Na Boniface Meena
Posted Jumanne,Septemba24 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Septemba24 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Eunice alisema aliutambua mwili wa mume wake
alipofika katika Hospitali ya M.P SHAR ambako ndipo ulipohifadhiwa na
kwamba wanafanya taratibu za kuusafirisha kwenda Kakamega kwa ajili ya
mazishi.
Nairobi. Imeelezwa kuwa magaidi waliovamia jengo
kubwa la maduka la Westgate jijini Nairobi, Kenya mwishoni mwa juma
lililopita waliingia na magari matatu aina ya Nissan na kumuua mlinzi
mkuu wa eneo hilo, Morris Adembesa kwa kumpiga risasi nane.
Akizungumzia tukio hilo kwenye Hospitali ya Aga
Khan Nairobi, mke wa mlinzi huyo, Eunice Kavesa alisema ameuona mwili wa
mumewe na kusema una matundu manane ya risasi alizopigwa na magaidi
hao.
Alisema aliuawa baada ya walinzi wenzake kumwita getini ili kuzungumza na magaidi hao ambao walikuwa wamekataa kupekuliwa.
“Walikataa kukaguliwa ndipo walipomwita mume wangu
ambaye ni mkuu wa ulinzi hapo na alipofika tu wakammiminia risasi nane
hapohapo,” alisema mama huyo.
Alisema mume wake alihamishiwa katika kituo hicho
akitokea Mombasa wiki moja iliyopita na siku mauti yalipomkuta ilikuwa
ni siku yake ya nne tangu alipoanza kazi hapo.
Eunice alisema aliutambua mwili wa mume wake
alipofika katika Hospitali ya M.P SHAR ambako ndipo ulipohifadhiwa na
kwamba wanafanya taratibu za kuusafirisha kwenda Kakamega kwa ajili ya
mazishi.
“Ameniachia watoto wawili niliozaa naye na yuko
mwingine, maisha yatakuwa magumu kwa kuwa ninafanya kazi za kawaida tu
na yeye ndiye aliyekuwa akitunza familia,” alisema Eunice.
Wakati akisema hayo mashambulizi yalikuwa
yakiendelea katika eneo hilo la Westgate ambalo limezingirwa na vikosi
mbalimbali vya usalama vya ndani na nje ya Kenya. Jana ilikuwa siku ya
tatu tangu magaidi hao walipoliteka jengo hilo na kuua watu 62 huku
wakiwajeruhi 175.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI