Na Mwandishi Wetu
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Ni kweli tunasimamia mradi wa mabasi yaendayo
haraka, lakini suala la ubomoaji ni la Halmashauri ya Jiji. Wao ndio
wanafahamu mkandarasi na kama alilipwa au hakulipwa,” alisema Mmari.
Dar es Salaam: Halmashauri ya Jiji la Dar es
Salaam ilikiuka taratibu za utoaji wa zabuni ya kubomoa jengo lililokuwa
ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo
(UBT), ambalo lilianguka mwanzoni mwa mwaka huu na kusababisha madhara
kwa watu na mali. Januari 21 mwaka huu, watu wanne walijeruhiwa baada ya
magari yao waliyokuwa wameyaegesha katika eneo la UBT kuangukiwa na
ukuta, huku magari 24 na bajaji nne zikiharibika vibaya.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa
Kampuni ya Makalla Contractors Ltd ndiyo iliyofanya kazi ya ubomoaji
huo, lakini hakukuwa na mkataba wa kazi hiyo baina yake na Jiji la Dar
es Salaam.
Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa, licha ya kutokuwa
na mkataba, Makalla Contractors Co. Ltd wamepeleka kwa uongozi wa jiji
hilo madai ya Sh59, 615, 252 wakitaka walipwe kutokana na kazi hiyo.
“Makubaliano yalifanyika kwa mdomo na kazi
ikaanza, hakukuwa na uitishwaji wa zabuni wala kufanyika taratibu zozote
za kisheria, walipeana kazi hiyo kirafiki na baada ya jengo kubomoka
ndipo walianza kuhaha jinsi ya kuwezesha kulipa fedha hizo,” kilisema
chanzo chetu.
Katika moja ya nyaraka za kampuni hiyo kwenda
Halmashauri ya Jiji, Kampuni hiyo ya Makalla inasema ilipewa kazi hiyo
kutokana na gharama zake kuwa za chini na kwamba iliombwa kuanza
kuitekeleza haraka kutokana na udharura wake kwa ahadi kuwa taratibu
nyingine za kupewa LPO na mkataba zingefuata. Hata hivyo, taratibu za
zabuni zinataka kazi itangazwe na hata kama kungekuwa na dharura
ilipaswa kufuata utaratibu wa ‘single sourcing’ ambao ungewezesha
kuchagua kampuni ya kutekeleza jukumu bila kuchelewa. Meya wa Jiji la
Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusaini
mikataba kwa niaba ya jiji hilo alisema: “Sijawahi kusaini mkataba
unaohusu kampuni hiyo unayoitaja (Makalla) na wala sijawahi kusaini
mkataba kuhusu ubomoaji wa pale Ubungo.” Alipobanwa akitakiwa aeleze
sababu za ubomoaji kufanywa bila yeye kuhusishwa alijibu: “Waulize
watendaji wa Jiji, muulize mkurugenzi maana huo ni wajibu wa watendaji
na siyo wajibu wa Meya, nilichokwambia ni kwamba mimi sijasaini mkataba
wowote kuhusu suala hilo.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es
Salaam, Wilson Kabwe alipoulizwa alisema hawezi kutoa taarifa kuhusu
suala hilo kwenye vyombo vya habari.
“Wewe hizo taarifa umezipata wapi?... Mimi siwezi
kukwambia mkandarasi gani aliyehusika, sitoi taarifa hizo kwenye vyombo
vya habari… unazitaka za nini? Wananchi ndio wamekutuma uwatafutie
taarifa? Wao wanatakiwa wasubiri huduma ikamilike, lakini siyo kumjua
mkandarasi, kalipwa au hakulipwa,” alisema Kabwe.
Malipo kwa Mkandarasi
Wakati Kabwe akihoji maswali lukuki, habari zaidi
zinasema ofisi yake imekuwa katika harakati za kuwezesha Kampuni ya
Makalla kulipwa, na kwamba kinachokwamisha malipo hayo ni kutokuwapo kwa
mkataba wa kazi. Fedha za ubomoaji kiasi cha Sh63 milioni zilitolewa na
Ofisi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na kuhamishiwa kwenye
akaunti za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini imebainika kuwa
kumekuwapo na harakati za fedha hizo kurejeshwa DART.
“Ofisi ya mkurugenzi inaendelea na mchakato wa
kurejesha fedha hizo DART ili Kampuni ya Makalla ikalipwe huko maana ni
ngumu malipo kufanyika hapa kwetu kwa sababu hakuna documents (nyaraka)
za mkataba wa kazi, huwezi kulipa, sasa huko DART nao sijui
watafanyaje,”kilidokeza chanzo chetu katika ofisi za Jiji. Hata hivyo,
Ofisa Mwandamizi wa DART, Jack Meena alisema suala hilo linawahusu
Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na Halmashauri ya Jiji ambao ndiyo
wamiliki wa kituo hicho.
“Sisi kazi yetu ni kuhakikisha eneo la mradi
linakuwa tayari kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo tulifanya tathmini na
kulipa fidia na kumwachia mkandarasi,” alisema Meena.
Msimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
katika Tanroads, Barakaeli Mmari alisema suala hilo linashughulikiwa na
Halmashauri ya Jiji, hivyo waulizwe wenyewe.
“Ni kweli tunasimamia mradi wa mabasi yaendayo haraka, lakini
suala la ubomoaji ni la Halmashauri ya Jiji. Wao ndio wanafahamu
mkandarasi na kama alilipwa au hakulipwa,” alisema Mmari.
Sheria za Ubomoaji
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya
Makalla iliandikiwa barua na Bodi ya Usajili wa Makadarasi (CRB),
ikitakiwa kutoa maelezo ya kuhusika kwake katika kazi hiyo, pia
vielelezo vilivyoonyesha jinsi kazi ilivyofanywa. CRB katika barua yake
ya Mei 9, 2013 kwenda kwa Mkurugenzi wa Makalla Contractors Co. Ltd
ambayo gazeti hili limeiona, ilitaka kampuni hiyo kuwasilisha mkataba wa
kazi, majina ya wataalamu walioshiriki katika kubomoa jengo hilo na
nyaraka za uthibitisho wa malipo yao.
Msajili wa CRB, Boniface Muhegi alikiri kwamba
Kampuni ya Makalla imesajiliwa. “Halmashauri ya Jiji ndiyo waliomwajiri,
ila kulipotokea malalamiko ndiyo tukawauliza (Jiji) wakakiri kwamba
ndiye aliyefanya kazi hiyo,” alisema Muhegi na kuongeza:
“Mwanzoni kulikuwa na ubabaishaji. Tulipouliza
tuliambiwa wenye magari waliambiwa wayaondoe kwanza… hilo ni tatizo la
Jiji, lakini tutaichukulia hatua Kampuni ya Makalla kwa sababu
imesababisha uharibifu wa mali za watu na kwa kutokuzingatia vigezo vya
usalama kazini.” “Katika tathmini zetu tuna alama, kama zikifikia 60 au
70 tunatoa adhabu kulingana na kosa. Inaweza ikawa onyo, kusimamishwa
kwa muda au kufutwa kabisa. Kwa kuwa hili ni kosa la kwanza tutaangalia
vigezo vyetu,”alisema Muhegi.
Septemba 4, mwaka huu gazeti hili liliwasiliana na
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Makalla Moseka ambaye awali
alisema taarifa zote kuhusu suala hilo zinapaswa kutolewa na Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam, lakini baadaye alimtaka mwandishi afike
ofisini kwake kesho yake kwa maelezo zaidi.
Gazeti hili lilifika katika ofisi hizo, chumba
namba tisa cha ghorofa ya 10 katika Jengo la Ushirika, Lumumba, lakini
ofisi hizo zilikuwa zimefungwa, huku majirani zake wakisema kuwa ofisi
hiyo imefungwa muda mrefu.
Baada ya kumkosa, mwandishi alimpigia simu siku
hiyo ya Septemba 5 ambapo Makalla alikanusha kwamba kampuni yake iliwahi
kufanya kazi ya aina hiyo.
“Sikiliza bwana, mimi sikuhusika na kazi hiyo,
inawezekana kuna watu walishafanya kazi kwenye kampuni hii, halafu
wakaenda kufanya kazi kwa jina la kampuni yangu,” alisema Makalla.
Baada ya kubanwa zaidi, Septemba 7, Makalla
aligeuka na kukiri kuhusika na kazi hiyo, huku akitaka mwandishi aonane
naye Septemba 8. Alipotafutwa siku hiyo, alisema kwamba yuko msibani,
hivyo kuahidi kwamba angekuwa tayari kuzungumza Septemba 10.
Gazeti hili lilimtafuta juzi na jana, lakini mara zote alipopigiwa simu alikuwa akikata baada ya mwandishi kujitambulisha.
source: Mwananchi
source: Mwananchi