Wednesday 25 September 2013

Mgogoro EALA ni wivu au masilahi ya kiuchumi?


Na Beatrice Moses, Mwananchi

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 14:18 PM
Kwa ufupi
Wakati Watanzania wakiendelea kujadili uhalali wa baadhi ya wabunge kususia Bunge la Tanzania, mambo yamekuwa yale yale katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Vikao viwili vya Bunge la Afrika Mashariki (EALA), vimevunjika kwa nyakati tofauti baada ya kutokea mgawanyiko miongoni mwa wabunge, hivyo kusababisha Spika Margaret Zziwa kuviahirisha.
Kwa wachambuzi wa siasa, mgawanyiko huo una sura nyingi lakini kubwa ni kuwa unaashiria kulegalega kwa uhusiano na ushirikiano wa nchi wanachama za jumuiya hiyo, huku hali hiyo ikifichwa kwenye kivuli cha madai kuwa vikao hivyo vinafanyika eneo moja tu – Arusha, Tanzania.
Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika EALA, Adam Kimbisa anasema matukio hayo yalichochewa na mambo mengi, ikiwamo siasa na uchumi, hasa baada ya kuonekana kuwapo vikao visivyo vya kawaida pembeni vilivyohusisha wabunge waliosusia Bunge siku ya kwanza.
“Mgogoro ule haukuwa katika sura inayoweza kuonekana na wengi, bali ulichangiwa na baadhi ya wabunge wanachama kuona kwamba Tanzania inanufaika kiuchumi kwa Bunge hilo kufanyika Arusha, lakini hayo ni mawazo ambayo yana ufinyu wa fikra,” anasema Kimbisa.
Kwa kawaida vikao vya EALA huwa na watu kama 70 wakiwamo wabunge 52 kutoka nchi wanachama na maofisa wengine kadhaa ambao huhudhuria, hivyo kuonekana kuwa kwa matumizi yao kama chakula na malazi, wananchi wa eneo husika, Arusha, ndiyo hunufaika kimapato.
Kimbisa anapuuza madai hayo, anasema Arusha ni Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki , pia ndipo lilipo jengo la Bunge la EALA, hivyo si ajabu vikao hivyo kufanyika mahali hapo, licha ya kwamba ni eneo la Tanzania ambayo iliridhia kutoa ardhi kwa matumizi hayo na Serikali ya Ujerumani ikagharimia ujenzi wa makao hayo.
“Katika jengo hilo kila mbunge ana ofisi yake, kwa hiyo jambo la kuzunguka katika kila nchini ni gharama za ziada, lakini wenzetu wakawa na vikao vya pembeni ndipo tukashangaa wamefanya uamuzi wa kususia kikao. Tulipofuatilia na kujua sababu, tulishangaa. 
“Utaratibu ni kwamba kila nchi ina wabunge tisa ambapo lazima katika kila kikao cha Bunge kuwe na wabunge japo watatu, kwa hiyo walipotoka wao tunashindwa kuendelea, lakini nasi baada ya majadiliano tuliona kwamba ni bora tuwakumbushe kwamba kanuni zimewekwa ili zifuatwe kama mwongozo, nasi tulitoka,” anasema.
Kimbisa anasema kutokana na hatua hiyo ya wabunge wa Tanzania ambayo iliwashtua wenzao, ikalazimika kukaa kamati, ndipo wakakubalina kwamba kila nchi wanachama wa jumuiya hiyo yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi nazo zitapata kikao kimoja kutokana na mzunguko utakavyopangwa.
“Haya yote yametokana na mgomo tulioufanya baada ya kuona wenzetu wanatumia isivyo kanuni, Bunge limeridhia vikao viwili kikiwamo cha bajeti na ukaguzi wa mahesabu ambavyo ni vikao muhimu sana katika Bunge vitaendelea kufanyikia Arusha,” anasema.
Kwa uamuzi huo nchi itakayokosa kikao kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014, itakuwa ndiyo nchi ya kwanza kupata kikao cha mwaka ujao wa fedha.
Kimbisa anafafanua kuwa katika ratiba ya vikao vya Bunge la EALA, Tanzania watapanga mahali kitakapofanyikia kati ya Dodoma, Dar es Salaam au Zanzibar kwa kuwa ndiyo yenye kumbi ambazo zina vifaa vinavyohitajika kwa vikao vya Bunge.

Utaratibu ulivyovunjwa
Kwa mujibu wa vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii, juhudi za Spika Zziwa za kujaribu kurejesha hali ya utulivu wa vikao hiyo zilishindikana, alitumia dakika 15 kushawishi wabunge hao, hatimaye akaamua kuahirisha Bunge hilo.
 Aliyeanzisha sakata hilo ni Mbunge wa Kenya, Peter Mathuki aliyetaka hoja yake ya kutaka utaratibu wa kufanyika Bunge kwa mzunguko ijadiliwe kwanza, kitu ambacho hakikuwa sahihi licha ya kwamba aliungwa mkono na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Spika alitoa mapumziko na kushauriana kwa dakika 15 na aliporejea wabunge wapatao 14 tu ndiyo walikubali kuingia ukumbini, wengine waligomea uamuzi wa Spika kukataa hoja ya mbunge  huyo.
Vikao vya EALA hadi mwaka wa fedha June 2012/June 2013 vilikuwa vitano kwa mwaka. Vikao hivyo vimeongezeka kuwa sita ambapo hufanyika kila baada ya miezi miwili, kwa kipindi cha wiki mbili kila kikao.
Wabunge Tanzania nao wasusia
Siku iliyofuata Mathuki aliwasilisha hoja hiyo kwa kufuata utaratibu, lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania nao kuamua kutoka nje wakiwa na msimamo ulioungana na Kamati ya Uongozi ya Bunge kuwa vikao vyote vifanyike katika ukumbi wa Bunge, Arusha.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo, kama wabunge watatu wa nchi moja, wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea Bunge linaahirishwa.
Wabunge wengine isipokuwa wa Tanzania walitaka vikao viendelee kwa mzunguko nchini Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Arusha.
Kimbisa anasema kwa kuwa walijipanga kusababisha mabadiliko walimbakiza ndani Makongoro Nyerere kuendelea na kikao na wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda, ambapo yeye ndiye aliwasilisha hoja kwa Spika kwamba idadi ya wabunge wenzake haijatimia.
Awali, Mbunge wa Tanzaia, Abdullah Mwinyi anatoa msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa walitoka kupinga kitendo cha wenzao kudharau kiti cha Spika na kutoka nje, hivyo nao wanaamua kutoka nje.
“Ilikuwa ni mara ya pili wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi tupinge kuvunjwa kanuni,” anasema Mwinyi.


Mwinyi anasema kitendo cha wabunge wenzao kinadhalilisha kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.
Naye Twaha Taslima anasema kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge ana hoja na anataka Bunge lijadili jambo ambalo si la dharura, ni lazima aiwasilishe kwa Spika saa 24 kabla ya kikao.

SOURCE: MWANANCHI