Tuesday 10 September 2013

Nitawashughulikia mafisadi Tazara, asema Mwakyembe


          
 
Na Raymond Kaminyoge

Posted  Jumatatu,Septemba9  2013  saa 22:27 PM
Kwa ufupi
Asema wanasababisha wafanyabiashara kukimbia Tazara na kwenda kwa wenye malori ya kusafirishia shehena.


Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), kuweka mabango yanayoonyesha bei za kusafirisha mizigo, ili kudhibiti wizi.
Jana Dk Mwakyembe altaka kujua sababu ya nauli za abiria kuwa wazi , lakini bei za kusafirisha mizigo zinakuwa siri.
“Wekeni hadharani bei za mizigo kama ilivyo kwa nauli za abiria, huu usiri kwenye mizigo unatokana na wizi,” alisema waziri.
Alisema amepata taarifa kwamba baadhi ya watumishi wa Tazara na hasa katika idara ya mizigo, wamekuwa wakiwatoza wasafirishaji wa mizigo, bei kubwa kuliko bei zinazotozwa na wenye malori.
“Hii ni hujuma, wasafirishaji wengi wanaamua kutumia malori kwa sababu ya watumishi wezi, nitawashughulikia na sitavumilia kuiona Tazara ikifa,” alisema.
Dk Mwakyembe alisema atawashughulikia viongozi watakaopatikana na tuhuma mbalimbali za kifisadi katika mamlaka hiyo.
Alisema hayo baada ya wafanyakazi kumkabidhi nyaraka za ushahidi wa namna viongozi wa mamlaka hiyo wanavyoiba.
“Nyaraka hizi zitanisaidia kuchunguza viongozi wezi na kuwachukulia hatua endeleeni kunipa ushirikiano,”alisema.
Alimpa Mkurugenzi Mtendaji wa Tazara, Ronald Phiri, muda wa wiki mbili kuhamia katika nyumba ya mamlaka hiyo badala ya kuishi kwenye hoteli ya kitalii. Amekuwa akiishi hotelini tangu aje nchini

source: Mwananchi