Wednesday 18 September 2013

Operesheni wahamiaji haramu ipanue wigo

 
Posted  Jumatano,Septemba18  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Kutokana na utamaduni wa Serikali uliokuwa umezoeleka, kwa maana ya kutoa maagizo pasipo kusimamia utekelezaji wake, wahamiaji wengi walikaidi agizo la Serikali kwa kudhani mamlaka husika zisingekuwa na uthubutu na dhamira ya kuwarudisha makwao.


Operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu inayoendelea nchi nzima imeonyesha mafanikio makubwa mpaka sasa. Baada ya miaka mingi ya wahamiaji hao kuishi nchini kinyume cha sheria na kuifanya nchi yetu kuwa kama haina mwenyewe, sasa wameanza kutambua kwamba hakika Tanzania ina wenyewe na sasa imedhamiria kuhakikisha wageni wanaoingia nchini wanafanya hivyo kwa kufuata sheria za nchi.
Kwa hali yoyote ile, Serikali za awamu zote zilizotangulia zinastahili lawama kwa kulea tatizo hilo la wahamiaji haramu. Tatizo hilo halikuanza leo wala jana, bali lilianza baada ya nchi yetu kupata uhuru mwaka 1961, ambapo sera nzuri ya Serikali ya kuwaona Waafrika wote kama ndugu ilipotoshwa ama ilitafsiriwa vibaya na baadhi ya Waafrika wenzetu, hivyo kuingia nchini kutoka kila pembe ya Afrika pasipo kufuata taratibu. Matokeo yake ni usalama wa taifa kuwekwa rehani kwa kuachia mipaka yetu kuvuja kirahisi kwa namna ambayo ni vigumu kuielezea.
Matokeo yake ni Watanzania wenzetu wanaoishi katika mikoa ya mipakani kulazimishwa kuishi kama mateka au wakimbizi katika nchi yao. Wahamiaji hao haramu pamoja na wengine wengi walioitwa wakimbizi kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi zao, waliifanya Tanzania kama kimbilio pekee katika pembe hii ya dunia. Muda si mrefu tulianza kushuhudia kuzorota kwa hali ya usalama kutokana na kushamiri kwa vitendo vya uhalifu kama mauaji, utekaji wa magari na kuzagaa kwa silaha za kila aina. Uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji uliongezeka kwa kasi ya kutisha na kuleta njaa na hata kusababisha baadhi ya watu kupoteza maisha.
Ni jambo la kupongeza kwamba agizo la Rais Jakaya Kikwete limetekelezwa kwa ufanisi mkubwa, aliposema wahamiaji haramu warudi makwao kwa hiari, vinginevyo ifanywe operesheni maalumu ya kuwarudisha makwao kwa nguvu. Ni kweli wakimbizi wapatao 14,000 walirudi makwao kwa hiari, lakini wenzao wengi walikaidi agizo hilo na kujibana kwa wenyeji na sehemu nyingine, yakiwamo mapori.
Kutokana na utamaduni wa Serikali uliokuwa umezoeleka, kwa maana ya kutoa maagizo pasipo kusimamia utekelezaji wake, wahamiaji wengi walikaidi agizo la Serikali kwa kudhani mamlaka husika zisingekuwa na uthubutu na dhamira ya kuwarudisha makwao. Hivyo, operesheni hiyo ilipoanza walitaharuki na kukumbwa na hali ya sintofahamu, huku wakitapatapa mithili ya mtu anayekumbuka shuka kukiwa tayari kumekucha.
Ndio maana kimbunga cha operesheni hiyo inayoendelea kwa kasi hivi sasa kimewanasa wahamiaji wengi wa kila aina. Taarifa zinasema wamenaswa wachungaji, walimu, wafanyabiashara na wafanyakazi wengi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika waliokuwa katika ajira mbalimbali kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na walioajiriwa katika sehemu nyeti kama Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere wa Dar es Salaam, maofisini na viwandani. Operesheni hiyo pia imewatia mbaroni Watanzania waliokamatwa wakiwa wamewaficha majumbani mwao wahamiaji hao haramu.
Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kuendesha operesheni hiyo kwa ufanisi mkubwa, tungependa kuitahadharisha kwamba wahamiaji haramu hawatoki nchi za Afrika pekee, bali pia nchi za Bara la Asia, zikiwamo China, India, Pakistan na nyinginezo. Tunatahadhalisha pia kwamba operesheni hiyo ifanywe kwa uadilifu, busara na hekima bila kuendekeza vitendo vya rushwa, ubaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu.

SOURCE: MWANACHI