenda kama ilivyopangwa, ingawa wahenga walisema siku njema huonekana asubuhi. 


Wanafunzi wa darasa la saba nchini kote jana walimaliza kufanya mtihani wa kuhitimu masomo ya elimu ya msingi. Tunafarijika kusikia kwamba mtihani huo ulifanyika katika mazingira ya amani na utulivu karibu nchi nzima, jambo ambalo pengine linadhihirisha kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imejifunza kutokana na makosa yaliyofanyika huko nyuma,  hivyo taratibu inaanza kutupeleka kule tunakotaka kwenda.
Kutokana na ukubwa wa nchi yetu, bado ni mapema mno kusema kwamba mambo yote yalikwenda kama ilivyopangwa, ingawa wahenga walisema siku njema huonekana asubuhi. Tulizoea kupata habari mbaya za mambo mengi kwenda mrama kila mtihani huo ulipokuwa ukifanyika, ikiwa ni pamoja na wizi wa mitihani, kucheleweshwa kwa vifaa, wasimamizi kutofika vituoni walikopangiwa na kadhalika.
Kwa siku mbili mfululizo, viongozi wa wizara hiyo katika ngazi zote nchini, wakiwamo Waziri, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo walikuwa wakizunguka katika shule mbalimbali kuhakikisha mtihani huo ulikuwa ukifanyika katika hali inayokubalika. Hii ni tofauti na miaka ya nyuma ambapo viongozi wengi walikuwa wakikaa katika ofisi zenye viyoyozi wakisubiri kuletewa taarifa za mwenendo wa mitihani hiyo, pasipo kujua kwamba taarifa nyingi zilikuwa za kubuni na nyingine zilikuwa zimechakachuliwa.
Kinachotakiwa sasa ni Wizara kujielekeza zaidi katika kutatua matatizo yanayokwamisha elimu ya msingi, badala ya kuridhika tu na mipango, matamko na mikakati sio tu isiyoendana na vitendo, bali pia isiyotekelezeka hata kama inafanywa kwa nia njema. Kwa mfano, Wizara inaonekana kama imepagaa na ‘Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa’ ambao, pamoja na kufanikiwa katika nchi nyingine kama Malaysia, inabidi tafsiri na utekelezaji wake ufanywe kwa kutilia maanani mazingira tuliyomo.
Mpango huo lazima uwe na dira ili uweze kutekelezeka. Kwa mfano, wanafunzi zaidi ya 800,000 waliomaliza jana elimu ya msingi walitayarishwaje ili elimu hiyo iwawezeshe kumudu maisha yao? Je, elimu hiyo inatosha au taifa lijielekeze sasa katika kufanya elimu ya msingi kuwa kidato cha nne?  Mwaka jana wanafunzi asilimia 64 tu waliofanya mtihani huo ndio waliochaguliwa kwenda sekondari, huku asilimia 36 ikiachwa kutokomea mitaani kueneza ujinga na kugawana umaskini.
Bahati mbaya Waziri Kawambwa bado ni mateka wa takwimu zinazompa ndoto za kufaulisha wanafunzi 80 kati ya 100 ifikapo mwaka 2015 katika elimu ya msingi. Alikaririwa juzi akisema mwaka huu ufaulu utaongezeka kutoka asilimia 31 hadi asilimia 60 na kwamba ongezeko hilo litakwenda sambamba na ongezeko la madarasa. Tatizo ni kwamba anasahau kwamba suala la elimu ni mtambuka, kwa maana kwamba kuongezeka kwa ubora wa elimu kunategemea mambo mengine mengi kama vifaa vya kufundishia, vitabu, walimu bora, usafiri, mitalaa sahihi, miundombinu (mabweni, maabara, madarasa) na huduma za maji, afya, nishati, chakula na kadhalika.
Pamoja na kuwapo umuhimu wa kupanua elimu ya msingi kuwa kidato cha nne, tunadhani pia wakati umefika wa kubadilisha mitalaa ili ijikite katika kutoa elimu ya kujitegemea.
Mkazo uwekwe katika elimu ya ufundi, kwa maana ya kuhakikisha angalao kila wilaya inakuwa na chuo kimoja cha kutoa elimu stadi mfano wa VETA. Vinginevyo, majeshi tunayozalisha kila mwaka kutoka shule za msingi yatasababisha  maafa na tutabaki kulia na kusaga meno.

SOURCE: MWANANCHI