Saturday 14 September 2013

Nazalisha hospitalini, naosha mikono nyumbani


Bryceson akiwa katika utendaji wake wa kila siku 
Na Goodluck Eliona, Mwananchi

Posted  Septemba14  2013  saa 13:17 PM
Kwa ufupi
Katika zahanati ya Kibuyuni iliyopo kata ya Panzuo, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, mama wajawazito wanaokwenda kujifungua hutakiwa kwenda na lita 40 za maji kwa ajili ya huduma ya uzazi na usafi.


Mkuranga. Kwa muda mrefu serikali imekuwa na sera ya kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, hata hivyo katika baadhi ya vijiji hapa nchini huenda sera hizo zikawa hazijafika au hazitekelezwi ipasavyo.
Katika zahanati ya Kibuyuni iliyopo kata ya Panzuo, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, mama wajawazito wanaokwenda kujifungua hutakiwa kwenda na lita 40 za maji kwa ajili ya huduma ya uzazi na usafi.
Zahanati hiyo inayowahudumia zaidi wa watu 5,000 kutoka vijiji vitano vya Kibuyuni, Mburani, Kibudi, Kumluwili na Nyakange, haina maji tangu ilipofunguliwa rasmi Desemba 7, 2001 na aliyekuwa Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Afya kwa wakati huo, Dk Hussein Mwinyi.
Muuguzi wa zahanati hiyo, Baraka Bryceson anasema kwa miaka mitatu aliyofanyakazi eneo hilo, amekuwa akiwasaidia kina mama wajawazito kujifungua bila kuwepo huduma ya maji, huku yeye mwenyewe akilazimika kurudi nyumbani kwake kunawa mikono baada ya kuwahudumia wagonjwa hao.
Ukosefu wa maji
“Hapa mahali hali ngumu sana, zahanati haina maji kabisa hasa wakati huu ambapo mvua hazinyeshi. Kwa kawaida nikisha wasaidia hawa wakina mama, huwa najipaka sabuni mikononi, halafu narudi nyumbani kwenda kunawa,” anasema Bryceson.
Muuguzi huyo anasema hawezi kuisahau siku ambayo alikuwa amebaki pekee yake kazini, ghafla wakati wa usiku walifika wakina mama wajawazito watatu waliokuwa wakihitaji msaada wa haraka.
“Siku hiyo nilikuwa pekee yangu kama nilivyo leo, walikuja wajawazito watatu; mmoja nilimlaza pale, mwingine hapa na mwingine kule ndani (anaonyesha kwa kidole), wakati namsaidia mmoja, wengine walikuwa wanapiga kelele wanahitaji msaada. Ilibidi niwasaidie hivyo hivyo bila hata kunawa mikono, katika mazingira kama hayo unafanyaje?” anahoji na kuongeza kuwa:
“Unajua tena Mungu alivyoweka kujifungua ni usiku, kokote kule wengi wanajifungua usiku, asilimia 80 hujifungua wakati huo.”
Wagonjwa wengi hushindwa kwenda zahanati wakiwa wamebeba maji kutokana na umbali pamoja na ukosefu wa usafiri, huku baadhi yao wakifika zahanati wakiwa wameshajifungua njiani.
“Nimeshawasaidia wajawazito zaidi ya mia moja, kujifungua tangu nilipofika hapa miaka mitatu iliyopita lakini wengi hufika hapa wameshajifungua njiani,” anasema.
Anasema wanawake wajawazito ambao mimba zao ni za kwanza au za tano na kuendelea, hawaruhusiwi kujifungulia katika zahanati hiyo lakini baadhi yao hufika hapo wakiwa katika hali mbaya.

“Mama mmoja mjamzito alikuja kujifungua mimba yake ya saba huku akiwa na hali mbaya, mtoto alikuwa ni mkubwa…tuliita gari la wagonjwa kutoka hospitali ya wilaya, bahati mbaya lilichelewa kufika hata walivyofika kule walichelewa tena zaidi ya nusu saa, yule mama baada ya upasuaji alifariki dunia akiwa wodini,” anasema.
Muuguzi pekee katika zahanati hiyo, Sikitu Swalehe anasema kutokana na ukosefu wa maji, wamekuwa wakipiga deki kwenye majengo ya zahanati msimu wa mvua tu.
“Hapa tunafanya usafi wakati wa mvua tu, hatuwezi kununua maji kwa ajili ya kudeki kila siku, hata wagonjwa wenyewe kuna wakati wanakuja na maji lita tatu, inabidi urudi nyumbani uchukue maji yako uwasaidie,” anasema.
Kauli ya mkunga
Naye mkunga katika zahanati hiyo, Mbusilo Antony anasema ukosefu wa maji ni tatizo kubwa linalotakiwa kuchukuliwa hatua za haraka kwa kuwa limekuwepo kwa muda mrefu bila kuwepo na jitihada zozote za kulimaliza.
Anasema utaratibu wa wanawake kubeba ndoo za maji vichwani kwa umbali mrefu, wakati wanakwenda zahanati umeanza kuzoeleka na kuchukuliwa kuwa hali ya kawaida na wanavijiji baada ya kukosa msaada.
“Wanawake wanatembea umbali mrefu huku wamejitwisha maji vichwani, bahati mbaya maji yenyewe wanayokuja nayo hayatoshi kwasababu mjamzito mmoja anahitaji maji lita 40, lakini mtu anakuja na lita tatu,” anasema.
Anasema inapotokea mgonjwa akafika zahanati bila maji, ndugu zake hutakiwa kwenda kijijini kununua maji kati ya sh 1,000 na 2,000 kwa ndoo moja.
Msimu wa mvua maji hujaa kwenye mapipa yaliyopo katika zahanati, lakini kutokana na kijiji kukosa maji, watu wasiojulikana huvamia na kuiba maji wakati wa usiku.
Salima Rajabu, mkazi wa kijiji cha Kibudi anasema ukosefu wa maji katika zahanati hiyo umemfanya kila mwanamke anayekaribia kujifungua kuanza kufikiria namna atakavyobeba maji.
“Kila mwanamke anayekaribia kujifungua anafikiria namna atakavyokwenda zahanati na maji, wanawake wengi wanaona ni bora waende wakajifungulie katika hospitali za mbali kuliko kupata shida ya kubeba maji,” anasema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kibuyuni, Hamis Dude anasema tatizo la ukosefu wa maji katika kijiji hicho limekuwa kubwa zaidi mwaka huu kutokana na ukosefu wa mvua.

Dude anasema mwaka 2004 shirika la AMREF, likishirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga walijenga kisima katika zahanati hiyo, hata hivyo kisima hicho kilikauka mwezi mmoja baadae.
“Baadaye wataalamu kutoka shirika lingine lisilo la kiserikali walikuja tufanya utafiti wa kuchimba kisima wakasema ili kupata maji ya uhakika katika zahanati kinatakiwa kichimbwe kisima chenye urefu wa mita 110,” anasema na kuongeza kuwa:
“Kwa kweli mpaka sasa sioni kama kuna suluhisho la haraka la kupata maji ya uhakika katika kijiji chetu.”
Ofisa huyo anasema kutokana na ukosefu wa maji, wakazi wengi wa kijiji hicho hawaogi, badala yake hutembea na maji kwenye madumu ya lita tano kwaajili ya kunawa baada ya kumaliza kazi za shambani.
“Asubuhi utawaona watu wanakwenda mashambani na vidumu vya maji kwaajili ya kunawa baada ya kumaliza kazi zao.”
Malengo ya milenia
Mwaka 2000 wanachama wa Umoja wa Mataifa walipanga malengo ya milenia, kwa Kiingereza yaliitwa ‘Millenium Development Goals (MDGs)’, ambayo utekelezaji wake ni kati ya mwaka 2000 na mwaka2015.
Wanachama hao waliweka malengo maneno, lakini lengo la nne na tano yanahusiana na mambo ya watoto na wanawake wajawazito.
Lengo la nne limedhamiria kupunguza vifo vya watoto na lengo la tano limelenga kuboresha afya ya kinamama wazazi, kutokana na hali hiyo ya Mkuranga, Tanzania bado ina safari ndefu katika kuyatekeleza malengo hayo ambapo imebaki mwaka mmoja kufika mwisho.
SOURCE: MWANANCHI