Kwa ufupi
Msangi alikamatwa juzi mchana kwenye Mgahawa wa
Didi’s, Masaki Dar es Salaam baada ya chanzo kimojawapo cha habari
kueleza kuwepo kwa promota huyo katika mgahawa huo.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi
linamshikilia kwa mahojiano Promota wa Ngumi za kulipwa kati ya Francis
Cheka na Phil Williams kutoka Marekani, Jay Msangi akituhumiwa kushindwa
kumlipa bondia wa Marekani Sh12 milioni.
Cheka na Williams walizikunja mwishoni mwa wiki
iliyopita kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee katika pambamo la kuwania
Ubingwa wa Dunia (WBF), ambapo Cheka alishinda kwa pointi 3-0.
Msangi alikamatwa juzi mchana kwenye Mgahawa wa
Didi’s, Masaki Dar es Salaam baada ya chanzo kimojawapo cha habari
kueleza kuwepo kwa promota huyo katika mgahawa huo.
Promota huyo anadaiwa kuondoka katika mazingira ya kutatanisha usiku, muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Marietha Minagi
alipopigiwa simu kuthibitisha kukamatwa kwa promota huyo, hakuwa tayari
kuzungumza zaidi ya kutaka aulizwe Ofisa wa Polisi aliyemtaja kwa jina
moja la Msangi.
Hata hivyo, alipotafutwa Msangi kwa namba za simu alizotoa msemaji huyo wa polisi hakupatikana.
Mmoja kati ya watu waliomsaidia promota huyo
kuandaa pambano hilo, Catherine Metili aliliambia Mwananchi kuwa bondia
wa Marekani alipaswa kulipwa pesa zake siku moja kabla ya pambano,
lakini hilo halikufanyika.
Mwananchi lilishuhudia promota huyo akiondolewa
katika mgahawa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi akiwa na makachero
kadhaa wa polisi. Kukamatwa kwa mtuhumiwa kulitokea baada ya mazungmzo
marefu na Mkurugenzi wa Baraza la Michezo, Leonard Thadeo.
Thadeo alifika kwenye mgahawa huo baada ya kupata
taarifa za kuwepo kwa Msangi na kufanya naye mazungumzo yaliyochukua
zaidi ya nusu saa kabla, polisi kufika na kumtia nguvuni.
Habari za ndani zinasema kuwa, promota alikuwa
mikononi mwa polisi mpaka jana. Inadaiwa kuwa, kabla ya pambano la juzi
baadhi ya mabondia waligoma kupanda ulingoni wakishinikiza kulipwa.
source: Mwananchi
source: Mwananchi