Posted Septemba21 2013 saa 8:34 AM
Kwa ufupi
Hatua ya kufanya mkutano huo, ilifikiwa jana baada
ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye
leo jijini humo.
Dar es Salaam. Vyama vya siasa vya upinzani vya
Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, leo vitafanya mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Jangwani kuhamasisha wananchi wapinge kile wanachodai ni
hujuma dhidi ya Mchakato wa Katiba Mpya.
Hatua ya kufanya mkutano huo, ilifikiwa jana baada
ya wenyeviti wa vyama hivyo kumvamia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini
(IGP), Said Mwema ofisini kwake wakipinga kitendo cha Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dar es Salaam kupiga marufuku maandamano waliyokuwa wayafanye
leo jijini humo.
Katika mkutano wao na IGP Mwema, viongozi hao
walikubaliana maandamano hayo yasitishwe kwa sababu za kiusalama, lakini
wafanye mkutano huo wa hadhara.
Wenyeviti hao wa vyama vya Upinzani, James Mbatia
wa NCCR-Mageuzi, Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba
(CUF), ambao walikutana na Mwema jana mchana.
Hatua ya viongozi hao ilitokana na tamko
lililotolewa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam,
Suleiman Kova kusitisha maandamano ya vyama hivyo yasifanyike.
Kova alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kuhofia
yatasababisha kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi pamoja na kuwepo
taarifa za kiintelijensia kwamba yatakuwa na vurugu.
Tamko hilo liliwakera viongozi wa vyama hivyo
vitatu vilivyotangaza kushirikiana katika kupinga kile wanachodai ni
uporaji wa haki ya wananchi kutunga Katiba yao.
Mazungumzo wenyeviti hao na IGP yalianza saa 6
mchana na kumalizika saa 11 jioni, ambapo walitoa taarifa ya pamoja
kuhusu waliyokubaliana.
Akitangulia kutoa taarifa hiyo, kwa niaba ya
wenzake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema: “Tumekubaliana
kesho tutafanya mkutano Viwanja vya Jangwani. Tumekubaliana kusitisha
maandamano hadi Oktoba 5, (mwaka huu).”
Aliongeza kuwa wamekubaliana pia kwamba watafanya mkutano mwingine wa hadhara Visiwani Zanzibar, Jumatano ijayo.
Hata hivyo, katika taarifa ya pamoja, ulitokea kuhitilafiana kwa kauli, pale IGP Mwema alipokuwa akitoa ya upande wake.
Hali hiyo ilitokana na kauli ya Profesa Lipumba
kusisitiza kuwa mikutano na maandamano ni haki ya msingi kwa vyama vya
siasa na kwamba wanachopaswa ni kutoa taarifa kwa polisi na wala siyo
kuomba kibali.
Awali, wakati Mwema akihitimisha taarifa hiyo ya pamoja alisema
kuwa wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali cha maandamano hayo ya Oktoba
5.
Alisisitiza kuwa kazi ya polisi ni kuhakikisha
usalama wa raia na mali zao, hivyo wanasiasa hao wanapaswa kuomba kibali
na baada ya polisi kuchunguza watakuwa na mamlaka ya kuridhia au
kukataa ombi lao.
Mwema alisema haoni haja ya kuwepo malumbano na
wanasiasa hao katika suala hilo kwa sababu lengo lao ni moja nalo ni
kudumisha ustawi wa jamii.
“Wote tunajenga nyumba moja, sioni sababu ya kugombania fito,” alisema Mwema.
Mzozo wa Katiba
Mzozo wa vyama vya siasa vya upinzani ulianzia
kwenye Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma,
lakini sasa umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo vimetangaza azma ya
kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea
na mchakato wa Katiba Mpya.
Viongozi hao wa upinzani wanadai kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho.
Wanadai kuwa hali hiyo inatoa mwanya kwa Serikali
inayoongozwa na CCM kupitia kwa rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa
wajumbe husika.
Vyama hivyo viliazimia kuanza rasmi leo harakati za kuhamasisha umma kupitia maandamano na mikutano ya hadhara.
Ndoa hiyo ya wapinzani waliifunga, Septemba 15,
kwa kuandika historia nyingine mpya kwenye tasnia ya siasa za Tanzania
wakipinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa
mwaka 2013.
Wanadai mapendekezo mengi yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalipendekezwa na
vyama hivyo, hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja na ya
Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha
umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na
mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Vyama hivyo vinadai kuwa vinaungwa mkono na makundi mbalimbali
yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa,
wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya
wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu
wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Misimamo ya wenyeviti
Profesa Lipumba anasema wanachopigania ni
kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, anaongeza kuwa
suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Tunamshauri Rais Kikwete asisaini muswada huu,
aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na
mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda
kumwona, ila aurejeshe bungeni,” anasema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima
na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa
kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza
kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mbatia anasema historia ya nchi inaonyesha kuwa
waasisi wa kutaka sauti, kauli na mawazo ya umma isikike katika kudai
Katiba Mpya ni vyama vya upinzani.
“CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania
kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini
Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo. CCM inaweza kufa,
lakini Tanzania itaendelea kubakia” anasema na kuongeza;
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu
wanakosea, hatuwezi kuangamiza wazo letu la kutaka Katiba Mpya, katika
taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo
yao.”
Mbowe anasema wameamua kuweka pembeni tofauti zao
kwa ajili ya kudai Katiba Mpya ya Watanzania wote, kwamba hata
wanahabari wanatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyombo vyao vya habari
vinavyomilikiwa na vyama vya siasa, kuwa wakweli katika kudai Katiba
Mpya.
“Waandishi wa habari msiwe vipaza sauti vya
watawala bila kutafakari kwa kina Tanzania ya miaka 100 ijayo itakuwaje,
wanahabari mnaweza kutunyima Katiba Mpya au mkatunyima kama ikitumika
vibaya,” anasema.
Anaongeza kuwa amani ya nchi inaweza kuvurugwa
kama mchakato wa katiba utahodhiwa na chama kimoja cha siasa (CCM),
“Ikiwa hivyo, sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue
kuwa kuna misingi ya kuipata amani hiyo, amani inapatikana kunapokuwepo
na haki.”
Huku akinukuu kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere cha ‘Freedom and
Unity’, anasema, “Ni rahisi mno kuliwasha taifa la watu ambao
wamekwazika, taifa hili watu wamekwazika sana. Mchakato wa katiba
unaweza kutibu majeraha makubwa ambayo yanalikabili taifa.”
Anasema fursa adimu ya kupata Katiba Mpya
inapotezwa na bunge na CCM na anasisitiza kwamba wapinzani watatumia
kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea ili washiriki
katika kuidai katiba iliyotokana na mawazo yao.
“Wapinzani hatutarudi nyuma na hatutakubali nchi
kurejeshwa chini ya uongozi wa katiba ya sasa. Hilo wenzangu (wenyeviti
wenzangu) naomba mnielewe, Chadema hatukubali na naomba na nyinyi
msikubali, maana ndani ya CCM kuna kundi linataka kurudi katika katiba
hii tunayoilalamikia,” alisema.
Anasema katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere
alisema, ‘Kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa
makini’, kwamba hoja ya kutaka Amani itaharibiwa na wale wenye dola,
siyo vyama vya upinzani.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI