Na Herieth Makwetta, Mwananchi
Posted Septemba14 2013 saa 13:22 PM
Posted Septemba14 2013 saa 13:22 PM
Kwa ufupi
Ugonjwa huu unatajwa kuwapata wanawake wakati wa
ujauzito, pasipo wao wenyewe kujua na matokeo yake hujifungua watoto
wenye uzito mkubwa, walio na matatizo ya kimaumbile na wengine huzaliwa
wakiwa na rangi ya manjano.
Idadi kubwa ya wanawake nchini inaelezwa kuugua
ugonjwa wa kisukari cha mimba kitaalamu ukijulikana kwa jina
la’Gestestional Diabetes’.
Ugonjwa huu unatajwa kuwapata wanawake wakati wa
ujauzito, pasipo wao wenyewe kujua na matokeo yake hujifungua watoto
wenye uzito mkubwa, walio na matatizo ya kimaumbile na wengine huzaliwa
wakiwa na rangi ya manjano.
Wataalamu wanaeleza kuwa ugonjwa huo unashika kasi
duniani na kwamba wanawake wajawazito, ambao huongezeka uzito kwa kasi
katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito wao, wanakabiliwa na hatari
zaidi ya kupata kisukari cha mimba.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi,
Mkuu wa Idara ya Kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH)
ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kisukari, Dk Mohammed J
Mohammed anasema kuwa ugonjwa huo huwapata kinamama hao hasa kipindi cha
miezi sita au zaidi ya ujauzito.
“Kisukari cha mimba humpata mwanamke kipindi cha
ujauzito hasa katika kipindi cha mwisho kuanzia wiki ya 24 na kuendelea.
Kisukari hiki hakidumu kwa muda mrefu kwani kinaweza kupotea mara tu
baada ya mama kujifungua, lakini pia kinaweza kuendelea na hapo tunasema
kimebadilika kuelekea katika hatua nyingine,” anasema Dk Mohammed.
Anasema kuwa idadi kubwa ya wanawake hawafanyi
vipimo vya kisukari cha mimba wanaokuwa wajawazito mijini na vijijini
hivyo kutojua hali zao kiafya na kama wapo katika hatari ya kupata
kisukari cha mimba.
“idadi kubwa ya wanawake hawafanyi vipimo, hawa
hujifungua bila kujua wana tattizo hilo hatima yake linaisha. Lakini
wapo pia ambao huendelea na tatizo hilo na baadaye linakuwa kubwa.”
Uchunguzi mpya unaonyesha kuwa wajawazito
watakaoongeza uzito wa gramu 403.70 kwa wiki, wako katika hatari zaidi
ya kupata kisukari cha mimba ikilinganishwa na watakaoongeza uzito wa
chini ya gramu 272.15 kwa wiki.
Sababu za kisukari cha mimba
Dk Mohammed anasema: “Kila binadamu ana mfumo wa
sukari mwilini mwake na inahitajika, lakini inategemea sukari ile
inaingia kwa kiasi gani mwilini na matumizi yake. Kupendelea kula
vyakula vyenye sukari kwa wingi ikiwemo soda na vyakula vingine vyenye
kuongeza sukari mwilini kunasababisha kongosho kuchoshwa, lakini pia
kuna sababu zinginezo.”
Anaeleza kuwa wakati mwingine ni usugu wa homoni
kutumia chembe hai na hii hutokea kwa watu wenye uzito mkubwa kwani
homoni ile inakuwa imezungukwa na mafuta. Pia husababisha ongezeko la
baadhi ya vichocheo kama Progesterone, Estrogen na free Cortisol
vinavyoongeza kiwango cha sukari katika damu.
Wakati huohuo kichocheo cha Human Placental
Lactogen huzuia insulin kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo kusababisha
kiwango cha insulin kuongezeka katika damu.
Dk Mohamed anafafanua kwamba, mwili unaposhindwa kutengeneza
insulin ya kutosha kupambana na ongezeko la sukari katika damu, kisukari
cha mimba hutokea, mara nyingi hutokea mimba ikiwa na umri wa miezi
mitano au zaidi na kwa kawaida huisha wiki sita baada ya mwanamke
kujifungua.
Dalili zake
Kisukari cha mimba kina dalili kadhaa, lakini kwa
kawaida huainishwa kwa vipimo (screening), vinavyochukuliwa wakati wa
ujauzito.
Kwa mujibu wa Dk Mohammed dalili za kisukari cha
mimba ni chache na mara nyingi hazionekani kwa uharaka zaidi ya
kujitokeza baada ya kujifungua, hivyo kuwashauri wajawazito kupima
kisukari mara kwa mara.
Anasema kuwa mwanamke anashauriwa kupima kisukari kabla ya ujauzito, anapokuwa mjamzito na baada ya ujauzito.
Mtaalamu huyo anabainisha kuwa kupimwa kwa tatizo
hilo husaidia mama kuanza matibabu mapema na kuondoa sukari iliyojaa
katika kondo.
Anataja dalili za mwanamke mwenye kisukari cha
mimba kuwa ni kuongezeka uzito siku za mwanzoni mwa mimba, kuwepo
historia ya kuwa na kisukari katika familia, kuwahi kujifungua mtoto
mwenye uzito mkubwa na mimba kuharibika mara kwa mara.
Nyingine ni historia ya kisukari cha mimba, mkojo
kuwa na sukari mara kwa mara, kuzaa mtoto mfu, uzito au unene
uliokithiri, shinikizo kubwa la damu la muda mrefu au umri zaidi ya
miaka 35.
Matibabu yake
Dk Mohamed anasema kuwa aina hii ya kisukari
huchomoza wakati wa mimba, na ili kulinda mtoto tumboni mara nyingi
inabidi mja mzito apewe insulin ili sukari iliyo katika damu iwe kati ya
4-8mmol/l.
Anabainisha kwamba ikwa mwanamke atakuwa na sukari
nyingi kwenye damu yake akiwa na mimba, kutakuwa na uwezekano mkubwa
kwamba, mtoto atazaliwa na athari tofauti au uzito uliopitiliza.
Baada ya kugundulika na kisukari cha mimba, mama
hushauriwa kutumia vyakula vya sukari visivyofyonzwa kwa uharaka kama
soda na juice, badala yake atumie matunda halisi yatakayomsaidia sukari
yake kutopanda kwa uharaka na pia nyuzinyuzi za matunda zitamsaidia
katika mmeng’enyo mzuri wa chakula. Daktari bingwa huyo anaeleza kwamba
mama atapewa dawa aina za insulin ni chembechembe, lakini kama pia
atakataa hizo, hupatiwa dawa za vidonge na huyu atalazimika kupima
sukari yake mara kwa mara.
Athari zitokanazo na ugonjwa huu
DK Mohamed anabainisha kuwa kuna hatari inayoweza
kumpata mtoto atakapozaliwa ambayo ni kifo iwapo sukari yake itashuka
kwa kasi, ndio maana mtoto mkubwa anapozaliwa hupewa glucose ili
aendelee kupata ile sukari kwa kipindi fulani. Pia mtoto anaweza
kuzaliwa na matatizo ya kimaumbile, kuzaliwa na rangi ya manjano.
Mama anaweza kupata athari za kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kwa kuwa mtoto atakuwa na uzito wa juu sana.
Asilimia 4 ya kina mama ambao watapata kisukari
wakati wa ujauzito wanakabiliwa na hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari
baadaye maishani mwao, hiyo ikiwa ni pamoja na watoto wao.
Mtoto kuzaliwa na uzito wa juu mtoto mwenye afya
anatakiwa kuzaliwa na uzito kuanzia kilogram 2.5 hadi kilogram 4 akizidi
zaidi ya hapo hilo ni tatizo jingine. Mtoto anapozaliwa na uzito mkubwa
mara nyingi huwa na njaa sana ndio maana hupewa nyongeza ya glucose na
atakuwa anakula sana kwa kuwa alikuwa akipata sukari hiyo alipokuwa
tumboni. Dk Mohammed anabainisha kuwa kondo analokaa mtoto
hujitengenezea sukari nyingi na hivyo kupelekea mtoto aliyemo ndani
kuitumia sukari hiyo inayomfanya azidi kukua siku baada ya siku. Anasema
mtoto atakapokuwa anakula sukari hiyo moja kwa moja mwili wake unazidi
kutengeneza mafuta kwa wingi.
Anasema tatizo hili pia linawapata zaidi watu wa
makabila ya Afrika, Wamarekani Weusi, Afrocaribeans, Hispania, nchi za
Pacific na Kusini mwa bara la Ulaya.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI