Saturday, 21 September 2013

Shahidi wa Mramba azua mvutano wa kisheria


Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba 

Na James Magai, Mwananchi

Posted  Septemba21  2013  saa 8:48 AM
Kwa ufupi
Ni kati ya mawakili wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayowakabili.

Dar es Salaam. Shahidi wa Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba, Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Felician Busigara, jana alizua mvutano mkali kati ya mawakili wa mashtaka na wale wa utetezi.
Busigara ambaye ni shahidi wa pili wa Mramba, alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ili kumtetea Mramba katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi za umma na kuisababishia Serikali hasara.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Wanakabiliwa na mashtaka ya kuisamehe kodi isivyo halali, Kampuni ya Ukaguzi wa Madini ya Alex Stewart (Assayers) ya Uingereza na kuisababishia Serikali hasara ya Sh11.7 bilioni.
Mvutano huo ulizuka baada ya upande wa mashtaka, kumpinga shahidi huyo, kutoa ushahidi wake kama mtaalamu wa masuala ya kodi, ukidai kuwa upande wa utetezi haukufuata taratibu za utoaji wa maoni kama mtaalamu.
Wakati akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na Wakili Herbert Nyange, anayemtetea Mramba, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya, alikuwa akinyanyuka mara kwa mara na kuweka pingamizi shahidi huyo kutoa ushahidi kama mtaalamu.Mbali na Wakili Tibabyekomya kupinga, mahakama pia ilikuwa ikihoji sababu za shahidi huyo kutoa ushahidi kama mtaalamu.
Akiongozwa na Wakili Nyange, Busigara alidai kuwa sheria ya kodi ya mapato inamtaja mwenye mamlaka ya kusamehe kodi kuwa ni Waziri wa Fedha.
“Nyange kuna haja gani ya kumleta shahidi anayezungumzia sheria, sheria zipo katika vitabu, hata wakili unaweza kuzungumzia hizo sheria katika majumuisho yako, mashahidi wako wasituambie kuhusu sheria,” alihoji Jaji Rumanyika.
Shahidi aliendelea kutoa ushahidi kwa kusoma kipengele kimoja cha mkataba kati ya Alex Stewart na BoT, akidai kuwa mkataba huo ulionyesha kwamba atakayelipa kodi ni benki na kampuni itapata fedha yake baada ya kodi.
Jambo lililosababisha Jaji Rumanyika kuingilia tena kati.

SOURCE: MWANANCHI