Friday, 13 September 2013

Wazazi nchini wanawafahamu vijana wao vizuri?


Na Julieth Kulangwa, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba13  2013  saa 12:35 PM
Kwa ufupi
Changamoto za kimaisha pia zinatajwa kuwa sababu katika malezi na wazazi kutozijua sababu za wazazi kutowajua vijana wao kwa kuwa muda mwingi wanakuwa katika pirika za kutafuta riziki.


Zaidi ya kuifahamu timu ya mpira wa miguu anayoipenda kijana wako au tamthilia anayoifuatilia binti yako, je ni kitu gani kingine hukipenda au hufanya anapokuwa mbali na upeo wa macho yako?
Dar es Salaam. Leo hii ukiambiwa kijana wako ameiba, au ukigundua binti yako ni mjamzito, hautashangazwa au kuwatupia lawama watu wengine?
Monica Makuba, anasema aliwalea watoto wake katika maadili mazuri, alihakikisha wanafika shuleni na kufuatilia masomo yao, kila Jumapili aliwapeleka kanisani  na kuhakikisha wanafuatilia maadili ya dini kwa kuepuka vitendo vyote viovu.
Monica ambaye ni mama watoto watatu anasema kuna mambo mengi ambayo vijana wake walikuwa wakiyajua na kuyafanya ambayo hakuwahi kufikiria kama wanayajua achilia mbali kuyafanya.
“Wakati mwingine kumlea kijana ni sawa na kuzamisha kichwa ndani ya mchanga kwani huwezi kuuona moto mpaka uanze kukuunguza miguu, watoto wetu wanajua vitu vingi kuliko tunavyodhani,” anasema na kuongeza;
“Niliwalea vizuri vijana wangu katika maadili mema na misingi ya dini lakini kumbe kuna mambo mengi walikuwa wakiyafanya bila mimi kujua, mfano siku moja nilishikwa na butwaa baada ya kumshuhudia binti yangu akicheza shoo katika mahafali shuleni, sikujua kama anajua kucheza dansi kiasi kile na sifahamu alijifunzia wapi,” anasema Monica.
Wataalamu wa Saikolojia wanasema vijana wanaishi katika dunia tofauti. Wapo vijana wa kisasa ambao wanaufahamu mkubwa juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea ulimwenguni na wenye ndoto mbalimbali wanazotaka kuzifanikisha baadaye.
Pia wanasema lipo kundi la vijana wanaoishi maisha ya anasa na wasio na maadili, kundi hili linaundwa na vijana wavuta bangi, wabwia unga, wanaopenda kujirusha klabu kila ifikapo mwisho wa wiki na kucheza gemu katika kompyuta.
Kundi la tatu ni lile la vijana wanaoishi chini ya uangalizi wa hali ya juu, wazazi huwapeleka shuleni na kuwarudisha, muda wa ziada huutumia kanisani au msikiti. Kundi hili linatajwa kuwa ni dogo sana katika jamii yetu.
Aidha kundi jingine linaloainishwa na wanasaikolojia ni kundi la vijana wa vijijini. Pamoja na kuwa asilimia kubwa ya maisha ya vijana hawa halijahabarishwa,  ndilo linalotajwa kuathirika zaidi na athari za ngono kama vile magonjwa ya zinaa na mimba zisizotarajiwa.
Sababu kubwa inayolifanya kundi hili kuathirika zaidi ni ile hali ya kujua ngono mapema kabla ya kujua njia zinazoweza kuzuia maambukizi na mimba.
Mtaalamu wa Saikolojia katika kituo cha Ushauri cha NEHOTA, Dk Bonaventura Mutayoba anasema ugumu wa wazazi kutokuwajua katika kipindi hiki unatokana na kasi ya mabadiliko ya kijana.

Mutayoba  anasema katika kipindi hiki kijana huanza kuitafuta ‘identity’ yake, hapa anaweza kufanya chochote anachokiamini na huwa mgumu kuelewa pale anapoeleweshwa tofauti na imani yake.
“Kijana akishafikia balehe huanza kujichunguza, mara nyingi kundi analoliona mbele yake ndilo linaloweza kuwa kioo chake cha kujitazama, kama ni baya ataelekea huko,” anasema Mutayoba.
Aidha Mutayoba anasema maandalizi ya kisaikolojia katika kipindi hiki kwa kuwa mabadiliko yanapoanza kumtokea huwa ni vigumu kwa kuwa pia huamini katika maamuzi binafsi.
“Kujiamria mambo yao wenyewe huwa moja ya imani zao, kijana akisha pevuka hufanya uamuzi katika kile anachokiamini, ndiyo maana ni vizuri kumwandaa na kumtahadharisha juu ya kitakachotokea siku za usoni,” anasema Mutayoba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi na Mtaalamu wa Saikolojia, Karatu Kiemo anasema ujana ni ile hali inayomtokea binadamu pale anapopevuka kimwili na kisaikolojia.Katika kipindi hiki binadamu huanza kujitambua kijinsia.
“Kupevuka kwa mwili na saikolojia huchochewa na homoni, hivyo wakati mwingine huwa vigumu kudhibiti matokeo ya mabadiliko haya, vijana hutarajia mambo mengi wanapofikia kipindi hiki  na hutamani kuyakamilisha yote katika kipindi kifupi,” anasema Kiemo.
Changamoto za kimaisha pia zinatajwa kuwa sababu katika malezi na wazazi kutokuzijua sababu za wazazi kutokuwajua vijana wao kwa kuwa muda mwingi wanakuwa katika pilika za kutafuta riziki.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ilala, Fransisca Makoye anasema  wazazi wengi wanatoa visingizio mbalimbali pale wanapozigundua tabia tofauti za vijana wao ikiwemo hii ya kuwa bize na shughuli za kuwaingizia kipato.
“Tunapokea kesi nyingi za vijana walioshindikana, wazazi huja kwetu wakitaka tuwachukue vijana hao na kuwapeleka katika shule za watoto watukutu, lakini ukitafuta ukweli utagundua kuwa vijana wengi hawaharibiki ukubwani, huanzie utotoni,” anasema Fransica na kuongeza;
“Kijana mwema hutayarishwa kutoka utotoni, tunapopata kesi kama hizi na kuzifanyia uchunguzi mara nyingi huwa tunagundua kuwa kijana huyu hakupata malezi mazuri tangu utotoni, mzazi anayezungumza na mtoto wake na kumwandaa na ujana huwa hasumbuki sana katika malezi,” anasema Fransisca.
Aidha alisema wazazi wengi hupeleka watoto wao katika shule za bweni ili wapate muda wa kufanya shughuli nyingine na huko vijana hujifunza vitu vingi bila wao kufahamu.

SOURCE: MWANANCHI