Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Septemba21 2013 saa 8:40 AM
Posted Septemba21 2013 saa 8:40 AM
Kwa ufupi
Akitoa uamuzi wake jana kuhusu ombi la upande wa
mashtaka, Jaji Grace Mwakipesile alisema anashindwa kuelewa kwa nini
upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ombi hilo la msingi la
kisheria, wakati kesi hiyo ikihamishiwa Mahakama Kuu.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam, imeridhia kuongeza mashahidi wawili muhimu wa upande wa mashtaka
katika kesi ya kihistoria ya dawa za kulevya zenye thamani ya Sh225
milioni.
Akitoa uamuzi wake jana kuhusu ombi la upande wa
mashtaka, Jaji Grace Mwakipesile alisema anashindwa kuelewa kwa nini
upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ombi hilo la msingi la
kisheria, wakati kesi hiyo ikihamishiwa Mahakama Kuu.
“Kinachonishangaza ni upande wa mashtaka kwa
makusudi na uzembe walishindwa kuwasilisha maombi hayo ya kuongeza
mashahidi wawili, wakati kesi ilipokuwa ikihamishwa,” alisema kwa
mshangao Jaji Mwakipesile.
Jaji Mwakipesile aliongeza kuwa: “Kutokana na
ukweli kwamba vidhibiti viliorodheshwa na mashahidi wawili walitajwa
wakati wa kusikiliza kesi, mahakama hii inachukuliwa ushahidi huo siyo
wa kutisha. Na kwa kuwa ushahidi huo ni muhimu katika kesi hii, nakubali
ombi la kuwaongeza mashahidi hao kutoa ushahidi,” alisema Jaji
Mwakipesile wakati akitoa uamuzi wake.
Kesi hiyo inawakabili watuhumiwa tisa akiwamo raia
wa Kenya, Mwanaidi Ramadhani Mfundo, maarufu kwa jina la Mama Leila au
Naima Mohammed Nyakiniwa.
Mama Leila kabla ya kukamatwa Juni 2011 eneo la
Mbezi, Dar es Salaam, pia alikuwa akitafutwa na Serikali ya Marekani kwa
makosa kama hayo.
Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Ben Ngare
na Anthony Karanja ambao ni raia wa Kenya na Watanzania watano Sara
Munuo, Alma Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi na Rajabu Juma.
Mashahidi walioongezwa ni Bertha Mamuya kutoka
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambaye ndiye aliyezifanyia uchunguzi
dawa hizo na kisha kuzifunga, pamoja na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)
Neema kutoka Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya ambaye pia ndiye mtunza
vielelezo hivyo.
Awali wakili wa utetezi, Evod Mmanda alitumia
Kifungu cha 289 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),
kupinga hoja ya upande wa mashtaka ya kutaka kuongeza mashahidi wawili.
“Mheshimiwa Jaji, Prosecution (upande wa mashtaka)
waliomba jana ahirisho ili waweze ku- file (kuwasilisha) hicho
walichokiomba (taarifa ya kumwongeza shahidi), ruhusa umeitoa leo kwenye
uamuzi wako, hivyo walitakiwa wa-file notice yao hiyo baada ya uamuzi
wako (wa leo),” alisema na kuongeza:
“Hivyo hakuna notisi halali hapa mahakamani.
Notisi halali ni ile watakayoiwasilisha baada ya uamuzi wako. Kwa hiyo
sisi tunasema kuwa hadi sasa hakuna notisi halali ya kuita mashahidi wa
ziada.
“Kama Mahakama yako itaikubali hii wanayoita
notisi, ingawa sisi tunasema siyo notisi halali, basi tunaomba Mahakama
yako ione kuwa haikutolewa ‘in a reasonable time’ (wakati mwafaka).”
“Hawa wanatajwa kuwepo katika mchakato tangu mwanzo. Mamuya
anakiri kupokea kifurushi (bahasha yenye vielelezo) Juni 16, 2011, hadi
leo ni miaka miwili na miezi mitatu imepita. Hivyo walijua uwepo wa
Mamuya mapema.
Huu si wakati mwafaka,’’ alisema Wakili Mmanda.
Hata hivyo, alisema hawana maelezo ya maandishi ya Mamuya wala ya ASP
Neema huku akidai kuwa maelezo ya ASP Neema yanaonyesha kuwa yameandikwa
Juni 11, mwaka huu wakati hatua ya maelezo ya kesi ilishakamilika.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Prosper
Mwangamila alidai kuwa katika kesi zote za jinai si jukumu la upande wa
mashtaka kuwapatia upande wa utetezi nyaraka mbalimbali wanazokusudia
kuzitumia katika kesi, bali Mahakama.
“Notisi wanayoitaja iko mahakamani tangu jana,
hivyo utaratibu uliotumika wao kupata nyaraka nyingine ndio unaotumika
kuwapatia notisi hii. Hivyo hoja ya upande wa mashtaka kuchelewa kuwa
‘serve’ (kuwapatia) haina msingi,” alisema Wakili Mwangamila.
Alisema taarifa hiyo iko mahakamani kisheria kwa
mujibu wa Kifungu cha 289 (1) na (2) cha CPA na kuiomba mahakama ione
kuwa imewasilishwa katika muda mwafaka.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI