"Sukari ya nje yatishia viwanda nchini"


Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chizza.

Tishio la viwanda vya sukari nchini kusimamisha uzalishaji kupinga uamuzi wa serikali kuruhusu wafanyabiashara wakubwa kuingiza shehena kubwa ya bidhaa hiyo kutoka nje, limeilazimisha serikali kuingilia kati.

Serikali iliwaruhusu wafanyabiashara wakubwa kuingiza tani 50,000 za biadhaa hiyo kutoka nje ya nchi ili kukabiliana na upungufu uliopo.

Baadhi ya wenye viwanda wanailalamikia serikali kwa kuruhusu sukari hiyo kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru, hivyo kusababisha viwanda vya ndani kuathirika kimapato kutokana na mawakala wa sukari ya kigeni kuuza sukari hiyo kwa bei ya kutupa tofauti na ile inayozalishwa na viwanda vya ndani.

Kutokana na sukari ya nje kuuzwa kwa bei chee mitaani, viwanda vya ndani vinadai hali hiyo imesababisha kuwapo kwa akiba kubwa ya sukari katika maghala yao kutokana na ushindani wa soko.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Christopher Chizza, amesema serikali inaadaa mkutano wa kitaifa ambao utawakutanisha wawekezaji, wafanyabiashara na walaji ili kujadili namna ya kumaliza tatizo hilo ambalo linatishia viwanda vya sukari kusimamisha uzalishaji.

Hata hivyo, alisema mahitaji ya taifa kwa sasa ni zaidi ya tani 500,000 za sukari wakati viwanda hivyo vina uwezo wa kuzalisha tani 380,000 pekee.
¡°Huwezi kusikia kelele toka kwa wananchi wa kawaida kwa sababu sukari inapatikana kwa bei nafuu na hata ningekuwa mimi ningenunua ile ambayo nina uwezo nayo kifedha.

Tumeliona hilo, lakini si nia yetu kama serikali kuona wazalishaji wetu wa ndani wakilalamika,¡± alisema jana na kuongeza: ¡°Wizara yangu imepanga kuwakutanisha walaji, wenye viwanda hivyo na wafanyabiashara ambao wamepata zabuni ya kuingiza sukari ya kigeni. Tunataka tujadili upungufu huu na namna ya kuufanya kila upande uridhike kwa maana hiyo, tunataka waendelee kuzalisha sukari katika viwanda vya ndani.

Kabla ya Waziri Chizza kuekeza nia ya serikali ya kuandaa mkutano huo, Ofisa Mtendaji (Utawala) katika Kiwanda cha Sukari cha TPC, Jaffari Ally, alisema kuzorota kwa soko hilo kunasababishwa na usimamizi mdogo wa mamlaka husika za serikali ambazo zinachelea kudhibiti mdororo huo kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya viwanda vya ndani.

¡°Sukari ya nje bado inangizwa nchini kwa wingi bila ya kulipiwa kodi wakati, sisi wa viwanda vya ndani tunaendelea na uzalishaji. Hali hii kwa ujumla wake imevifanya viwanda vyetu kushindwa kumudu gharama za uendeshaji na kusababisha kuwapo kwa akiba kubwa ya sukari kwenye maghala ya viwanda vyetu na hasa TPC,¡± alisema.

Sukari inayozalishwa na viwanda vya ndani hivi sasa inauzwa katika mikoa ya kaskazini kati ya Sh. 69,000 na 75,000 kwa mfuko wa kilo 50 wakati sukari inayoingizwa kutoka Kenya na nchi yingine za Afrika inauzwa kwa Sh. 50,000 kwa mfuko.

CHANZO: NIPASHE