Wednesday 25 September 2013

Mwanamke aliyeongoza shambulizi la kigaidi la Westgate adaiwa kuuawa



 
Na Waandishi Wetu

Posted  Jumatano,Septemba25  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Hata hivyo, viongozi wa usalama wa Kenya hawakutaka kuingia kwa undani juu ya taarifa za kifo cha Lewthwaite.

Dar es Salaam/Nairobi. Huku mapambano yakiwa yamepamba moto, anayedaiwa kuwa Kiongozi wa kundi la magaidi lililovamia jengo la kibiashara la Westgate, Samantha Lewthwaite inadhaniwa kuwa ameuawa.
Lewthwaite, ambaye anaitwa kwa jina la utani la ‘Mjane Mweupe’ anadaiwa kuongoza shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu 62 na kujeruhi wengine 170 mjini Nairobi.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Mail la Uingereza, mwanamke huyo inasemekana aliuawa juzi usiku na wanajeshi wa Kenya wanaoshirikiana na maofisa wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) na wale wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Gazeti hilo lilieleza kuwa mwanamke huyo ambaye ni mjane wa mlipuaji wa kujitoa muhanga, Jermaine Lindsay, aliuawa pamoja na magaidi wengine watatu.
Kitendo cha kukutwa kwa mwanamke aliyevalia hijab ndicho kilichowafanya maofisa wa usalama kuamini kuwa mwanamke huyo ameuawa.
Hata hivyo, viongozi wa usalama wa Kenya hawakutaka kuingia kwa undani juu ya taarifa za kifo cha Lewthwaite.
Milio ya bunduki na mabomu vilisikika siku nzima ya jana lakini vyanzo mbalimbali vya polisi vilisema kuwa operesheni hiyo ilikuwa inaendelea vizuri na havikutaka kuzungumzia suala la mwanamke huyo.
Polisi wa Kenya wamekuwa na kazi ya kutegua mabomu, ambayo yametegwa ndani ya jengo hilo ambalo magaidi wamejichimbia.
“Tuna kazi ya kutegua mabomu yaliyotegwa na magaidi ili tuweze kuwafikia na kuwakamata,” ilisema taarifa ya Jeshi la Polisi wa Kenya kupitia Mtandao wa Twitter.
Waziri wa Kenya aibua mapya
Katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Al-Jazeera, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed alikiri kuwa shambulizi hilo liliongozwa na mwanamke huyo wa Uingereza.


“Huyu mwanamke ameshiriki mara nyingi katika vitendo vya kigaidi katika ukanda huu,” alisema.
Kauli ya Mohamed inapingana na ile ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Ole Lenku, ambaye alisema juzi kwamba hakuna mwanamke aliyeshiriki katika shambulizi hilo, bali kulikuwa na wanaume waliovaa mavazi ya kike.
Aliwahi kuja Tanzania
Kwa muda mrefu, Lewthwaite amekuwa akiwakimbia polisi kwa kuvaa hijab akitembelea kati ya nchi za Tanzania, Somalia na Kenya.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, mwanamke huyo amekuwa akiishi kwa kujificha na amefanikiwa kutumia pasi za kusafiria za nchi tofauti.
Amekuwa akitambulika kama raia wa Uingereza na Australia lakini inasemekana amekuwa pia akitumia pasi ya kusafiria inayoonyesha kwamba yeye ni raia wa Afrika Kusini akitumia jina bandia la Natalie Faye.
Mwanajeshi wa Uingereza aokoa watu 100
Askari wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza ambaye alikuwa mapumzikoni Nairobi ameibuka shujaa baada ya kusaidia kuokoa zaidi ya watu 100 katika shambulio hilo.
Wakati wa tukio hilo, askari huyo alikuwa akinywa kahawa kwenye maeneo hayo wakati magaidi hao wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kundi la Al-Shabaab walipovamia.
Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Mail, taarifa za askari huyo kuamua kuingia kazini zilitolewa na mashuhuda aliowasaidia wakati milio ya risasi ikiendelea kusikika kwenye eneo la jengo hilo kwa siku ya nne jana huku kukiwa na taarifa kwamba askari walifanikiwa kuwaua wavamizi sita, kati ya wanaodhaniwa kufikia 13 waliokuwa wakifanya mashambulizi.


Vyanzo hivyo vilieleza kwamba askari huyo ambaye hawezi kutajwa jina lake kwa sasa, alikuwa kwenye Jeshi la Maji la Uingereza na kwa sasa anaishi Nairobi, Kenya.
Jeshi la Uingereza limekuwa likiendesha mafunzo yake katika nchi za nje ikiwamo Kenya na limekuwa likifuatilia kwa karibu raia wa Uingereza ambao wamekuwa wakihusishwa na makundi yenye msimamo mkali.

SOURCE: MWANANCHI