Na Kalunde Jamal, Mwananchi
Posted Septemba21 2013 saa 13:15 PM
Posted Septemba21 2013 saa 13:15 PM
Kwa ufupi
Wiki iliyopita Amri Athumani ‘King Majuto’,
alizungumzia umaarufu wake Kenya na vijana wa sarakasi. Leo anazungumzia
familia yake. Endelea...
Majuto anasema kuwa ana watoto tisa ingawa
hakuwa tayari kuwazungumzia mama wa watoto hao zaidi ya kumwongelea
mkewe wa sasa, Aisha Mbwana kwa kuwa wake zake aliozaa nao baadhi ya
watoto kwa bahati mbaya walishafariki dunia.
Alisema kuwa yanapokuja masuala ya familia huwa
anapenda azungumze mkewe na kwa ridhaa yake. Kwa mujibu wa Majuto
anapenda aitwe mke halali kwa kuwa wake feki anao wengi kupitia michezo
ya kuigiza na wengine wenye fikira potofu hutumia picha hizo kutengeneza
habari za uongo.
Aisha anaizungumziaje familia yake
Kama kawaida ya wanawake wa Tanga ana lafudhi ya
huko ambayo huvutia kuzungumza nao, anaanza kwa kunieleza kuwa alianza
kuitwa mke halali wa nguli huyo wa sanaa za maigizo mwaka 1997,
walipofunga ndoa .
Anasema kuwa alikutana na nguli huyo maeneo ya
Buguruni, Dar es Salaam, ambako alikuwa akiishi na dada yake aliyekuwa
kaolewa na rafiki yake mzee Majuto, ‘Mwanachia’ (kwa sasa ni marehemu),
ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.
Anasema hakuwa na hili wala lile hadi alipoamua
kuondoka na kurudi kwao maeneo ya Vingunguti, ambako ndiko walikokuwa
wanaishi wazazi wake na kupewa taarifa kuwa posa imepelekwa kwa ajili
yake.
“Nilipoambiwa kuhusu hiyo posa sikufikiria kama
atakuwa ni mzee Majuto kwa kuwa alikuwa ni kama shemeji yangu kutokana
na kuwa karibu na shemeji yangu,” anasema Aisha ambaye ni mama wa watoto
watatu.
Anaendelea kueleza kuwa siku ambayo wanafamilia
walikutana na kumuuliza kama anamfahamu mchumba na kutajiwa jina kuwa ni
Amri Athumani, aliuliza mara mbili kwa kuwa alikuwa hamfahamu huyo mtu
hadi alipoambiwa kuwa ni King Majuto.
“Kwa mila za Wabondei mchumba wa kwanza
anakubaliana na wazazi, halafu binti anapewa taarifa na kwa kuwa wazazi
ni wakubwa inabidi binti akubali, na ndivyo ilivyokuwa kwangu nikakubali
na kuolewa na Majuto,” anasema mama huyo.
Anaingia kwenye uigizaji kufuata nyayo za mumewe
Aisha anafafanuwa kuwa kabla ya kuolewa na Majuto
hakuwa mwigizaji lakini baada ya kuolewa, mumewe huyo alimwingiza kwenye
uigizaji na filamu ya kwanza kuigiza na mumewe huyo ni ‘Fukara
hatabiriki’.
Mkewe huyo anasema kipindi hicho Majuto alikuwa
anafanya kazi bila kuwa na kikundi zaidi ya wanafamilia, hivyo na yeye
alikuwa mmoja wao akicheza kama mama na Majuto kama baba.
Anazungumziaje mafanikio yao
Katika kuashiria kuwa ni yeye alikuwa chachu ya mkewe kuwa
mwigizaji Majuto anaunga mkono kwa kusema kuwa; “kipindi filamu hiyo
inatoka hakukuwa na filamu kabisa na kama nilivyosema mwanzo kwa hapa
nyumbani inaweza kuwa ni moja ya zile za kwanza kabisa, hivyo niligundua
kipaji cha mke wangu kwa kumtazama tu, kwani hakuna ambako aliwahi
kujifunza kama sasa ambapo unaweza kutazama filamu mbili tatu ukajifunza
kitu, kwani wakati huo hata televisheni hatukuwa nayo, kwa kweli
alijitahidi,” anasema kwa msisitizo Majuto.
“Nilimjaribu nyumbani kama anaweza kuigiza filamu
fupi fupi akaweza, nikaona kwa nini nisifanye naye kazi kwa faida ya
familia na kupunguza kufanya kazi na watu wengi ambao watahitaji
niwalipe na wakati huo hakukuwa na fedha kama sasa,” anasema Majuto na
kuongeza kuwa:
“Alifanya vizuri hadi sikuamini kuwa kulikuwa na
kipaji nakipita hadi moyo wangu ulipodunda ndiyo nakigundua,” anasema
nguli huyo huku anacheka na kuchekesha kidogo kama kawaida yake.
Aisha anaongeza kuwa hakuishia hapo kwani alicheza
michezo zaidi ya 10, kabla ya kupumzika baada ya kupata ujauzito wa
mtoto wake wa kwanza mwaka 2000, ambapo baada ya hapo hakuwahi kufanya
kazi tena na mumewe zaidi ya ile ya ‘mazingira ya misitu’ na ‘mazingira
ya bahari’, ambayo zilikuwa ni filamu maalumu za kueleimisha kuhusu
kutunza misitu na bahari.
Anazungumziaje mafanikio yao
Anaendelea kueleza kuwa ameishi na mumewe huyo kwa
kazi hiyo ya uigizaji na hapo nyuma haamini jinsi ambavyo maisha
yalikuwa magumu, akilinganisha na jinsi ambavyo wamepiga hatua hivi
sasa.
Mkewe Majuto anasema kuwa anajivunia hatua
waliyopiga katika maisha hasa kutokana na kusota sana siku za nyuma,
kwani hata wakati wanajenga na mumewe nyumba hiyo hali haikuwa nzuri.
“Naamini maneno ya wahenga kuwa kujenga ni akili
na siyo mali, kwani nikikumbuka kipindi tunajenga nyumba hii hali
ilivyokuwa na sasa hali ilivyo naona tulitumia akili zaidi ya fedha,
kwani fedha alizokuwa anapata mume wangu zilikuwa ndogo ukilinganisha na
sasa,” anasema mama huyo.
Majuto anakubaliana na mkewe kwa kusema kuwa
uigizaji ulikuwa ni mgumu sana kipindi hicho na fedha ilikuwa ndogo,
tofauti na sasa kila kitu kipo lakini na fedha ipo, kibaya zaidi
waigizaji wenye vipaji kama wao hakuna.
Aisha anasema kuwa alipata mtoto wa kwanza mwaka
2001, aitwaye Bilali, ambaye anasoma darasa la sita, wa pili Halima
ambaye alimpata mwaka 2007 na wa tatu ni Rutifia aliyempata mwaka huu.
Ninataka kujua kama mzee Majuto bado anaendelea
kupata watoto zaidi ya hao kwa kuwa ukijumlisha na wengine atakuwa na
watoto tisa, “Wewe Mnyamwezi usiniletee wazimu nisimpe mimba kwa nini
wakati mke wangu bado binti na anahitaji watoto, nawahitaji na awalete
tu hadi waishe,” anajinasibu Majuto huku anacheka kwa nguvu.
Hata hivyo, Aisha anamwelezea mumewe huyo kuwa ni mpole na mkarimu anayependa watu.
Mafanikio
Anaendelea kueleza kuwa ukimtazama Majuto na mambo yake huwezi
amini kuwa ni baba bora na mkarimu kwa familia, na hana utani katika
mambo ya msingi.
Mkewe huyo anaeleza mafanikio yao ambayo anaamini
pamoja na mumewe kuwa mstari wa mbele kutafuta fedha, lakini yeye ana
mchango mkubwa.
Mafanikio
Anasema amepata mafanikio kiasi kutokana na kazi
ya mumewe na anachofanya ni kuhakikisha fedha yao haifanyi mambo yasiyo
ya lazima katika familia.
Mkewe huyo anafafanua kuwa kwakuwa hakuna
anayekunywa pombe wala kuvuta sigara, hakuna sababu ya kukosa maisha
mazuri na fedha za ziada.
Anayataja mafanikio kuwa ni kumuhimiza mumewe
kununua shamba kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya baadaye; “alinisikia
na tukanunua shamba la ekari 20 huko Muheza ambako tumeotesha mihogo,
mahindi na michungwa, ikiwemo ufugaji wa kuku 600, nikiwa ndiyo
msimamizi mkuu, na ninataka aniongezee cherehani katika kiwanda ambacho
kwa sasa zipo saba tu,” anasema Aisha.
Majuto anamalizia kwa kuwataja baadhi ya watoto
wake akianza na mwanawe wa kwanza aitwaye Athumani ambaye ana miaka 40,
Haruna, Omari, Yusuphu, Shafii, Hamza, na watoto wake watatu ambao
aliwapata akiwa na mkewe anayeishi naye sasa Aisha Mbwana, ni Bilali,
Halima na Rutifia.
Kwa kumalizia Majuto alitoa wito kwa vijana hasa
wasanii kwenda na kasi ya maisha kwa maana ya kuwekeza kwa ajili ya
maisha ya baadaye, kwa kuwa tasnia ya sanaa imekuwa na watu wengi, huku
wapya na wenye uwezo wakizaliwa kila siku.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI