Na Suzy Butondo, Mwananchi
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 10:11 AM
Posted Alhamisi,Septemba12 2013 saa 10:11 AM
Kwa ufupi
Ayubu anasumbuliwa na tatizo la saratani ya
shingo, hivyo kusababisha shingo yake kuvimba na kumfanya ashindwe kutoa
sauti ipasavyo kwani sehemu kubwa ya koo lake imeziba.
Joseph Ayubu ni mkazi wa Kijiji cha
Nyenze, Shinyanga.Ugonjwa unaomsumbua unaendelea kumwathiri, huku akiwa
hana uwezo wa matibabu.
Maisha yamejaa changamoto, unaweza kulia kwa sababu ya tatizo hili, mwingine akalia kwa lile.
Wataalamu wa saikolojia, wakiwemo Fernald LD na
Hockenbury Hockenbury kutoka New Zealand, wanasisitiza katika
machapisho yao kadhaa yakiwemo kitabu cha Life is like this, yaani
maisha ni kama hivi, kwamba unapokuwa na tatizo, tuliza kichwa, tafakari
sababu hasa ni nini na nini cha kufanya ili kuondokana na hali hiyo.
Ilimradi uko hai, shida zipo, huna sababu ya
kukata tamaa, cha msingi chukua hatua kuzishinda shida zinazokusumbua,
ikiwezekana shirikisha wengine.
Mfano wa Joseph Ayubu
Joseph Ayubu (40) mkazi wa Kijiji cha Nyenze
wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga, kwa miaka mingi amekuwa akihangaika
kupata tiba ya tatizo lake bila mafanikio.
Ayubu anateswa na ugonjwa wa kansa, hali yake kwa
sasa ni mbaya, anatokwa na usaa mwingi; akiukinga usaha unaotoka
shingoni, kikombe hujaa ndani ya dakika moja.
“Nimevumilia mno, kadri siku zinavyokwenda mbele
naona kifo kinakuja. Sitaki kuamini kama ulimwengu wote au Watanzania
wote wanaweza kuwa na roho ngumu ya kushindwa kuniokoa, naomba msaada
niondokane na shida hii,” anasema Ayubu.
Anawaomba wasamaria wema wamchangie fedha ili akatibiwe katika Hospitali ya KCMC iliyoko mkoani Kilimanjaro.
Ayubu anasumbuliwa na tatizo la saratani ya
shingo, hivyo kusababisha shingo yake kuvimba na kumfanya ashindwe kutoa
sauti ipasavyo kwani sehemu kubwa ya koo lake imeziba.
Anaeleza kuwa kutokana na ugonjwa huo, kichwa nacho kinazidi kuvimba na kupata maumivu makali.
Macho nayo yanavimba na kumsababishia ashindwe
kuona mbali. Mbaya zaidi ni kwamba kwa namna anavyoona, kila siku
ugonjwa unaendelea kukua katika mwili wake.
Anasema ugonjwa huo umeshindikana kutibiwa katika hospitali za
kawaida hivyo anatakiwa aende kutibiwa Hospitali ya KCMC (Kilimanjaro
Christian Medical Centre).
Ayubu anatakiwa kuchomwa sindano sita, kila
sindano gharama yake Sh218,000, hivyo anatakiwa awe na Sh1,308,000 kwa
matibabu hayo pekee, nje ya tiba zingine, gharama za kuishi huko KCMC na
mengineyo.
Ugonjwa ulivyoanza
Alianza kuugua maradhi hayo mwaka 2010, ulianza
uvimbe mdogo shingoni, baadaye ukaongezeka, ikamlazimu kununua dawa za
kutuliza maumivu hasa Panadol, kwa vile uvimbe huo ulikuwa unasababisha
maumivu makali.
“Hali yangu ya kiafya inazidi kudhoofika, siwezi
tena kufanya kazi za kuniingizia kipato kwani maumivu ninayoyahisi ni
Mungu tu ndio anajua, ni maumivu makali mno. Ninaomba sana Watanzania
wenzangu na yeyote ambaye si Mtanzania anisaidie, nina mke na watoto
ambao bado wadogo na sina namna ya kuwasaidia kwa sasa”anasema.
“Wakati mwingine mwili wangu unakufa ganzi na
fahamu kupotea, wakati mwingine fahamu zinarudi naweza kujielewa vizuri,
ninachokisubiri kwa sasa ni huruma yenu Watanzania, ndiyo itasababisha
maisha yangu kurudi kama nilivyokuwa mwanzo”
Anasema watoto wake wanasoma lakini kwa sasa wamesimamishwa kwa sababu hana fedha za kuwalipia ada na huduma zingine za masomo.
Anasema alipokuwa hajaugua ugonjwa huo alikuwa
akifanya shughuli mbalimbali ndogo ndogo za kuingiza kipato, huku
akifanya pia kazi kama Mwalimu wa Kwaya katika Kanisa la KKKT kijijini
hapo. Kwa sasa hawezi tena kufanya kazi yoyote kwa sababu ya maumivu
makali anayohisi na pia hali ngumu ya kiafya inayoendelea kumsumbua.
“Nimeshawahi kwenda hospitali mbalimbali mkoani
hapa lakini hali haibadiliki, nilienda hadi kwa waganga wa kienyeji,
ugonjwa unaongezeka.
Hali yake kwa sasa ni mbaya, ndani ya dakika moja
naweza kujaza usaha kwenye kikombe, huku maumivu yakiendelea kuwa makali
zaidi.
Ayubu anasema ameendelea hivyo, mpaka alipokwenda
Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, ambako alishonwa ndipo angalau sasa
usaha umepungua, ingawa hali yake bado ni mbaya hasa shingo kuendelea
kuvimba.
“Mpaka sasa siwezi kugeuka nikitaka kugeuka
inabidi nigeuze mwili wote sio siri nateseka sana endapo maumivu haya
yangekuwa yanawezekana kumwachia mtu mwingine ningekupa ukaona maumivu
yake.
“Nina watoto wananitegemea, nilikuwa nalima na kufanya biashara
mbalimbali, kwa sasa siwezi kutokana na kupata maumivu makali ambayo
yananisababishia hata kushindwa kula”anasema Ayubu.
Maisha yake kwa sasa yamekuwa ya kubahatisha, kuna wakati hulala bila kula japo ni mgonjwa.
“Sisi Watanzania wote ni ndugu nihurumieni
mwenzenu naumia, naomba sana mnisaidie kulingana na ulichonacho,”anasema
Ayubu huku akitokwa machozi.
Kwa mujibu wa Ayubu, madaktari wamemshauri kwamba
akipata fedha hizo tatizo lake linaweza kutibiwa na kurudi katika hali
yake ya kawaida.
Kwa mujibu wa vitabu vitakatifu, kusaidia wenye
uhitaji huchangia kupata baraka katika maisha, lakini kama wanadamu
tunapaswa kusaidiana...duniani tunapita.
Kwa yeyote mwenye moyo wa kumsaidia chochote, Ayubu awasiliane na Mhariri wa Jarida la Ndani ya Habari, 0754498972.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI