Kwa ufupi
- Arejea katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Dodoma na kutia saini hati hiyo ya dhamana.
Dodoma. Polisi mkoani Dodoma, wamelazimika
kumrudisha kwa mara ya pili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
katika ofisi za Kituo Kikuu cha mjini hapa, baada ya kusahau kuweka
saini katika dhamana yake.
Mbilinyi maarufu Sugu, anatuhumiwa kumpiga askari, kuharibu kipaza sauti na kuchana koti la mpambe wa Bunge.
Tukio hilo la kurudi kwa mara ya pili katika ofisi
za upelelezi, lilitokeza jana baada ya Sugu kuripoti na kuruhusiwa
kuondoka mahali hapo.
Mbunge huyo ambaye aliitwa na mmoja wa maofisa
wapelelezi wa jeshi hilo, alikuwa tayari ameshaingia ndani ya gari
tayari kwa kuondoka katika eneo hilo.
Akiwa katika hali ya ucheshi na kufikia hatua ya
kugongeshana mikono na afisa huyo wa polisi, aliingia katika ofisi za
upelelezi na kutoka baada ya dakika 15.
Wakili wa Mbilinyi, Tundu Lissu, aliliambia gazeti
hili kuwa waliitwa kwa mara ya pili ili kwenda kusaini dhamana ya
polisi kwa sababu awali hawakufanya hivyo.
Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema waliitika wito wa
jeshi hilo na walipofika waliambiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
unaendelea.
“RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa
Mkoa), ametuambia kuwa atawasiliana na sisi baada ya kama wiki mbili
hivi ili kujua wamefikia uamuzi gani,” alisema:
“Mimi nitashangaa sana kama polisi watampeleka
mahakamani, katiba ya sasa ibara 100 (2), inasema mbunge hatashtakiwa
wala kufunguliwa shauri lolote la madai kwa jambo lolote alilosema ama
kufanya akiwa ndani ya Bunge, alisema.
Alisema hilo neno Bunge limetafsiriwa ndani ya
sheria ya Kinga na Mamlaka ya Bunge, ndani ya Bunge, nje ya ukumbi na
maeneo yote yaliyopo ndani ya uzio wa Bunge.
“Mbunge akifanya lolote ama kusema lolote huwezi
kushtakiwa, nitashangaa sana hao wanaopiga kelele na kundi lao na
Serikali yao wataamua hili jambo liende mahakamani,” alisema.
Kwa upande wake, Mbilinyi, alisema tukio hilo halijamletea usumbufu wowote.
Mbunge huyo alihojiwa Ijumaa, kutokana na vurugu zilizotokea
bungeni Alhamisi iliyopita wakati wa Mjadala wa Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba.
Vurugu hizo zilitokea wakati wabunge wa Chadema,
NCCR-Mageuzi na CUF, walipokuwa wakimzuia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe, asitolewe kwa nguvu na askari wa Bunge ndani ya
ukumbi.
source: Mwananchi
source: Mwananchi