Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Septemba14 2013 saa 13:2 PM
Posted Septemba14 2013 saa 13:2 PM
Kwa ufupi
Imebainika kuwa miongoni mwa mbinu mpya wanazotumia
ni kusafirisha dawa hizo kwa kutumia ndege za mizigo ambapo huweza
kuweka dawa za kulevya kwenye mdoli, jarida, makopo ya maziwa ya watoto,
vinyago vya kimakonde na kuutuma kama kifurushi kwenda sehemu nyingine.
Wakati vyombo vya sheria vikiendelea kupambana
na biashara ya dawa za kulevya nchini, wasafirishaji hao kila siku
wanaendelea kuwa wabunifu na kubuni mbinu mpya na za kutisha za
kusafirisha dawa hizo kutoka eneo moja hadi lingine.
Imebainika kuwa miongoni mwa mbinu mpya
wanazotumia ni kusafirisha dawa hizo kwa kutumia ndege za mizigo ambapo
huweza kuweka dawa za kulevya kwenye mdoli, jarida, makopo ya maziwa ya
watoto, vinyago vya kimakonde na kuutuma kama kifurushi kwenda sehemu
nyingine.
Pia, wasafirishaji hao kwa sasa wanaweza kuvaa
kama watawa (masista na mapadre) na kujifanya wameshika rozari zao
wakisali na kumbe wamehifadhi dawa hizo ndani ya mavazi yao makubwa.
Pia, imebainika kuwa siku hizi si lazima
kusafirisha dawa za kulevya zilizo tayari bali kemikali zinazotumika
kutengeneza dawa za kulevya(kwa mfano amphetamine inayoweza kutengenezwa
maabara), husafirishwa na baada ya kufika kemikali huchanganywa katika
maabara za siri na dawa za kulevya huanza kusambazwa mitaani.
Kamishna Mkuu wa Polisi Kitengo cha Dawa za
Kulevya, Alfred Nzowa alisema wasafirishaji hao wanabuni mbinu mpya kila
kukicha lakini alitaja mbinu kuu ya kusafirisha mzigo mkubwa ni kwa
njia ya meli au ndege za kukodi, za abiria au binafsi kupeleka mzigo
kutoka nchi moja hadi nyingine.
“Dawa nyingi zinazosambazwa hapa zinakuja kwa njia
ya meli. Zinapofika kwenye mipaka ya bahari ya nchi za Afrika Mashariki
kama Mombasa na Dar es Salaam hupakuliwa na kuwekwa katika boti ndogo
ndogo ziendazo kwa kasi na kusambazwa,” alisema Kamishna Nzowa.
Kwa mfano, ripoti ya mwaka 2013 ya Umoja wa
Mataifa kitengo cha Uhalifu na Dawa za Kulevya (UNODC) inaeleza kuwa kwa
sasa njia inayotumika kupitisha dawa za kulevya kufika Tanzania ni
maeneo ya visiwani hasa Tanga na Zanzibar, ambapo wasafirishaji hutumia
boti binafsi ndogo. Mzigo unaposhushwa hapa hupelekwa kama mizigo midogo
midogo Dar es Salaam.
Nzowa alisema mbinu nyingine iliyobuniwa na
inayotumiwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ni kusafirisha
kwa kutumia ndege ndogo binafsi, ambazo huweza kupita bila kukaguliwa.
Nzowa alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni
mbinu nyingi kila siku ili kuwazidi ujanja wakaguzi walio katika
viwanja vya ndege na katika mipaka, ambapo kwa sasa wasafirishaji wadogo
wanaweza kuzificha katika soli za viatu, sehemu za siri au katika
matiti.
“Tuliwahi kumkamata msichana mmoja wa Kifilipino
ambaye kwa wakati mmoja alitumia mbinu tatu kuficha dawa aina ya heroin.
Aliweka gramu 400 katika viatu, ambapo gramu 200 kiatu kimoja na gramu
200 katika kiatu cha kushoto. Alificha kiasi kingine kwenye matiti na
kiasi kingine sehemu za siri,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema wasafirishaji hao wanaendelea kubuni
njia mpya kila siku, ambapo kwa sasa wamejikita zaidi kusafirisha kwa
njia ya meli na ndege ili kuweza kusafirisha kiasi kikubwa bila
kugundulika.
“Wale wasafirishaji wa ndani ya nchi wanatumia
njia kama hizo za kumeza, lakini wale manguli wanatumia meli za kukodi
na ndege binafsi. Wanaweza kusafirisha hata kilo 800 kwa wakati mmoja,”
alisema Nzowa.
Msemaji wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya
nchini Florence Mlay, alisema wasafirishaji hao kwa sasa wanatumia meli
binafsi kusafirisha dawa hizo na baada ya kufika Tanzania zinashushwa
katika bandari ndogo ndogo ikiwamo Oysterbay.
Mlay alisema kutokana na watuhumiwa wanaokamatwa
Tume hiyo imegundua mbinu nzito zinazotumika kusafirisha dawa za
kulevya, kwa mfano kuweka dawa za kulevya katika chupa za poda, biblia
au majani ya chai.
“Wanaweka poda, katikati unga, kisha poda juu, ni
vigumu kubainika. Lakini wengine wanatumia ma ‘hotpot’ ya vyakula
kuzisindika dawa hizo” alisema Mlay.
Tume hiyo imegundua mbinu nyingine kama ya kutumia
biblia ambapo wanachana karatasi katikati ya biblia kisha wanazifunga
dawa kwa utaalamu mkubwa kiasi cha ‘scanner’ kutoweza kuzibaini.
Karatasi maalumu
Mlay alisema wasafirishaji wanatumia mbinu ya
kuifunga mizigo hiyo kwa kutumia karatasi maalumu, ambayo huzuia mashine
ya kukagulia mizigo kubaini utofauti wa mzigo huo na dawa za kulevya.
Kwa mfano bangi huweza kufungwa katika pakiti za majani ya chai na kufungwa kwa karatasi hiyo bila ‘scanner’ kugundua.
Chanzo kimoja cha habari ambacho kiliwahi kuwa
mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na mtumiaji, alizungumza na
Mwananchi na kusema kuwa njia nyingine ya kushangaza inayotumiwa na
wasafirishaji hao ni kuwatumia watoto wadogo ambao bila kufahamu
hubebeshwa dawa hizo na kupita uwanja wa ndege au mipakani bila
kukaguliwa.
“Dawa zinafungwa vizuri, zinawekwa katika begi la
mgongoni la mtoto, kisha dawa zinapuliziwa marashi ili kuficha harufu.
Si rahisi watoto kuhisiwa kuwa wamebeba dawa hizo,” kilisema chanzo
chetu.
Alieleza mbinu nyingine kuwa wanaposafirisha dawa
hizo kwa njia ya ndege za mizigo huweza kufunga boksi lenye dawa hizo
kisha nje kuandika ni chakula cha mbwa, vitabu, matunda au mboga za
majani na kumbe ndani kuna dawa hizo. Imebainika kuwa wakati mwingine
wasafirishaji huweza kushonea dawa za kulevya katika ngozi ya mnyama,
kisha kuificha na mbwa wa uwanja wa ndege wasiweza kubaini.
Chanzo hicho kilitaja mbinu kama kuficha dawa
katika soli za viatu, katika chupa za maziwa ya watoto, au kuzisafirisha
kwa kutumia mtu ambaye hajui alichobeba ni nini lakini watumaji
wanakuwa wameufunga kwa ujanja.
Wasafirishaji hao inaelezwa kuwa wakati mwingine
wanatumia magamba ya konono wa baharini kusweka dawa hizo, kisha huziba
kwa gundi na kuweka katika mizigo yao na kuipitisha mipakani.
Ripoti ya UNODC inaeleza kuwa kwa mwaka 2012 pekee, Watanzania
zaidi ya 400 walikamatwa kwa kujaribu kusafirisha kilo 260 za heroin na
kilo 151 za cocaine.
Hivi karibuni watanzania wawili walikamatwa nchini
Ethiopia wakisafirisha dawa za kulevya huku meli ya Tanzania ya Mv Gold
Star ilikamatwa na tani 30 za bangi.
Pia Julai mwaka huu wasichana wawili wa kitanzania
walikamatwa uwanja wa ndege wa OR Tambo wakiwa na mzigo mkubwa wa dawa
za kulevya aina ya methamphetamine (Tik).
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI