Wednesday 4 September 2013

Miswada ya Serikali bungeni ‘bora liende’


 


Posted  Jumanne,Septemba3  2013  saa 21:6 PM
Kwa ufupi
Tutakuwa hatukosei hata kidogo tukisema Serikali ndio ibebe lawama kwa kuwapo hali hiyo ya aibu na fadhaa. Utendaji na uendeshaji wa taasisi nyeti za kitaaluma kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haupaswi kuwa wa ubabaishaji kama ule tunaoushuhudia katika ofisi nyingi za Serikali ambapo watumishi wengi hawafanyi kazi kwa malengo na uwajibikaji.


Ni bahati mbaya sana kwamba sasa limekuwa jambo la kawaida kwa Bunge kuikataa miswada inayowasilishwa na Serikali kutokana na kuwa chini ya viwango. Ni bahati mbaya pia kwamba Serikali inaona hali hiyo kama ya kawaida. Katika hali ya kawaida tungetarajia kwamba Serikali makini ingefadhaishwa na hali hiyo ya kudhalilika mbele ya Bunge kila wakati.
Katika nchi nyingi duniani, muswada wa Serikali kuondolewa bungeni kwa sababu yoyote ile ni tukio lisilo la kawaida. Ni tukio la aibu kwa Serikali ambapo watumishi husika hulazimika kuwajibika. Hapa nchini matukio ya aina hiyo ni mengi na tafsiri ya hali hiyo ni kuwapo udhaifu mkubwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ikiwa ni pamoja na wizara inayoshughulikia masuala ya sheria na Katiba.
Hatuna chembe ya mashaka wala woga kusema hapa kwamba kiwango cha weledi walichonacho watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sio tu kinatia mashaka, bali pia kinaibua maswali mengi kutokana na nafasi yao kama washauri wa Serikali katika mambo nyeti, ikiwa ni pamoja na kutayarisha mikataba mbalimbali. Hali hiyo pengine inaweza kuwa mwanzo wa kupata majibu kuhusu mikataba mingi ya Serikali ambayo imeonekana katika miaka ya karibuni kuwa mibovu na kutokuwa na manufaa kwa taifa.
Miswada ambayo imeondolewa bungeni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni mingi kiasi cha kutufanya tupoteze hesabu yake. Jambo la kusikitisha ni kuona Serikali ikikaa kimya pasipo kurekebisha hali hiyo kwa kuhakikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inaimarishwa kwa watumishi kupewa vitendea kazi stahiki na mafunzo yanayolingana na uzito wa kazi zao. Tuliwahi kupendekeza kuwa, ajira katika Ofisi hiyo zisitolewe kienyeji kwa sababu majukumu yake yanahitaji watu wenye uwezo na uzoefu mkubwa katika taaluma ya sheria.
Tutakuwa hatukosei hata kidogo tukisema Serikali ndio ibebe lawama kwa kuwapo hali hiyo ya aibu na fadhaa. Utendaji na uendeshaji wa taasisi nyeti za kitaaluma kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu haupaswi kuwa wa ubabaishaji kama ule tunaoushuhudia katika ofisi nyingi za Serikali ambapo watumishi wengi hawafanyi kazi kwa malengo na uwajibikaji. Dhana ya Matokeo Makubwa Sasa, kwa mfano haiwezi kuingia katika vichwa vya watumishi hao kwa sababu inahimiza uwajibikaji, wakati utamaduni wa watumishi wengi ni kulundika na kuzungusha mafaili mezani asubuhi hadi jioni pasipo kuyafanyia kazi.
Tukirudi katika suala la miswada mibovu inayopelekwa bungeni, pengine Serikali ingefanya vyema iwapo ingewaeleza wananchi hatua ilizochukua dhidi ya watumishi wazembe ambao wamekuwa wakisababisha miswada kuondolewa bungeni kutokana na upungufu wa kitaaluma. Tunamheshimu sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, lakini tunadhani pengine amechelewa mno kuwajibika kutokana na miswada inayopelekwa bungeni pasipo kuwa na vichwa au miguu.
Katika Mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma hivi sasa, tumeshuhudia kujirudia kwa hali hiyo ya aibu. Miswada mitatu kati ya sita iliyopelekwa bungeni imeondolewa kutokana na sababu kama hizo, ukiwamo muswada nyeti na muhimu wa Kura ya Maoni. Ni siri iliyo wazi sasa kuwa, hata miswada mitatu iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge ilikuwa na upungufu mkubwa, lakini Bunge hilo liliona ni busara kufunika kombe ili mwanaharamu apite.

source: Mwananchi